Wakati Watanzania
wakijiandaa kusherehekea sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya, viongozi wa
dini wameeleza mambo manne yanayopaswa kuchukuliwa tahadhari na jamii
mwaka 2018.
Wameyataja mambo hayo kuwa ni ukiukwaji wa haki za binadamu, uhalifu,
ubaguzi; na uvunjifu wa amani wakibainisha kuwa yalichukua nafasi kubwa
mwaka huu.
Viongozi hao wametaka yadhibitiwe ili yasijitokeze tena mwakani. Kwa
waumini wa Kikristo, huenda huo ukawa ndio ujumbe utakaotolewa kwa
waumini katika ibada hizo za sikukuu za mwisho mwa mwaka.
Katibu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Raymond Saba
alisema matukio ya uvunjifu wa amani mwaka huu yalikuwa tishio, hivyo
ni muda sahihi wa Watanzania kujifunza namna ya kulinda tunu ya Taifa.
“Amani ndiyo kila kitu, amani ikitoweka hakuna malengo yoyote
yatakayotekelezwa, kwa hiyo jamii ijitafakari katika kipindi hiki
kuhakikisha amani inadumu, matukio ya wizi, utapeli yatoweke kabisa
katika jamii,” alisema.
Rais wa Baraza hilo, Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa alisema jamii
inatakiwa kujenga utamaduni wa kulinda amani ya nchi, kutenda haki na
kuhimiza upendo.
“Tunaelekea kwenye Krismasi tujali haki, tujali amani ya nchi yetu na
upendo. Tumwombe Mungu atuongoze zaidi katika kipindi hiki, atusaidie
katika kilimo chetu kwa sababu mvua haijaanza kunyesha,” alisema.
Msemaji wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Rajab Katimba
aliwataka Watanzania kujitathmini na kutenda haki ili mwaka ujao uwe wa
amani na kila mwananchi ajisikie huru kuishi katika nchi yake.
Alibainisha kuwa, mwaka huu umekuwa na matukio mengi ambayo yanaonyesha ukiukwaji wa haki za binadamu.
Aliyataja baadhi ya matukio hayo kuwa ni mauaji, baadhi ya watu kufungwa
bila hatia na wengine kutoweka katika mazingira ya kutatanisha.
“Tumeshuhudia matukio ya kuokotwa kwa miili ya watu kwenye fukwe za
Bahari ya Hindi na watu kupotea. Hivi ninavyoongea kuna mwandishi mmoja
(Azory Gwanda) naye amepotea. Tunataka viongozi wahakikishe haki
inatendeka katika Taifa hili,” alisisitiza.
Kiongozi huyo ametaka Jeshi la Polisi kufanya kazi kwa weledi ili
kulinda haki za Watanzania na hasa wanyonge wasio na sauti, akisisitiza
haki ndiyo msingi wa maendeleo ya Taifa lolote duniani.
“Bila haki Taifa linakufa. Uwanja wa siasa nao uwe huru ili vyama vya
upinzani navyo vipate haki ya kufanya siasa kwa mujibu wa sheria na
Katiba,” alisema.
Kwa mtazamo wake, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana, Jacob Chimeledya
alisema sasa ni wakati wa kila Mtanzania kutambua thamani ya mtoto na
kumlinda ili akue katika njia iliyo bora na baadaye kuwa msaada kwa
Taifa.
Dk Chimeledya alimtaka kila mwananchi kuangalia namna atakavyogusa
maisha ya mtoto kwa kila anachokifanya ili kumjengea mustakabali mwema
kimaadili, kielimu na kimaendeleo.
“Maisha ya mtoto ni tunu kwa Taifa, hivyo akitunzwa ana faida kubwa
baadaye. Mungu amepandikiza karama na vipawa kwa kila mtoto, kama
hakutunzwa vizuri basi anapoteza karama na vipawa hivyo,” alisema.
Aliwataka wazazi na walezi kutimiza wajibu wa kutunza watoto wao katika misingi ya haki, imani na maadili ya Taifa.
Akiuzungumzia mwaka huu, Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa
Salum alisema umekuwa na changamoto nyingi kwa sababu wananchi
hawakuzoea kuona yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, ikiwamo
matumizi mazuri ya rasilimali.
Alisema ni wakati wa wananchi kujipanga kuijenga nchi iwe yenye
kujitegemea, isiyoyumbishwa na mataifa mengine na kulinda rasilimali za
nchi kwa manufaa yao wenyewe, “Tujenge nchi yetu kwa pamoja maana nchi
hii ni yetu sote. Tujenge umoja wa kitaifa, wanadini na wanasiasa
tujenge utamaduni wa kuvumiliana,” alisema.
Kuhusu haki za binadamu alisema, “Watanzania hawapati maelezo ya kutosha
kwa mambo kadhaa kama vile miili ya watu inayookotwa fukweni na wengine
kutoweka. Hatutarajii kuendelea na hali hiyo mwaka ujao.”
Mchungaji wa Kanisa la Maombezi, Anthony Lusekelo alisema, “Ubaguzi ni
mbaya watu wanapaswa kuheshimu sheria na Katiba ya nchi, tunapaswa
kuishi vyema bila kujali tofauti zetu za kisiasa na kidini.” alisema.
0 comments: