Tume
ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imethibitisha kumtoa kwenye kinyang’anyiro
cha ubunge Singida Kaskazini mgombea kwa tiketi ya Chadema, David
Djumbe.
Mgombea huyo ameondolewa kwenye orodha baada ya kutimiza masharti ya kujitoa katika uchaguzi kwa mujibu wa sheria.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Ramadhan Kailima alisema jana kuwa Djumbe alifuata maelekezo kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi.
“Kama
Sheria inavyosema Kifungu cha 49(1)(2) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi,
Sura 343 mgombea anaweza kujitoa kwa kuandika barua na kuisaini yeye
mwenyewe pamoja na ahadi ya kiapo cha sheria alichoapa mbele ya hakimu.
“Tume
haimkubalii wala haimkatalii sababu ni hiari yake. Amewasilisha taarifa
hizo na Tume imemfuta katika orodha ya wagombea,” alisema Kailima
alipoulizwa jana kuhusu hatima ya mgombea huyo.
Desemba
20, Djumbe aliwasilisha nyaraka za kujitoa katika uchaguzi huo
uliopangwa kufanyika Januari 13 mwakani akieleza kuwa jina lake
lilipelekwa kimakosa.
Mkanganyiko
ndani ya Chadema ndiyo uliosababisha jina la Djumbe kupelekwa NEC na
kupitishwa kuwa mgombea ubunge Singida Kaskazini.
Wakati
Chadema ngazi ya Taifa ikisema haitashiriki katika uchaguzi huo mpaka
NEC itakapokutana na wadau kujadili changamoto zilizojitokeza katika
uchaguzi wa udiwani katika kata 43, uongozi wa chama hicho mkoani
Singida ulipeleka Tume jina la Djumbe kuwa mgombea.
Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Singida, Shaban Limu alisema Djumbe aliteuliwa kugombea na kamati ya utendaji ya wilaya.
Alisema wakati anateuliwa uongozi wilaya na mkoa ulikuwa haujawasiliana na makao makuu kujua msimamo juu ya uchaguzi huo.
Jimbo
la Singida Kaskazini liko wazi baada ya aliyekuwa mbunge kwa tiketi ya
CCM, Lazaro Nyalandu kujivua uanachama wa chama hicho hivyo kupoteza
nyadhifa zote ukiwamo ubunge. Alijiunga na Chadema.
Uchaguzi
pia unafanyika katika majimbo ya Longido ambako matokeo ya uchaguzi wa
ubunge ya mwaka 2015 yalibatilishwa na Mahakama; na Songea Mjini ambako
aliyekuwa mbunge kwa tiketi ya CCM, Leonidas Gama alifariki dunia.
0 comments: