Balozi wa Misri katika Umoja wa mataifa Abdellatif Aboulatta.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatafakari kupitisha mswada
unaosema mabadiliko yoyote ya hadhi ya mji wa Jerusalem hayatakuwa
na athari kisheria na yanapaswa kubadilishwa.
Misri imesambaza mswada huo Jumamosi (16.12.2017), na
wanadiplomasia wamesema baraza huenda likapiga kura kuhusiana na
mapendekezo hayo mapema hata Jumatatu.Akijitoa katika mwelekeo wa kimataifa , rais wa Marekani Donald Trump mwezi huu alitangaza kwamba atautambua mji wa Jerusalem katika mji mkuu wa Israel na kuhamishia ubalozi wa Marekani katika mji huo kutoka Tel Aviv, hatua hiyo imezusha maandamano na shutuma kali.
Mswada huo wa azimio uliopatikana na shirika la habari la AFP unasisitiza kwamba Jerusalem ni suala , "ambalo linaamuliwa kupitia majadiliano" na kueleza "masikitiko makubwa katika uamuzi wa hivi karibuni kuhusiana na hadhi ya mji wa Jerusalem," bila kutaja moja kwa moja uamuzi wa rais Trump.
"Uamuzi wowote na hatua ambazo zitaonekana kubadilisha hadhi, hali na jamii iliyopo katika mji huo mtakatifu wa Jerusalem havitakuwa na athari ya kisheria, na ni batili na ni lazima ubadilishwe," mswada huo umesema.
Wanadiplomasia wanasema wanatarajia Marekani kutumia uwezo wake wa kura ya turufu kuzuwia hatua hiyo wakati , wengi kama sio wote , wajumbe 14 wa baraza la Usalama wanatarajia kuunga mkono mswada huo wa azimio. (DW SWAHILI)
0 comments: