WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Kanda ya Kusini, Bw. Ogesa Charles Tale afike eneo la mgodi wa dhahabu wa Namumgo na kuitisha kikao cha wananchi leo (Jumapili) saa 4 asubuhi.
“Sasa hivi natoka kwenda Matambare, twende wote, lakini kesho (leo) saa 4 asubuhi uje hapa Namungo, uitishe mkutano wa hadhara na uwasikilize hawa wachimbaji wadogo na kisha uniletee maelezo ofisini kwangu,” alisema.
Ametoa agizo hilo jana mchana (Jumamosi, Desemba 30, 2017), wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Namungo, wilayani Ruangwa baada ya kupokea mabango mawili kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo. Waziri Mkuu yuko kwenye mapumziko ya mwisho wa mwaka, na ameamua kukagua miradi ya maji, ujenzi wa zahanati na kuzungumza na wananchi katika wilaya hii.
Waziri Mkuu alisema Serikali ya awamu ya tano imejikita kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi na alipomuuliza afisa huyo kama ameshawahi kupata nafasi ya kuwasikiliza wachimbaji wadogo, alijibiwa kwamba hajawahi kufanya hivyo.
“Hawa ndiyo nguvukazi ya mgodi, hawa ndiyo wanaingia kule chini kuchimba udongo, hawa ndiyo wanapata machungu ya kazi ya uchimbaji, kwa hiyo uje uwasikilize na uniletee taarifa kesho mchana,” alisisitiza.
Baada ya kuyasoma mabango yao, Waziri Mkuu aliwaita wakazi ambao waliyaleta mabango hayo na kuwataka waeleze kwa undani ni matatizo gani yanayowakabili. Bango la kwanza lilisema wananchi wananyanyaswa na viongozi kwa maslahi binafsi ya viongozi na la pili lilisema wamekatazwa wasiseme matatizo yao kwenye mkutano huo wa Waziri Mkuu.
Mkazi wa kijiji cha Mtondo, kata ya Nambilanje, Bw. Mussa Omari Kimatilo, alisema wananyanyaswa na uongozi wa kijiji pamoja na uongozi wa wenye machimbo ya dhahabu na kwamba wananyimwa uhuru wa kujieleza kila wanapokutana na viongozi hao.
“Tunanyanyaswa na uongozi wa machimbo, tunanyanyaswa na uongozi wa kijiji na tukilalamika hakuna wa kutusikiliza. Tumekaa na Rajani (mmiliki wa mgodi) amekubali kutulipa lakini wananchi hatuna uhuru wa kujieleza,” alisema.
Alidai hata Naibu Waziri wa Madini alipotembelea mgodi huo mapema mwezi huu, hakupewa fursa ya kukutana na wachimabji wadogo, na badala yake alipitishwa kijijini hapo na kuingizwa mgodini kisha akaondoka.
Naye Bahati Mikael, mkazi wa kijiji cha Namungo alisema kumekuwa na ukiritimba wa kutoa leseni kuhusu mgodi huo na kwamba tangu ilipotolewa rasmi mwaka 2014, bado hawajalipwa malipo yao.
“Hapa pana ukiritimba wa kutoa leseni ya uchimbaji. Mwekezaji amekuwa akichimba kinyemela; tangu mwaka 2006 alikuwa hajapewa leseni hadi mwaka 2014 ndipo alipopewa,” alisema.
Alipoitwa na Waziri Mkuu atoe ufafanuzi juu ya madai ya wakazi hao, Kaimu Afisa Madini wa kanda hiyo alisema eneo wanalodai wakazi hao ni la Mzee Kishor Rajani na inaeleweka hivyo na kwamba miaka ya nyuma walichimba kwa maelewano tu bila mikataba yoyote.
“Yale ya nyuma yalishapita kwa sababu hamkuwa na mkataba naye, mlifanya naye kazi kwa makubaliano ya mdomo tu. Sasa hivi mmeanza kuwekeana mikataba, zamani alikuwa anachukua asilimia kubwa lakini sasa hivi anachukua asilimia 17.5 na inayobaki amewaachia ninyi,” alisema Bw. Tale.
Waziri Mkuu anaendelea na ziara ya jimboni kwake.
0 comments: