Wednesday, 27 December 2017

Marais Afrika Nzima Kukutana January Kwa Ajili ya Mageuzi Makubwa




Wakuu wa nchi na Serikali za Afrika, wakiwemo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), mapema mwakani wanatarajiwa kusaini makubaliano ya kuanzishwa kwa eneo huru la biashara la bara hilo (CFTA).

Wanatarajiwa kuwa na mkutano wa 30 wa kawaida Januari 28 na 29 mwakani katika ukumbi wa Nelson Mandela uliopo kwenye Kituo kipya cha Mikutano (AUC) jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Mkutano huo utakaokuwa nakaulimbiu; “Kushinda Vita Dhidi ya Rushwa: Mwelekeo Endelevu wa Mabadiliko Afrika,” utatanguliwa na mkutano wa 35 wa Kamati ya Wawakilishi wa Kudumu (Januari 22-23) na mkutano wa 32 wa kawaida wa Baraza la Utendaji (Januari 25-26).

CFTA itakuwa soko la zaidi ya watu bilioni 1.3 na wanatarajiwa kufika takribani bilioni mbili ifikapo mwaka 2025. Yatakaposainiwa, makubaliano hayo ya kibiashara yatakuwa makubwa zaidi barani humo yakizihusu nchi zote 54 za Afrika, na yatakuwa ya pili kwa ukubwa duniani. Makubaliano makubwa zaidi duniani ni ya Shirika la Biashara la Dunia (WTO) yaliyosainiwa mwaka 1994.

Kwa sasa Afrika ina masoko mawili makubwa yanayozihusu baadhi ya nchi, ikiwemo Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA).

EAC yenye nchi sita wanachama za Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini, Tanzania na Kenya, ina zaidi ya watu milioni 170. Mkutano wa 18 wa kawaida wa wakuu wa nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia Januari 2012, uliamua kuwa hadi mwaka 2017 CFTA iwe imeanzishwa. Majadiliano kuhusu uanzishwaji huo yalianza rasmi Juni 2015.

Juni mwaka huohuo, wakati wa mkutano wa 25 wa wakuu wa nchi za AU uliofanyika Afrika Kusini, viongozi hao walikubaliana lianzishwe eneo huru la biashara ifikapo mwaka 2017 kupitia makubaliano na biashara huria za bidhaa na huduma.

Kwenye mkutano wa nne wa mawaziri wa biashara kutoka nchi za Afrika, uliofanyika hivi karibuni Niamey, Niger viongozi hao waliidhinisha muundo wa makubaliano na kuzingatia maendeleo, yaliyofikiwa kwenye majadiliano ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mkutano ujao wa wakuu wa nchi na serikali. CFTA itatoa uhakika wa mazingira ya uwekezaji, maendeleo ya viwanda na ongezeko la thamani ya bidhaa na huduma, hivyo kutengeneza fursa za ajira na vipato vya familia.

Hivi karibuni, wakati anafungua mkutano wa mawaziri mjini Niamey, Rais wa Jamhuri ya Niger Issoufou Mahamadou alipongeza maendeleo yaliyofikiwa katika majadiliano kuhusu makubaliano hayo.

CFTA na makubaliano mengine yakiwemo ya Kuharakisha Maendeleo ya Viwanda Afrika (AIDA), Programu ya Maendeleo ya Kilimo Afrika (CAADP), Mpango wa Programu ya Maendeleo ya Miundombinu Afrika (PIDA) vitaiwezesha Afrika kufanikiwa katika malengo ya mabadiliko.

Makubaliano ya kuanzisha eneo huru la biashara Afrika, yanaweka ajenda kwa ajili ya mijadala kuhusu biashara ya bidhaa, biashara ya huduma na utatuzi wa migogoro. CFTA itashughulikia itifaki mbili, ikiwemo ya biashara ya bidhaa na itifaki ya biashara ya huduma. Makubaliano hayo yanatarajiwa kuboresha biashara baina ya nchi za Afrika.

Malengo makuu ya CFTA ni kuiwezesha Afrika kuwa na soko moja la bidhaa na huduma, litakalotoa uhuru kwa wafanyabiashara na uwekezaji na hivyo kutoa fursa ya kuongeza kasi ya kuanzisha umoja wa forodha barani humu.

0 comments: