Saturday, 23 December 2017

Wataka JPM aunde tume kuchunguza ubinafsishaji sakata la Airtel

Sakata la hisa za Kampuni ya Airtel limeendelea kuchukua sura mpya baada ya Rais John Magufuli kushauriwa aunde tume huru ya kuchunguza ubinafsishaji uliofanyika ili watakaobainika wachukuliwe hatua kali.

Ushauri huo kutoka kwa wanasiasa umekuja siku mbili tangu mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Omary Nundu na menejimenti yake kuzungumza na wanahabari na kuitaka Airtel kurejeshwa TTCL na si vinginevyo.

Hata hivyo, kampuni ya Bharti Airtel inayomiliki hisa nyingi za kampuni hiyo ya mawasiliano ya simu imetoa tamko ikieleza kuwa uwekezaji wake ulifuata na kuzingatia sheria na taratibu kabla haujapata baraka zote za Serikali ya Tanzania.

Jana, kwa nyakati tofauti, Kiongozi wa Chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe, waziri kivuli wa Fedha na Mipango, Halima Mdee na kada mpya wa CCM, David Kafulila walisema kuundwa kwa tume huru kutahitimisha mjadala na ukweli kujulikana.

Desemba 20, Rais Magufuli alimuagiza Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kufuatilia utata uliopo kwenye umiliki wa Airtel akisema ni mali ya Serikali.

Zitto ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Mjini alisema kunahitajika kutazamwa mchakato mzima wa ubinafsishaji kwa kufanya ukaguzi maalumu wa sera ili kutoa mapendekezo ya kurekebisha makosa yaliyofanyika kwani jambo hilo linaweza kuzaa matunda mazuri zaidi. Alisema Serikali inaweza kuunda tume kutazama namna ubinafsishaji ulivyofanyika na kuchukua hatua za kisayansi baada ya matokeo ya kazi hiyo huku akidokeza kwamba akiwa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) walifanyia kazi sera ya ubinafsishaji.

“Katika kila taarifa yetu ya mwaka tulikuwa na sehemu maalumu iliyoeleza ufuatiliaji wetu wa utekelezaji wa sera ya ubinafsishaji,” alisema Zitto kupitia taarifa yake kwa umma aliyoitoa jana.

Zitto alisema ubinafsishaji wa TTCL ni suala walilolitolea taarifa mara kadhaa bungeni na ya mwisho ilikuwa Januari 2015.

“Ni ukweli usio na shaka kuwa kampuni ya Celtel (sasa Airtel) haikulipa chochote kuwezesha kumiliki hisa kwenye Celtel Tanzania na pia uuzwaji wa Celtel kwenda Zain na kisha Airtel, ulisababisha Tanzania kupoteza mapato ya kodi ya ongezeko la mtaji (capital gains tax),” alisema.

Hata hivyo, alisema kunahitajika kushughulikia suala la Airtel kwa muktadha wa kazi nzima ya ubinafsishaji nchini.

Zitto alisema PAC iliagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya uchunguzi baada ya ubinafsishaji wa mashirika kadhaa, ikiwamo Benki ya NBC na matokeo waliyawasilisha bungeni.

“Uuzwaji wa NBC nao ulikuwa ni wa bure na huwezi kushughulika na kampuni mojamoja bila kutazama muktadha mzima wa ubinafsishaji wa mashirika ya umma,” alisema Zitto anaungwa mkono na Mdee ambaye pia ni mbunge wa Kawe (Chadema) aliyesema suala la Airtel si jipya kwani iliuzwa kinyemela na walioiuza walilindwa hivyo umefika wakati wakawekwa hadharani.

“Kama dhamira ni kutaka kuanza kufanyia kazi kilichopigiwa kelele na kambi rasmi ya upinzani bungeni na iliyokuwa kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma ni rahisi sana,” alisema na kuongeza, “Wote waliokuwa na dhamana ama katika shirika au wizara ambayo TTCL ilikuwa chini yake ambao kwa namna moja au nyingine walishiriki katika mchakato huo wawekwe wazi na hatua zichukuliwe.”

Alisisitiza, “Mkataba wa mauzo uwekwe wazi ijulikane masilahi ya pande zote yalikuwa nini? Nani alipata au kukosa nini na kwa sababu gani na nani aliyesababisha hasara husika na kwa masilahi ya nani? Tunataka Watanzania wajue mbivu na mbichi kwa hoja zilizo mezani na sio kwa matamko.”

Kafulila ambaye ni mbunge wa zamani wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi) alisema, “Kuirudisha mali ni jambo moja na dogo, lakini waliosababisha hasara au kupindishwa kwa sheria na taratibu wanapaswa kujulikana.”

“Mimi nashauri iundwe kamati, Rais (Magufuli) aunde tume au kama Rais atashindwa, basi Waziri Mpango aunde kamati na yeye kama atashindwa basi Bunge liunde kamati teule ili kuchunguza kuanzia Celtel hadi Airtel.”

Kafulila alitolea mfano kamati iliyoundwa na aliyewahi kuwa waziri wa uchukuzi, Samuel Sitta (marehemu) kuchunguza mabehewa mabovu mwaka 2015.

“Ingawa ripoti yake haikusomwa bungeni lakini ilibaini wahusika na ndiyo hii ya Airtel na TTCL. Iundwe kamati ichunguze na ije na ukweli ili waliohusika wachukuliwe hatua,” alisema.

0 comments: