TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imetoa uamuzi wa kuitupa rufaa
iliyowasilishwa na mgombea ubunge Jimbo la Singida Kaskazini kupitia
Chama cha AFP.
Mgombea huyo alikuwa akipinga uamuzi wa Msimamizi wa Uchaguzi ngazi ya
jimbo dhidi ya pingamizi alilomwekea mgombea wa Chama Cha
Mapinduzi(CCM).
Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC) Ramadhan Kailima amesema
leo jijini Dar es Salaam kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari.
Kailima kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 40(6) cha Sheria ya Taifa
ya Uchaguzi, Sura ya 343 ikisomwa pamoja na Kanuni za 34 na 35 za
Kanuni za uchaguzi wa Rais na Wabunge za mwaka 2015, NEC ilipokea rufaa
moja kutoka kwa mgombea wa ubunge jimbo la Singida Kaskazini.
Pia NEC ilipokea rufaa mbili, ya kwanza iliwasilishwa na mgombea wa
udiwani Kata Keza – Halmashauri ya Wilaya Ngara kwa tiketi ya CCM
akipinga uamuzi wa Msimamizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo dhidi ya
pingamizi alilomwekea mgombea wa NCCR - Mageuzi.
Wakati rufaa ya pili ilitoka kwa mgombea wa udiwani Kata ya Kwagunda
katika Halmashauri ya Wilaya Korogwe kwa tiketi ya CCM akipinga aumuzi
wa Msimamizi wa Uchaguzi ngazi ya jimbo dhidi ya pingamizi alilomuwekea
mgombea wa Chama cha Wananchi(CUF.
Kailima amefafanua kwenye kikao chake cha kawaida kilichofanyika Desemba
24, mwaka huu, NEC ilipitia rufaa hizo na kutoa uamuzi. Akizungumzia
rufaa ya mgombea ubunge,NEC imekubaliana na uamuzi ya Msimamizi wa
Uchaguzi,hivyo mgombea aliyekatiwa rufaa aendelee kuwa mgombea wa ubunge
jimbo la Singida Kaskazini.
Amesema kuhsu rufaa za wagombea udiwani kata ya Keza na Kwagunda, NEC
imekubaliana na uamuzi wa Wasimamizi wa Uchaguzi. “Hivyo wagombea
udiwani waliokatiwa rufaa waendelee kuwa wagombea wa udiwani katika kata
husika,”amsema Kailima.
Ametumia nafasi hiyo kueleza tayari NEC imetuma taarifa ya uamuzi huo
kwa Wasimamizi wa Uchaguzi ili watoe taarifa kwa wahusika kuhusu
kilichoamriwa.
0 comments: