Monday 18 December 2017

Mwenyekiti wa CCM kuchaguliwa leo

Mkutano mkuu wa Taifa wa Chama cha Mapinduzi nchini Tanzania unaanza leo mjini Dodoma ukiwa na lengo la kumchagua Mwenyekiti wa Chama na Makamu wake wawili kutoka Tanzania bara na Zanzibar.
Chama hicho kinaendeleza mkakati wa kurejesha hadhi yake baada ya kishindo cha uchaguzi wa mwaka 2015. Licha ya kushinda urais kwa tabu, wapinzani chini ya mwamvuli wa UKAWA walipata karibu theluthi moja ya viti vyote vya ubunge na kudhibiti halmashauri katika miji muhimu ikiwemo Dar es Salaam, hii ikiwa ni rekodi mpya.
Miaka miwili ndani ya utawala wa Rais Magufuli, upepo unaonekana kugeuka. Upinzani unaelekea kudhoofika, wakati CCM ikiimarika.
Hata hivyo, kwa upande mwingine, hadhi ya CCM inarejea kwa gharama kubwa kwa demokrasia changa ya Tanzania. Katika siku za hivi karibuni madiwani na wabunge wa upinzani wameshuhudiwa wakihama vyama vyao kwa madai kuwa Rais Magufuli anafanya kazi nzuri. Kwa upande wake, upinzani unadai rushwa imekuwa ikitumika kuwashawishi wahamie CCM.
Wakati huo huo, Rais Magufuli amekuja na maagizo mapya juu ya namna ya kufanya siasa. Hakutakuwa tena na mikutano ya siasa ya hadhara mpaka wakati wa chaguzi isipokuwa kwa wabunge na madiwani katika maeneo yao. Wakati huo huo, Rais Magufuli mwenyewe anafanya mikutano kama kawaida akichanganya shughuli za chama na serikali.
Aidha, viongozi wa upinzani wamejikuta matatani wakikamatwa na kushtakiwa kwa uchochezi pale wanapotoa matamshi mbalimbali, huku wengine wakihofia usalama wao kwa madai ya kupokea vitisho.(BBC SWAHILI)

0 comments: