Monday 18 December 2017

AJALI yaua Watano Mwanza

 Kamanda wa Polis mkoa, Ahmed Msangi.

WATU watano wamefariki dunia na wengine 13 kujeruhiwa kwa ajali iliyohusisha magari mawili yaliyogongana wilayani Nyamagana jijini hapa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Ahmed Msangi alisema jana kuwa tukio hilo la kusikitisha lilitokea Desemba 16 mwaka huu majira ya saa moja na nusu usiku katika barabara ya Mwanza- Shinyanga Mtaa/Kata ya Buhongwa.
Alisema ajali hiyo ilihusisha gari lenye namba za usajili T 107 BKK Toyota Coaster mali ya Kampuni ya Auki wa Mwanza iliyokuwa ikiendeshwa na dreva Badru Habibu (33) mkazi wa Nyegezi jijini Mwanza lililokuwa likitoka Geita kwenda jijini Mwanza ambalo liligongana na gari lenye namba za usajili T 504BZB lori- Scania lenye tela namba T 880 ASA lililokuwa likiendeshwa na Salim Omary (28) mkazi wa jijini Dar es Salaam.
“Lori hilo lilikuwa likitokea jijini Mwanza kwenda jijini Dar es Salaam na kusababisha vifo kwa watu watano na majeruhi 13 abiria wote waliokuwa kwenye Toyota Coaster,” alisema. Alisema hadi sasa mtu ambaye ametambuliwa katika ajali hiyo ni Abdul Mustafa mwenye umri kati ya 45 na 50 ili hali ya marehemu wengine wanne majina yao bado hayajafahamika hadi sasa na majeruhi wote 13 wamelazwa katika hosipitali ya rufaa ya Bugando kwa ajili ya kupatiwa matibabu na hali zao zinaendelea vizuri.
Alisema miili ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali ya Bugando kwa ajili ya uchunguzi na utambuzi, ambapo alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi wa dreva wa gari la Toyota Coaster aliyejaribu kuyapita magari mengine yaliyokuwa mbele yake bila kuchukua tahadhari na kusababisha ajali hiyo.
Alisema madereva waliosababisha ajali hiyo wamekamatwa na wanahojiwa na polisi na uchunguzi utakapokamilika watafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria. “Nitoe wito kwa madereva wawe makini wanapokuwa barabarani na wazingatie sheria za usalama barabarani,” alisema na kuwataka abiria kutoa taarifa polisi kuhusu madreva wanaovunja sheria za usalama barabarani. Aidha amewaomba wananchi kwenda katika hosipitali ya rufaa ya Bugando kwa ajili ya kutambua majeruhi na ndugu waliofariki dunia kwenye ajali hiyo.

0 comments: