Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema itatumia zaidi ya Sh1.2 bilioni kwa maadhimisho ya miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo kilele chake kitakuwa Januari 12 mwakani.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed amesema hayo leo Jumapili Desemba 24,2017 ofisini kwake Vuga mjini Unguja alipotoa taarifa ya maandalizi ya sherehe hizo.
Amesema fedha hizo zinatarajiwa kutumika katika maandalizi ya siku ya kilele, ufunguzi wa miradi 49 ya maendeleo ya kiuchumi, miradi ya maji, majengo ya shule, umeme na barabara.
Waziri amesema miradi 33 itazinduliwa baada ya kukamilika na 16 itawekwa mawe ya msingi. Miradi hiyo ni ya taasisi za umma, jamii na ya wawekezaji.
Waziri Mohamed amesema Serikali imepiga hatua katika kufanikisha huduma za kijamii na maendeleo sambamba na lengo la Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.
Amesema wananchi wanapaswa kujitokeza kuunga mkono jitihada za Serikali katika kufanikisha maadhimisho hayo ambayo yatazinduliwa Desemba 30,2017 kwa kufanya usafi wa mazingira.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Dk Idriss Muslim Hijja amesema miradi iliyopendekezwa kuingizwa katika maadhimisho imefuatiliwa na kutolewa taarifa kwa sekretarieti ya halmashauri ya sherehe na maadhimisho ya kitaifa.
Amesema katika uzinduzi na uwekaji wa mawe ya msingi ya miradi, viongozi wa kitaifa wa Serikali zote mbili wamejumuishwa wakiwemo marais, mawaziri na wastaafu wa pande zote mbili.
Kilele cha maadhimisho hayo kitakuwa Januari 12,2018 katika Uwanja wa Amani mjini Unguja ambako Rais Ali Mohammed Shein atakuwa mgeni rasmi.
0 comments: