Wednesday, 27 December 2017

Kura za uchaguzi wa Marudio wa Rais zaanza kuhesabiwa Liberia

Shughuli ya kuhesabu kura imeanza Liberia kufuatia duru ya pili ya uchaguzi wa rais. Uchaguzi huo utaamua ni nani atakuwa Rais mpya wa Liberia kati ya mwanasoka wa zamani George Weah na Makamu wa Rais Joseph Boakai.

Kulingana na mwenyekiti wa tume ya uchaguzi ya Liberia Jerome Korkoya, matokeo rasmi yanatarajiwa katika kipindi cha siku chache zijazo. Kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 70, taifa hilo la magharibi mwa Afrika litashuhudia serikali iliyochaguliwa kwa njia ya kidemokrasia ikikabidhi madaraka kwa nyingine.
 Duru hiyo ya pili ya uchaguzi wa rais ilicheleweshwa baada ya kesi kuwasilishwa katika mahakama ya juu kupinga kufanyika kwa kura hiyo kwa madai ya kuwepo udanganyifu wa kura katika duru ya kwanza.
Sirleaf anaondoka madarakani
Rais Ellen Johnson Sirleaf anaondoka madarakani baada ya kuhudumu mihula miwili ya miaka 12 kwa jumla. Bi Sirleaf ambaye ni mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel, ndiye mwanamke wa kwanza barani Afrika kuwa Rais.

Mtandao wa waangalizi wa uchaguzi wa Liberia wenye zaidi ya waangalizi 1,000 waliotumwa kote nchini humo wamepongeza uchaguzi huo kuwa ulifanyika kwa utulivu na uliandaliwa vyema kuliko duru ya kwanza ya uchaguzi iliyofanyika tarehe 10 mwezi Oktoba. Waangalizi wa Umoja wa Ulaya pia walikuwa na mtizamo huo.
Rais wa zamani wa Nigeria Goodluck Jonathan ambaye ni mwaangalizi chini ya taasisi ya masuala ya demokrasia ya NDI yenye makao yake Marekani amesema ufanisi wa uchaguzi huo ni suala la umuhimu mkubwa linalofuatiliwa na jumuiya ya kimataifa.

Nani atakuwa Rais kati ya Weah na Boakai?
George Weah mwenye umri wa miaka 51, mwanasoka wa zamani maarufu aliyevichezea vilabu vya Paris Saint Germain, AC Milan, Chelsea na Manchester City anaungwa mkono na idadi kubwa ya vijana nchini Liberia, lakini anakosolewa kuhusu utendaji wake alipohudumu katika baraza la seneti kuanzia mwaka 2014.

Boakai mwenye umri wa miaka 73 kwa upande wake anaonekana kuwa mgombea urais atakayeendeleza sera za serikali na amesifiwa kwa kuhudumu kwa miaka mingi kama mtumishi wa umma na kuwa kiongozi asiyehusishwa na ufisadi licha ya kuwa anakosolewa kwa kushindwa kupambana na umasikini akiwa serikalini.
Weah alishinda duru ya kwanza kwa asilimia 38.4 huku Boakai akiibuka wa pili kwa asilimia 28.8.  Atakayeshinda uraia ana kibarua kikubwa cha kuimarisha uchumi wa Liberia.
Bi Sirleaf alifanikiwa kulikwamua taifa hilo kutoka athari za vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kuanzia mwaka 1989 hadi 2003, na pia kulikwamua kutoka athari za janga la Ebola kati ya mwaka 2014 hadi 2016 lakini anashutumiwa kushindwa kupambana na umasikini na ufisadi. Viwango vya maisha Liberia vinasalia kuwa miongoni mwa vibaya zaidi duniani.

DW Swahili.

0 comments: