Idadi ya waliofariki kufuatia kimbunga kilichopiga kusini mwa Ufilipino
imefikia watu 182 mapema leo asubuhi, huku watu 153 wakiwa bado
hawajulikani walipo. Kimbunga Tembin kimekuwa kikivuma katika kisiwa cha
pili kwa ukubwa nchini humo cha Mindanao tokea Ijumaa iliyopita, na
kusababisha mafuriko pamoja na maporomoko ya matope. Hapo jana maafisa
wa polisi, wanajeshi na wafanyakazi wa kujitolea walilazimika kuchimba
matope na vifusi kutafuta miili ya watu walioathirika katika kijiji cha
Dalama. Wakati huo huo waokoaji waliopoa maiti kadhaa kutoka katika mto
wa Salog karibu na mji wa Sapad. Idadi ya vifo katika rasi ya Zamboanga
ya kisiwa cha Mindano pia imeongezeka hadi watu 28, na polisi imeripoti
kwamba watu wengine 81 bado hawajulikani walipo baada ya matope na mawe
kuporomoka katika jamii za pwani huko Sibuco na miji mingine ya uvuvi.
Viongozi wa Ufilipino wamesema hapo jana kwamba maporomoko ya ardhi
yamezuia misafara yauokoaji na misaada za kiutu kuyafikia maeneo
masikini.
(DW SWAHILI)
0 comments: