BAADA ya kufunga bao lake la pili tangu atue Yanga, kiungo mshambuliaji
wa timu hiyo amewaambia mashabiki wa timu hiyo: “Tulieni, mbona
mtafurahi sana.” Kauli hiyo, aliitoa wikiendi iliyopita mara baada ya
kuifungia timu yake bao la kuongoza akipokea pasi ya Mrundi, Amissi
Tambwe wakati Yanga ilipovaana na Reha FC katika mechi ya Kombe la FA
iliyochezwa Uwanja wa Uhuru jijini Dar.
Kiungo huyo, hilo ni bao lake la pili kulifunga tangu ametua kuichezea
Yanga kwenye msimu huu wa Ligi Kuu Bara akitokea Mbao FC ya Mwanza.
Akizungumza na Championi Jumatano, Buswita alisema anafahamu mashabiki
wa Yanga wanapenda kumuona akionyesha kiwango cha juu zaidi ya hicho
amekionyesha kwa kifupi, hivyo ameomba muda kidogo.
Buswita alisema, ana mfupi tangu ametua kuichezea Yanga, hivyo kikubwa
mashabiki wamvumilie huku akiendelea kuwathibitishia ubora wake taratibu
kwenye mechi zijazo za ligi kuu na mashindano mengine. “Kikubwa watu
wanatakiwa wafahamu kuwa, mimi nimetoka kwenye timu ndogo ya Mbao na
nimekuja kwenye timu kubwa ya Yanga yenye presha kubwa ya mashabiki.
“Hivyo, ni lazima nibadilike taratibu kutoka mfumo niliokuwa nautumia
nikiwa na Mbao na kuuchukua huu wa Yanga, hivyo siyo kazi ndogo
inayohitaji muda kidogo wa mimi kuushika, pia kuzoeana na wenzangu.
“Niwaahidi Wanayanga kuwa, mtafurahi na kunielewa wenyewe, kwani
ninaamini uwezo wangu wa ndani ya uwanja ikiwemo kufunga na kutengeneza
nafasi za kufunga mabao,” alisema.
0 comments: