Adam Kimbisa.
Wateule wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) wanaowakilisha
nchi zao ndani ya Jumuiya hiyo, wanatarajia kuapishwa na pia kuchagua
Spika mpya wa bunge hilo, katika kikao cha Bunge hilo, kinachoanza
jijini Arusha leo.Kwa upande wa Tanzania, Adam Kimbisa amejitokeza kuwania nafasi hiyo akichuana na Leontine Nzeyimana (Burundi) na Martin Ngoga (Rwanda). Hatua hiyo, itatanguliwa na wabunge hao kwanza kuapishwa rasmi mbele ya Katibu wa Bunge hilo kuwa wabunge wa Bunge hilo.
Kwa mujibu wa Msemaji wa Bunge hilo, Bobi Odiko, Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai, anatarajiwa kuhudhuria uchaguzi huo pamoja na maspika wenzake kutoka nchi za jumuiya hiyo wa Kenya, Rwanda, Uganda, Burundi na Sudan Kusini.
Spika mpya wa EALA atakayechukua nafasi ya aliyekuwa spika wa Bunge hilo, Daniel Kidega, anatarajiwa kuongoza chombo hicho kwa miaka mitano ijayo. Nchi zote sita wanachama wa EAC zimewasilisha majina nane ya wabunge wanaoziwakilisha ndani ya Bunge hilo kwa Bunge hilo lenye makao yake makuu, jijini Arusha.
Ajenda kuu katika Bunge hilo, ni uapisho wa wabunge wapya, uchaguzi wa spika na uapisho wa wajumbe wa Kamisheni ya EALA na uteuzi wa kamati mbalimbali. Bunge hilo, lilitarajiwa kuanza vikao vyake tangu Juni 4, mwaka huu na kumalizika Juni 5, mwaka huu lakini ilishindana baada ya nchi tatu tu ambazo ni Uganda, Tanzania na Burundi kukamilisha taratibu zote.
Nchi ya Sudan Kusini ambayo kwa sasa Bunge lake ni la mpito ilibidi lirejee tena uchaguzi wake wa wabunge wa Afrika Mashariki baada mmoja wa wananchi wa nchi hiyo, Wani Salantino kukata rufaa katika Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) kupinga utaratibu mzima wa uchaguzi huo.
Kutokana na hatua hiyo, Bunge hilo la Sudan Kusini ilibidi lirejee tena uchaguzi huo, Agosti 3, mwaka huu na kuwasilisha majina ya wabunge waliochaguliwa kuiwakilisha nchi hiyo EALA.
Uganda ilikuwa ndiyo nchi ya kwanza kufanya uchaguzi wa wabunge wa EALA Machi Mosi, mwaka huu na wabunge waliochaguliwa ni pamoja na Susan Nakawuki, Fred Mukasa Mbidde na Chris Opoka.
Wengine ni Rose Akol, Mathias Kasamba, Mary Mugyenyi na Hon Paul Musamali. Dennis Namara, na George Stephen Odongo. Bunge la Tanzania lilimrejesha aliyekuwa mbunge wa EALA, Adam Kimbisa na Maryam.
Wabunge wengine wapya wa EALA wanaoiwakilisha Tanzania ni Josephine Lemoyan, Happiness Lugiko, Pamela Maassay, Dk Ngwaru Maghembe, Dk Abdullah Makame, Habib Mnyaa na Fancy Nkuhi.
Kwa upande wa Rwanda wabunge wanaoiwakilisha nchi hiyo EALA ni Pierre Celestin Rwigema, Martin Ngoga, Gasinzigwa Oda, Kalinda Francois Xavier, Alex Bahati, Fatuma Ndangiza, Rutazana Francine, Barimuyabo Jean Claude na Uwumukiza Francoise.
Aidha, kwa upande wa Burundi, wabunge wa Afrika Mashariki wanaowakilisha nchi hiyo ni Jean Marie Muhirwa, Leontine Nzeyimana, Ahingejeje Alfred, Burikukiye Marie Claire, Burikukiye Victor, Karerwa Mo-Mamo, Nduwayo Christophe, Rurakamvye Pierre Claver na Nsavyimana Sophie.
Wabunge wa Sudan Kusini ni Dk Ann Itto Leonardo, Gai Deng Nhial Deng, Dr Woda Jaremiah Odok, Gabriel Garang Ahol, Dk Gabriel Garang Arol, Thomas Deng, Mukulia Kennedy Ayason, Kim Duop na Gideon Gatpan Thoar. Bunge la Afrika Mashariki ni chombo cha jumuiya hiyo kilichoanzishwa mwaka 2001 kikiwa na hadhi ya Bunge lenye wawakilishi wa nchi zote wanachama
0 comments: