Wednesday, 21 March 2018

Tanzania na Kenya zinajitenga na Afrika? Ufa waibuka Bonde la Ufa na kuongeza uwezekano Afrika kugawanyika

Kuibuka kwa ufa mkubwa katika eneo la Suswa katika Bonde la Ufa kusini magharibi mwa Kenya kumezua wasiwasi kuhusu uthabiti wa eneo la Afrika Mashariki kijiolojia.

Wataalamu wanasema kutokea kwa ufa huo katika jimbo la Nakuru ni shughuli ya kijiolojia inayochukua muda mrefu ambayo imekuwa ikiendelea kwa muda.

Hilo limezua hatari ya kuanza kutokea tena kwa mitetemeko ya ardhi na milipuko ya vilkano.

Wanajiolojia wanasema baada ya mamilioni ya miaka, bara la Afrika litapasuka na kuwa vipande viwili.
Sehemu ya mpasuko itakuwa kwenye Bonde la Ufa jambo ambalo linazua uwezekano wa Kenya na Tanzania, pamoja na mataifa mengine ya Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika, kujitenga na bara la Afrika.

Mwanajiolojia David Adede ameambia BBC kwamba ufa huo ni sehemu ya kutengana kwa vipande viwili vikubwa vya bara Afrika ambako kutasababisha bara Afrika kutengana na kuwa mabara mawili.

Amesema shughuli hiyo imekuwa ikiendelea kwa muda lakini dalili zake zilikuwa zinafichwa na majivu ya volkano ambayo polepole yamekuwa yakiziba ufa kila unapotokea.

"Maji ya mvua yamesomba majivu hayo pamoja na mchanga na kuufanya ufa huo kuonekana zaidi," amesema.

Saturday, 17 March 2018

Hoja tatu kutoka kwa hotuba ya Mugabe

Chama cha National Patriotic Front, NPF, kilichoundwa na waliokuwa mawaziri wa Zanu PF kimemtangaza Rais wake.

Chama hicho kipya kimetangaza kuwa Brigedia mstaafu Ambrose Mutinhiri atakuwa Rais wake, hatua ambayo inaelezwa kuungwa mkono na Robert Mugabe.

Ijumaa juma lililopita, Mutinhiri alijiuzulu ubunge na ndani ya Zanu PF, akionyesha kutounga mkono kuondolewa kwa Mugabe madarakani.

Mkutano wa Mugabe wa kwanza na waandishi wa habari tangu aondoke madarakani inasemekana uliandaliwa na chama cha NPF ambacho kina matumaini ya kumuondoa

Mnangagwa kwenye kinyang'anyiro cha mwezi Agosti.

Kwa miezi kadhaa sasa imekuwa ikidhaniwa kuwa huenda Mugabe atarejea tena kwenye ulingo wa siasa dhidi ya chama chake cha zamani.

Lakini ni mambo yapi haswa aliyoyasema Mugabe kwenye hotuba yake?

Sikudhani kama angeweza kunigeuka'' Alisema Mugabe

Mugabe amesema kuwa Mnangagwa asingeweza kumuondoa madarakani kwani ni yeye ndiye aliyemuweka serikalini, alimsaidia alipokuwa gerezani, na hakuwaza kuwa siku moja Mnangagwa angemtoa madarakani.

Sunday, 25 February 2018

Wajue kiundani wababe wakiarabu watakaokutana na SIMBA SC. Si wa mchezo mchezo
Kaskazini mashariki mwa Misri unapatikana mji wa Port Said. Mji wa Port Said una ukubwa wa kilometa 30 tu sawa na mile 19. Una idadi ya wa watu wasiopungua laki sita. Mji huu ulianzishwa mwaka 1859 wakati wa ujenzi wa mfereji wa Suez. Miaka 61 baada ya kuanzishwa Port Said mwaka 1920 klabu ya Al Masry ilianzishwa.  Klabu ya Al Masry inatumia uwanja wa Al Masry club stadium unaobeba mashabiki 17,000. Uwanja huu inasadikia ulisababisha kusimamishwa kwa ligi kuu Misri mwaka 2012 baada ya vurugu kutokea.
Klabu ya Al Masry inakutana uso kwa uso na klabu ya Simba katika kombe shirikisho. Klabu ya Simba imeweka makazi yake mashariki mwa Tanzania katika jiji la Dar es salaam. Simba ilianzishwa miaka 16 baada ya Al Masry kuanzishwa mnamo mwaka 1936.  Jiji la Dar Es salaam pia lipo kwenye ukanda wa pwani kama ililivyo kwa jiji la Port  Said ambapo klabu ya Al Masry inapatikana. Jiji la Dar es salaam hapo awali lilijulikana kama Mzizima yaani mji wa afya njema kutokana na hali nzuri ya vyakula hasa hasa shughuli ya uvuvi wa samaki.

Sultan Majid bin said aliamua kutengeneza mji wake ndani ya Mzizima akauita nyumba ya aman yaani Dar (Nyumba) Es saalam (Amani). Kumbe Dar es salam maana yake nyumba ya amani ambapo kinyume chake ni Dar al hard yaan nyumba ya vita. Hapa majiji mawili yanakutana Jiji La Porto lenye vitimbi vya migogoro hasa katika mfereji wa Suez, pamoja na Vurugu za uwanja wa Port Said na jiji la Dar Es Salaam linalosifika kwa utulivu na aman.
Klabu ya Al Masry inaongozwa na kocha mkuu Hossan Hassan ambaye pia aliwahi kuwa mchezaji nguli wa zamani wa taifa la Misri. Hossan Hassan alizaliwa mwaka 1966 katika jiji la Cairo katika eneo la Helwan ambalo rais wa zamani wa Misri Gamal Abdel Nasser alitangaza eneo hilo kuwa mji wa viwanda. Hossan Hassan ndiye mfungaji bora wa muda wote wa timu taifa ya Misri akiwa na magoli 69 kwenye michezo 169. Anatajwa kama mchezaji bora katika historia ya soka barani Afrika. Anakumbukwa sana kule nchini Uswisi kwa kuitandika klabu ya Celtic magoli manne kwenye mchezo mmoja akiwa na klabu ya Neuchatel Xamax kwenye michuano ya kombe la UEFA.
Pia aliwahi kuichezea klabu hiyo Al Masry kunako mwaka 2004 mpaka 2006. Mnamo mwaka 2008 alipewa kandarasi ya kuionoa klabu hiyo. Alitundika daruga akiwa na miaka 42.
 Awali ya yote ni watoe hofu mashabiki wa Simba ambao wanadhani Al Masry ni klabu kubwa kama akina Al Ahly au Zamalek. Klabu hii haijawahi kutwaa ubingwa ligi kuu Misri tokea ligi hiyo ianzishwe mwaka 1948. ila imejitahidi kumaliza  nafasi tatu za juu kwenye msimamao wa ligi mara sita tu. Licha ya kuwa haina mafanikio makubwa sana ligi kuu lakini ni klabu yenye mashabiki wengi sana nyuma ya al Ahly, Zamalek na Ismalia. Ilikuwa na mafanikio makubwa sana miaka ya 1921 mpaka 1989. Imetwaa kombe la sultan mara 3, kombe la Misri mara moja mwaka 1998, na kombe la shirikisho la Misri mara moja nayo ni mwaka 1992.
Pia imetwaa kombe la kanda ya mfereji wa Suez mara 17 kombe ambalo kwa sasa halipo tena na lilikuwa likijumuisha timu za majiji matatu tu. Kikubwa Heshima kubwa walio nayo ni kuwa imekosa kushiriki ligi kuu miaka miwili tu, walishuka daraja mwaka 1957 mpka 1959 baada ya mgogoro mkubwa kwenye mfereji wa Suez ambapo mapato ya klabu yalishuka na baadhi ya wachezaji kuondoka. Kiwango chao msimu huu sio cha kutisha sana kama cha kama moto walio nao vijana wa Manara. Kwanza wapo nafasi ya 4 kwenye msimamo wao wa ligi wakiwa na alama 42 baada ya michezo 23. Katika michezo kumi ya mwisho ya ligi wameshinda michezo mitano wametoka suluhu michezo mitatu na wamepoteza miwili.
 Nitoe tahadhari, hawa jamaa nao wana balaa lao, wanagawa vipigo kwa timu kubwa na vya magoli mengi. Mnamo tarehe 5 mwezi wa pili walitoa dozi ya magoli manne ugenini kwa klabu ya El Maqasa, wakaliza El Tanta magol sita kwa mbili,  wakaizibua El Nasri ugenini kwa magoli matatu kwa mawili. Pia wakaitandika Zamalek ugenini goli moja.
Katika klabu hii wachezaji wa kuogopwa ni A Bance mwenye mabao matano akiwa na umri miaka 33, pamoja na mshambuliaji Ahmed Gomaa mwenye magoli 11 akiwa na umri wa miaka 29,  Ahmed Sokri kiungo machachari na mkongwe mwenye magoli matano akiwa na umri wa miaka 30, mwingine ni pamoja na Islam Abou Slemma mwenye magoli matano. Ni hayo tu.

Wednesday, 17 January 2018

Watanzania washinda tuzo ya fasihi ya Kiswahili Afrika

Watanzania wawili wametangazwa washindi wa Tuzo ya Kiswahili ya Mabati-Cornell ya Fasihi ya Afrika kwa mwaka 2017.

Wawili hao watazawadiwa $5,000 kila mmoja katika sherehe ambayo itafanyika jijini Nairobi mwezi ujao.

Dotto Rangimoto alishinda kwenye kitengo cha ushairi kwa mswada wake Mwanangu Rudi Nyumbani naye Ali Hilal Ali akashinda kitengo cha riwaya kwa mswada wake wa Mmeza Fupa.

Waziri wa habari, utamaduni na Sanaa Tanzania Dkt Harrison Mwakyembe amewapongeza wawili hao kwa ushindi huo na kusema ushindi wao "unachagiza juhudi za serikali kuibidhaisha lugha ya Kiswahili."

"Ushindi wa Watanzania hawa ni ushindi wa taifa kwa ujumla," amesema Dkt Mwakyembe kupitia taarifa.

Tuzo hiyo ilianzishwa mwaka 2014 na Dkt Lizzy Attree (Mkurugenzi wa Tuzo ya Caine) na Dkt Mukoma wa Ngugi (Chuo Kikuu cha Cornell, Marekani), kwa lengo la kuthamini uandishi kwa lugha za Kiafrika.

Aidha, tuzo hiyo inakusudiwa kuhimiza sanaa ya tafsiri baina ya lugha za Kiafrika zenyewe kwa zenyewe, na pia kutafsiri maandishi ya lugha nyengine kwa lugha za Kiafrika.

Wengine waliokuwa wanashindania tuzo hiyo ni: Mbaruk Ally - Hali Halisi (ushairi); Hassan Omar Mambosasa - Nsungi (riwaya); Mwenda Mbatiah - Kibweta cha Almasi (riwaya) na Richard Atuti Nyabuya - Umalenga wa Nyanda za Juu (ushairi).
Majaji walikuwa Ken Walibora Waliaula (Mwenyekiti wa Majaji), mwanataaluma na mwandishi; Daulat Abdalla Said, mwanataaluma na mwandishi, anayesomesha Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar; na Ali Attas, mwandishi na mwalimu wa Kiswahili na Kiingereza, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje, Japan.

"Mashairi yaliyomo katika diwani hii yametumiliwa lugha iliyojaa taswira na majazanda yanayowakilisha vyema hisia zinazoelezwa katika dhamira mbalimbali," walisema majaji kuhusu diwani ya Mwanangu Rudi Nyumbani.

"Mshairi amefaulu sana kuzitumia mbinu na miundo kadha wa kadha ili kuyajadili maswala yanayohusu hali na mazingira tafauti tafauti katika maisha ya binadamu. Anayazungumza maswala mazito mazito, lakini kwa namna ambayo hayamuelemei msomaji wake."

Walimsifu pia Bw Ali Hilal na kusema: "Si mno mtu kukutana na riwaya ya Kiswahili ambayo mwandishi wake amejidhihirisha kuwa ni mbuji wa lugha fasaha na ya kisanii, inayotiririka kitabia kwa hiari yake, na bila ya kuonesha dalili zozote kwamba imelazimishwa."

"Licha ya kwamba matukio ya riwaya hii yanatokea katika kisiwa cha kubuni, maswala yanayojadiliwa humu ni miongoni mwa yale maswala sugu yanayoendelea kulisumbua bara la Afrika kisiasa, kijamii na kiuchumi."

Tuzo ya Kiswahili ya Mabati-Cornell ya Fasihi ya Kiafrika, yenye thamani ya jumla ya Dola za Marekani 15,000, hutolewa kila mwaka kwa miswada bora, au kwa vitabu vilivyochapishwa miaka miwili kabla ya mwaka wa kutolewa zawadi, katika fani za riwaya, ushairi, wasifu na riwaya za picha.

Miswada inayoshinda huchapishwa na shirika la uchapishaji vitabu la East African Educational Publishers (EAEP) na shirika la uchapishaji vitabu la Mkuki na Nyota Publishers

Na mswada bora wa ushairi hufasiriwa kwa Kiingereza na kuchapishwa kitabu na shirika la Africa Poetry Book Fund.

Tuzo hii inadhaminiwa na kampuni ya Mabati Rolling Mills, Kenya, na kampuni ya ALAF Limited, Tanzania na pia Ofisi ya Makamu wa Mkuu wa Masuala ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Cornell, na Idara ya Taaluma za Afrika ya Chuo Kikuu cha Cornell, Marekani.
Utafiti: Mbwana Samatta, Salim Kikeke wana ushawishi mkubwa Tanzania
Mchezaji wa soka kutoka Tanzania Mbwana Samatta amechaguliwa kuwa kijana mwenye ushawishi mkubwa nchini Tanzania kulingana na kura ya maoni iliofanywa na chombo cha habari cha Avance media.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 25 anaichezea klabu ya Genk na timu ya taifa ya soka nchini humo taifa Stars.

Nahodha huyo wa Tanzania alishinda tuzo ya mchezaji bora wa shirikisho la soka barani Afrika Caf miongoni mwa wachezaji wanaosakata kandanda barani Afrika 2016 baada ya kuisaidia timu yake ya TP Mazembe kushinda kombe la ligi ya Afrika.
Naye mtangazaji wa habari wa BBC Swahili Salim Kikeke alikuwa wa saba katika kura hiyo akimshinda msanii wa bongo fleva Diamond Platinumz.
Matokeo ya kura hiyo nchini Ghana na Nigeria yalitolewa mapema mwaka huu.
Mchezaji Victor Moses alichaguliwa kuwa mtu mwenye ushawishi mkubwa huku wakili wa rais wa Ghana Kow Essuman akichaguliwa mtu mwenye ushawishi mkubwa nchini humo.

Tazama orodha kamili ya vijana walio na ushawishi mkubwa Tanzania:


Monday, 15 January 2018

Rais Magufuli ataja sababu za kumuunga mkono Kagame kuongoza Umoja wa Afrika (AU)
Rais John Magufuli amesema Rais Paul Kagame wa Rwanda anafaa kuongoza Umoja wa Afrika (AU) kwa sababu ya historia yake na hivyo anazifahamu changamoto zinazolikabili bara hili.

Rais Magufuli alisema hayo jana Ikulu wakati Kagame alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja, ikiwa ni mara yake ya pili kufanya ziara tangu Rais Magufuli alipoapishwa. Alifanya ziara kwa mara ya kwanza Julai Mosi, 2016.

Magufuli alimwaga sifa hizo akianzia matatizo yaliyoibuka nchini Libya baada ya kiongozi wake wa kijeshi, Muamar Gadaffi kuondolewa madarakani kwa vurugu licha ya kuliongoza taifa hilo vizuri kiuchumi.

“Baada ya kiongozi wa Libya kuondoka, na nyinyi nyote mnajua, matokeo yake ni haya. Na haya ndiyo ya ukweli na utabaki kuwa ukweli,” alisema Rais Magufuli katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu jana.

“Nina uhakika Mheshimiwa Kagame atakapokuwa mwenyekiti wetu Afrika, atayaadress (atayashughulikia haya), atayaadress vizuri masuala ya migogoro miongoni mwa nchi za Afrika, atayaaddress vizuri masuala ya ukoloni mamboleo unaoweza kuletwa na mtu yeyote kutoka nje akasababisha matatizo kwa Waafrika.

“Mheshimiwa Kagame hadi kufikia urais anafahamu shida za wananchi wa Rwanda; anajua historia ya Rwanda ilitokotoka hadi ikatokea genocide (mauaji ya watu wengi). Anafahamu mateso ya Wanyarwanda; anafahamu mateso yanayoweza kuletwa na mtu hata mmoja tu, inawezekana ikawa ni media kwa kutangaza au kuandika kitu cha ovyo kikaleta multiplying effect.”

Alisema ndio maana anaamini kutokana na mchango wake kwa Afrika na kwa sababu ni mwanamapinduzi mzuri, uzoefu wake utasaidia maendeleo ya Afrika.

“Rais Kagame ni mwanamapinduzi wa kweli wa Afrika, ameishi maisha ya Kiafrika, maisha ya mateso tangu akiwa kijana; ameishi kwenye nchi za ugenini kama mkimbizi, anayafahamu mateso ya kijana,” alisema.

“Kwa hiyo kwa yale maisha aliyoyaishi kama mkimbizi, kama kijana, nina uhakika ataleta mageuzi makubwa Rwanda ambayo ameshaanza kuyaleta, lakini ataleta mageuzi makubwa Afrika.”

Alisema Tanzania inamuunga mkono Rais Kagame kwa nguvu zote ili kuwepo kwa mabadiliko ya kiuchumi kwa Waafrika wote hasa kwa vijana ambao ndiyo nguvu kazi kubwa katika bara hili.

Thursday, 11 January 2018

Ethiopia imekataza raia wa kigeni kuasili watoto wa Ethiopia
Serikali ya Ethiopia imekataza raia wa kigeni kuasili watoto wa Ethiopia kwa madai kuwa watoto hao hunyanyaswa na kutelekezwa wakiwa ughaibuni.

Ethiopia ni miongoni mwa nchi ambazo ni vyazo vikuu vya watoto wanaoasiliwa na raia wa Marekani kwa kiwango cha kufiki asilimia 20 kwa kwa ujumla.

Watu maarufu kama Brad Pitt na Angelina Jolie ni miongoni mwa walioasili watoto kutoka Ethiopia.

Hata hivyo, mwaka 2013, wanandoa wawili kutoka marekani walishtakiwa kwa kumuua binti mmoja wa Ethiopia waliyekuwa wamemuasili. Kesi ambayo ilileta mjadala mkali nchini Ethiopia.

Mchakato mzima wa kuasili watoto nchini Ethiopia umekumbwa na maswali mengi asasi za kutetea haki za binadamu wakisema kuwa unawanufaisha wafanyabiashara wanaosafirisha binadamu.

Miaka miwili iliyopita , Denmark ilisitisha kuasili watoto kutoka Ethiopia.
Watunga sheria wa nchi hiyo wanasema kuwa yatima na watoto wote wasiojiweza wanatakiwa kutunzwa chini ya msaada utakao patikana nchini Ethiopia kwa ajili ya kuwalinda.

Ingawa baadhi ya wabunge wanasema nchi hiyo bado haina huduma bora inayoweza kuwapa uangalizi mzuri watoto hao wenye uhitaji.

Tangu mwaka 1999, watoto zaidi ya 15,000 wameasiliwa Marekani kutoka Ethiopia.

Wengine wengi wakiwa wanapelekwa katika nchi za ulaya kama Hispania, Ufaransa na Italia.
Kanisa la muhubiri anayetengeza ''fedha za miujiza'' lafungwa Botswana
Taifa la Botswana limelifunga kanisa la muhibiri mmoja wa Malawi mwenye utata anayedaiwa ''kutembea angani''.

Serikali ilithibitisha kufungwa kwa kanisa la Bushiri la Christian Gathering Church ECG mjini Gaborone mara kadhaa kutokana na wasiwasi kuhusu ''fedha za miujiza''.

Chombo cha habari cha Malawi24 kimeripoti kwamba kanisa hilo lilipinga uamuzi huo mahakamani uliochukuliwa chini ya mwaka mmoja baada ya muhibiri huyo kupigwa marufuku kuingia nchini humo.

Alikuwa ametarajiwa kuhudhuria kongamano fulani.

Hatahivyo waziri wa Botswana Edwin Batshu alitangaza mnamo mwezi Aprili 2017 kwamba bwana Bashir ambaye sasa anaishi Afrika Kusini atahitaji Visa ili kuingia, licha ya raia wa Malawi kutohitaji kibali hicho kulingana na chombo cha habari cha AllAfrica.com

Serikali imetangaza kwamba kanisa hilo litafungwa kabisa, huku gazeti hilo la Botwana likipata barua ilioambia usimamizi wake kwamba kibali cha kuendesha kanisa hilo kimefutiliwa mbali.
Maandamano ya ghasia kupinga mfumuko wa bei yaendelea Tunisia
Kumekuwa na muendelezo wa siku tatu wa ghasia za maandamano nchini Tunisia katika mji mkuu wa Tunis na miji mingine ya nchi hiyo.

Polisi wamekuwa wakirusha mabomu ya machozi kwa kundi kubwa la watu ambao wamekuwa wakilalamikia juu ya mfumuko wa bei ambao unaathiri upatikanaji wa mahitaji muhimu.
Waziri mkuu , Youssef Chahed amelaani kwa kile alichokiita kuwa ni hakikubaliki kwa kuwepo kwa fujo za waandamanaji.

Kwa upande wao waandamanaji ,nao pia wametoa malalamiko yanayofanana juu ya polisi.
Maandamano ni juu ya bei kuwa ghali , wamepandisha, nadhani hii ni hali ngumu sana kubadilika , labda kama rais huyu tutamuondoa"
Wafanyabiashara wengi wamekamatwa na polisi na kuibiwa huku vyombo vya usalama wakiwa wamewekea mkazo kulinda majengo ya serikali.

Watu wapatao mia mbili wamefungwa mpaka sasa na huku kuna kuna mpango mwingine wa kuwepo kwa maandamano mengine makubwa hapo kesho.

Tuesday, 9 January 2018

Mfumuko wa Bei wasababisha Maandamano Tunisia
Mtu mmoja amekufa na wengine watano kujeruhiwa katika maandamano ya kiuchumi katika mji mkuu wa Tunisia, tunis. Maandamano hayo yameenea katika maeneo mengine kumi nchini humo.

Uchumi wa nchi hiyo umekua ukitetereka tangu mwaka 2011 wakati kiongozi wa kipindi hicho Zine El Abdine Ben Ali akiondolewa madarakani.

Kwa sasa fedha ya Tunisia imeshuka zaidi ikilinganishwa na Uero,

Miongoni mwa sababu ya maandamano hayo ni mfumko wa bei ambao umesababisha kuongezeka kwa kodi katika bidhaa zinaingizwa nchini kama magari na bidhaa nyingine.

Shirika la habari la Tunisia limesema kuwa Polisi wametumia mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji wanaopinga kupanda kwa bei katika bidhaa mbalimbali katika maeneo mbalimbali.

Watu wengine Zaidi ya mia tatu wameingia barabarani katika mji wa kati wa Sidi Bouzid, huku wakipinga juu ya ukosekani wa ajira na maendeleo hafifu katika maeneo yao .

Tunisia inategemea misaada kutoka nje kupanda na kuporomoka kwake kwa uchumi,Na hii yote ni matokeo ya mapinduzi ya 2011 na mashumbulio mawili makubwa mwaka 2015 ambapo bado athari yake ni kubwa katika sekta ya utalii nchini humo.

Monday, 8 January 2018

Ongezeko la bei ya mkate lazua maandamano Sudan Kusini
Kumekuwa na maandamano katika miji mbalimbali nchini Sudan Kusini mara baada ya gharama ya mkate kuongezeka mara mbili zaidi.

Hatua hiyo ya maandamano imekuja baada ya serikali ya nchi hiyo kufanya maamuzi ya kuondoa ruzuku ya vyakula na kusababisha gharama ya mkate kuwa kubwa mara dufu.

Huko magharibi mwa Darfur, mwanafunzi mmoja aliyekuwa katika maandamano aliuwawa na wengine sita kujeruhiwa mara baada ya maandamano hayo kugeuka kuwa ya fujo
Katika mji mkuu wa Khartoum, polisi walitumia mabomu ya machozi kusambaratisha watu ambao walikuwa wamefunga barabara na kuchoma matairi.

Naibu waziri wa mambo ya ndani alikanusha kuwa maandamano hayo hayakutoea kutokana na ongezeko la bei na kuahidi kuwa atawashughulikia wale wote waliokuwa wanafanya maandamano yenye fujo.

Serikali ya Sudan pia imezuia magazeti yote yaliyokosoa ongezeko la bei kutouzwa.

Maamuzi ya kuongeza bei ya mkate kwa serikali ya Sudan ni sehemu ya kufuata matakwa ya IMF ili kukuza uchumi wa nchi hiyo.

Sunday, 7 January 2018

Mawaziri wawili wa zamani wakamatwa kwa tuhuma za rushwa Zimbabwe
Walter Mzembi aliyekuwa waziri wa mambo ya nje amesema tuhuma hizi ni za kisiasa

Mawaziri wawili wa zamani wa Zimbabwe wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za rushwa.

Samuel Undenge ambaye alikua waziri wa nishati anatuhumiwa kutumia dola elfu kumi na mbili kwa kampuni ambayo haukufanya lolote.

Kwa upande wa wake Walter Mzembi aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wakati wa utawala wa Robert Mugabe aliyeondolewa madarakani mwezi Novemba, anatuhumiwa kuchangia baadhi ya mali za televisheni ya Taifa kwa kanisa moja nchini humo bila ya idhini ya serikali.

 

Wote wawili wamekana mashitaka hayo.Inatarajiwa kesi hizo zitasikilizwa tena baadae mwezi huu.

Rais mpya Emmerson Mnangagwa ameapa kupambana na rushwa iliyodumu karibia wakati wote wa utawala wa Robert Mugabe.

Lakini wakosoaji wanasema watu wanaokamatwa na kufikishwa mahakamani ni wale tu wanaohoji namna Mnangagwa aliyoingia madarakani.

Wednesday, 3 January 2018

Waziri mwingine ang'atuka madarakani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Zambia, Harry Kalaba, ametangaza kujiuzulu wadhifa wake, kwa kile alichodai kushindwa kwa Rais Edgar Lungu, kupambana na rushwa.

Kalaba amesema uamuzi wake umetokana na kiwango cha juu cha rushwa ambayo inafanywa na watu ambao wanatarajiwa kuwa suluhisho

Amesema tayari amewasilisha barua yake ya kujiuzulu kwa Rais Lungu, na kwamba amechukua uamuzi huo kwa moyo mzito, hata hivyo Msemaji wa Rais, Amos Chanda, amesema Ikulu bado haijapokea barua ya kujiuzulu kwa Kalaba.

Kalaba anakuwa Waziri wa tatu kuondoka ndani ya serikali ya Rais Lungu baada ya kutimuliwa kwa Mawaziri wawili akiwemo Waziri wa Mipango na Waziri wa Habari na Utangazaji.

Kalaba, ambaye ni Mbunge wa chama tawala cha Patriotic Front (PF), anatajwa kuwa mgombea wa urais katika uchaguzi wa urais utakaofanyika mwaka 2021 ikiwa Lungu atajiweka pembeni.

Tuesday, 2 January 2018

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa kwa Rais Kabila wa DRC kumtaka ajiuzulu
Umoja wa Mataifa umemwambia Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Joseph Kabila kutimiza ahadi aliyoiweka ya kuachia madaraka na kupisha uongozi mwingine kuiongoza nchi hiyo hususani wakati huu ambapo nchi hiyo imejaa migomo na maandamano ya kushinikiza ajiuzulu.

Rais Kabila mwenye miaka 46, ameiongoza DRC kwa miaka 17 na msimu wake wa mwisho wa uongozi uliisha tangu December 31, 2016 na akatakiwa aachie ngazi lakini uchaguzi wa kupata Rais na viongoi wapya umekuwa ukiahirishwa mara kwa mara.

Suala hili limesababisha vurugu na maandamano ya raia wa DRC ambao hata hivyo inaelezwa kuwa wamekuwa wakipigwa na askari polisi jamabo ambalo kwenye taarifa ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa December 31, 2017 imelaani vikali vitendo hivyo hususani Jijini Kinshasa ambapo watu watano waliuawa na polisi siku hiyo vya Jumapili kwenye maandamano.

Wednesday, 27 December 2017

INASIKITISHA, INAUMA: HII HAPA HOTUBA YA MWISHO YA MAREHEMU MUAMMAR GADDAFI WA LIBYA
QADAFFI ANAANZA HIVI: "Kwa jina la Mwenyezi Mungu (Allah), Mungu mpaji, na mwenye rehema....

Kwa miaka takribani 40 ama ilikuwa zaidi sikumbuki. Nachokumbuka ni kuwa nilifanya kila nilichoweza kuwapa watu wangu nyumba, hospitali na shule. Na kila walipohisi njaa niliwapa chakula. Niliifanya Benghazi kutoka jangwa kuwa ardhi nzuri ya kilimo.

Nilisimama imara dhidi ya Ronald Regan (Rais wa zamani wa Marekani), alipomuua binti yangu niliyemuasili. Alikua anajaribu kuniua mimi lakini akamuua yule binti yatima masikini. Niliwasaidia kaka na dada zangu waafrika fedha kupitia AU.

Nilifanya kila nililoweza kuwafanya watu wangu waelewe maana halisi ya demokrasia; ambapo watu wa tabaka la chini niliwapa madaraka.

Lakini hawakuridhika. Hata aliyekuwa na nyumba ya vyumba kumi, nguo mpya, na fanicha nzuri, hakuridhika. Alihitaji zaidi.

Kwa jinsi walivyokuwa wabinafsi walihitaji zaidi. Hivyo wakawaambia Marekani kuwa wanataka "demokrasia" na "uhuru". Hawakujua kuwa "demokrasia" waliyoitaka ilikua ni mfumo wa unyonyaji ambapo mbwa mwenye nguvu zaidi huwala mbwa wadogo.

Walikua hawasikii wala hawaoni. Walitaka "demokrasia". Wakasahau kuwa hata Marekani hakukuwa na huduma za afya za bure, dawa bure, elimu bure na chakula cha bure. (Huduma hizi za bure zilipatikana Libya tu).

Nchini Marekani mtu masikini/fukara hana cha bure. Labda awe ombaomba au avuje jasho kuhemea.
Haikujalisha nilifanya kwa kiasi gani bado hawakuridhika. Lakini wapo waliojua mimi ni mtoto wa Gamal Abdel Nasser, mwarabu pekee halisi na kiongozi wa kiislamu tuliyewahi kuwa nae tangu enzi za Salah-al-Deen.

Wakati Nasser anapigania mfereji wa Suez kwa watu wake nami nilikua naipigania Libya kwa watu wangu. Nilikua najaribu kufuata nyayo zake ili kuwaweka watu wangu huru kutoka kwenye makucha ya wakoloni wanaotuibia.
Lakini kwa sasa niko mateka katikati ya majeshi makubwa ya dunia katika historia. Mwanangu mpendwa mwenye asili ya Afrika, Obama anataka kuniua.

Ili achukue uhuru wetu, achukue haki yetu ya huduma za bure za afya, huduma za bure za elimu, na chakula chetu; na kutuletea mfumo mpya wa kimarekani wa kuiba uitwao "Ubepari"
Lakini wote katika dunia ya tatu tunajua maana yake. Maana yake ni kuwa "washirika" wanatawala mataifa, wanatawala dunia, na watu wanaishia kuteseka.

Kwa hiyo hakuna mbadala kwangu. Lazima niwe na msimamo. Na kama Mungu atapenda nitakufa kwa mapenzi yake.

Mapenzi yake yaliyofanya nchi yetu kuwa na ardhi yenye rutuba, chakula bora, na huduma bora za afya. Mapenzi ya Allah yaliyowezesha tukawasaidia kaka na dada zetu waafrika na waarabu waliokuwa na shida.

Sipendi kufa; lakini kama nitakufa ili kuiokoa ardhi hii, kuokoa watu wangu, na wengine ambao ni kama wanangu; acha nife.!

Acha sauti hii iwe agano langu kwa dunia kuwa nilisimama kupinga uvamizi wa NATO. Nilisimama kishujaa kupinga usaliti wa nchi za magharibi na nia mbaya za kikoloni. Na hapa nimesimama na ndugu zangu waafrika, kaka na dada zangu waislamu kama ngao yangu ya matumaini.

Wakati wengine walipokuwa wanajenga majumba ya kifahari, mimi niliishi kwenye nyumba ya kawaida na kwenye mahema. Siwezi kusahau maisha yangu ya utoto kule Sirte.

Sikutapanya rasilimali za nchi yangu kipumbavu. Na kama alivyokua Salah-al-Deen, kiongozi wetu katika uislamu, nilichukua kidogo sana kwa ajili yangu, na sehemu kubwa niliwapa wananchi.

Watu wa magharibi wameniita "kichaa", "mwendawazimu" lakini wanajua ukweli kuwa mimi si kichaa wala mwendawazimu; ila waache waendelee kudanganya. Wanajua hii ardhi ni huru na haipo kwenye himaya ya kikoloni. Huu ndio msimamo wangu na dira yangu na imekuwa wazi kwa watu wangu.

Nitapambana hadi pumzi yangu ya mwisho ili watu wangu wawe huru. Mwenyezi Mungu atusaidie tubaki waaminifu na tuwe huru.
-- Mu'uammar Qaddafi.
Kura za uchaguzi wa Marudio wa Rais zaanza kuhesabiwa Liberia
Shughuli ya kuhesabu kura imeanza Liberia kufuatia duru ya pili ya uchaguzi wa rais. Uchaguzi huo utaamua ni nani atakuwa Rais mpya wa Liberia kati ya mwanasoka wa zamani George Weah na Makamu wa Rais Joseph Boakai.

Kulingana na mwenyekiti wa tume ya uchaguzi ya Liberia Jerome Korkoya, matokeo rasmi yanatarajiwa katika kipindi cha siku chache zijazo. Kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 70, taifa hilo la magharibi mwa Afrika litashuhudia serikali iliyochaguliwa kwa njia ya kidemokrasia ikikabidhi madaraka kwa nyingine.
 Duru hiyo ya pili ya uchaguzi wa rais ilicheleweshwa baada ya kesi kuwasilishwa katika mahakama ya juu kupinga kufanyika kwa kura hiyo kwa madai ya kuwepo udanganyifu wa kura katika duru ya kwanza.
Sirleaf anaondoka madarakani
Rais Ellen Johnson Sirleaf anaondoka madarakani baada ya kuhudumu mihula miwili ya miaka 12 kwa jumla. Bi Sirleaf ambaye ni mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel, ndiye mwanamke wa kwanza barani Afrika kuwa Rais.

Mtandao wa waangalizi wa uchaguzi wa Liberia wenye zaidi ya waangalizi 1,000 waliotumwa kote nchini humo wamepongeza uchaguzi huo kuwa ulifanyika kwa utulivu na uliandaliwa vyema kuliko duru ya kwanza ya uchaguzi iliyofanyika tarehe 10 mwezi Oktoba. Waangalizi wa Umoja wa Ulaya pia walikuwa na mtizamo huo.
Rais wa zamani wa Nigeria Goodluck Jonathan ambaye ni mwaangalizi chini ya taasisi ya masuala ya demokrasia ya NDI yenye makao yake Marekani amesema ufanisi wa uchaguzi huo ni suala la umuhimu mkubwa linalofuatiliwa na jumuiya ya kimataifa.

Nani atakuwa Rais kati ya Weah na Boakai?
George Weah mwenye umri wa miaka 51, mwanasoka wa zamani maarufu aliyevichezea vilabu vya Paris Saint Germain, AC Milan, Chelsea na Manchester City anaungwa mkono na idadi kubwa ya vijana nchini Liberia, lakini anakosolewa kuhusu utendaji wake alipohudumu katika baraza la seneti kuanzia mwaka 2014.

Boakai mwenye umri wa miaka 73 kwa upande wake anaonekana kuwa mgombea urais atakayeendeleza sera za serikali na amesifiwa kwa kuhudumu kwa miaka mingi kama mtumishi wa umma na kuwa kiongozi asiyehusishwa na ufisadi licha ya kuwa anakosolewa kwa kushindwa kupambana na umasikini akiwa serikalini.
Weah alishinda duru ya kwanza kwa asilimia 38.4 huku Boakai akiibuka wa pili kwa asilimia 28.8.  Atakayeshinda uraia ana kibarua kikubwa cha kuimarisha uchumi wa Liberia.
Bi Sirleaf alifanikiwa kulikwamua taifa hilo kutoka athari za vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kuanzia mwaka 1989 hadi 2003, na pia kulikwamua kutoka athari za janga la Ebola kati ya mwaka 2014 hadi 2016 lakini anashutumiwa kushindwa kupambana na umasikini na ufisadi. Viwango vya maisha Liberia vinasalia kuwa miongoni mwa vibaya zaidi duniani.

DW Swahili.
Marais Afrika Nzima Kukutana January Kwa Ajili ya Mageuzi Makubwa



Wakuu wa nchi na Serikali za Afrika, wakiwemo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), mapema mwakani wanatarajiwa kusaini makubaliano ya kuanzishwa kwa eneo huru la biashara la bara hilo (CFTA).

Wanatarajiwa kuwa na mkutano wa 30 wa kawaida Januari 28 na 29 mwakani katika ukumbi wa Nelson Mandela uliopo kwenye Kituo kipya cha Mikutano (AUC) jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Mkutano huo utakaokuwa nakaulimbiu; “Kushinda Vita Dhidi ya Rushwa: Mwelekeo Endelevu wa Mabadiliko Afrika,” utatanguliwa na mkutano wa 35 wa Kamati ya Wawakilishi wa Kudumu (Januari 22-23) na mkutano wa 32 wa kawaida wa Baraza la Utendaji (Januari 25-26).

CFTA itakuwa soko la zaidi ya watu bilioni 1.3 na wanatarajiwa kufika takribani bilioni mbili ifikapo mwaka 2025. Yatakaposainiwa, makubaliano hayo ya kibiashara yatakuwa makubwa zaidi barani humo yakizihusu nchi zote 54 za Afrika, na yatakuwa ya pili kwa ukubwa duniani. Makubaliano makubwa zaidi duniani ni ya Shirika la Biashara la Dunia (WTO) yaliyosainiwa mwaka 1994.

Kwa sasa Afrika ina masoko mawili makubwa yanayozihusu baadhi ya nchi, ikiwemo Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA).

EAC yenye nchi sita wanachama za Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini, Tanzania na Kenya, ina zaidi ya watu milioni 170. Mkutano wa 18 wa kawaida wa wakuu wa nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia Januari 2012, uliamua kuwa hadi mwaka 2017 CFTA iwe imeanzishwa. Majadiliano kuhusu uanzishwaji huo yalianza rasmi Juni 2015.

Juni mwaka huohuo, wakati wa mkutano wa 25 wa wakuu wa nchi za AU uliofanyika Afrika Kusini, viongozi hao walikubaliana lianzishwe eneo huru la biashara ifikapo mwaka 2017 kupitia makubaliano na biashara huria za bidhaa na huduma.

Kwenye mkutano wa nne wa mawaziri wa biashara kutoka nchi za Afrika, uliofanyika hivi karibuni Niamey, Niger viongozi hao waliidhinisha muundo wa makubaliano na kuzingatia maendeleo, yaliyofikiwa kwenye majadiliano ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mkutano ujao wa wakuu wa nchi na serikali. CFTA itatoa uhakika wa mazingira ya uwekezaji, maendeleo ya viwanda na ongezeko la thamani ya bidhaa na huduma, hivyo kutengeneza fursa za ajira na vipato vya familia.

Hivi karibuni, wakati anafungua mkutano wa mawaziri mjini Niamey, Rais wa Jamhuri ya Niger Issoufou Mahamadou alipongeza maendeleo yaliyofikiwa katika majadiliano kuhusu makubaliano hayo.

CFTA na makubaliano mengine yakiwemo ya Kuharakisha Maendeleo ya Viwanda Afrika (AIDA), Programu ya Maendeleo ya Kilimo Afrika (CAADP), Mpango wa Programu ya Maendeleo ya Miundombinu Afrika (PIDA) vitaiwezesha Afrika kufanikiwa katika malengo ya mabadiliko.

Makubaliano ya kuanzisha eneo huru la biashara Afrika, yanaweka ajenda kwa ajili ya mijadala kuhusu biashara ya bidhaa, biashara ya huduma na utatuzi wa migogoro. CFTA itashughulikia itifaki mbili, ikiwemo ya biashara ya bidhaa na itifaki ya biashara ya huduma. Makubaliano hayo yanatarajiwa kuboresha biashara baina ya nchi za Afrika.

Malengo makuu ya CFTA ni kuiwezesha Afrika kuwa na soko moja la bidhaa na huduma, litakalotoa uhuru kwa wafanyabiashara na uwekezaji na hivyo kutoa fursa ya kuongeza kasi ya kuanzisha umoja wa forodha barani humu.

Tuesday, 26 December 2017

Leo ni duru ya pili ya uchaguzi wa rais Liberia kati ya George Weah na Joseph Boakai
Watu nchini Liberia wanapiga kura katika duru ya pili kati ya makamu wa rais Joseph Boakai na nyota wa zamani wa kandanda George Weah.
Bwana Weah, 51, alishinda duru ya kwanza lakini hakufanikiwa kupata asilimia 50 ya kura kumwezesha kuwa mshindi.
Duru ya pili ya uchaguzi wa urais kuchukua mahala pake Ellen Johnson Sirleaf, ilichelewa kufuatia kesi iliyokuwa mahakamani.
Vituo vya kupigia kura vinafunguliwa saa mbili asubuhi na kufungwa saa kumi na mbili.
Zaidi ya watu milioni mbili wamejiandikisha kama wapiga kura.

Wagombea ni nani?

Bw. Boakai 73, amekuwa makamu wa rais nchini Liberia kwa miaka 12 lakini haonekani kunufaika na uungwaji mkono kutoka kwa rais.

Naye Weah, ambaye ni nyota wa zamani wa kandanda ana matumaini ya kushinnda baada ya kuwania kwa mara ya tatu.
Alimshinda Bi Johnson Sirleaf wakati wa duru ya kwanza mwaka 2005, lakini akashindwa wakati wa duru ya pili.
Wakati wa uchaguzi ulioafuata akiwa mgombea mwenza, muungano wake ulisusia duru ya pili ukidai kuwepo udanganyifu.

BBC Swahili

 

Sunday, 24 December 2017

Waziri wa Ulinzi Dr. Hussein Mwinyi amewatembelea wanajeshi wa Tanzania nchini DRC
Ikiwa zimepita siku 16 tangu kuuawa kwa askari 14 wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) waliokuwa kwenye  oparesheni ya ulinzi wa amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Waziri wa Ulinzi wa Tanzania Husssein Mwinyi  amewatembelea wanajeshi wa Tanzania waliopo nchini humo.
Mwinyi alifika nchini humo December 22, 2017 ambapo  alipowatembelea Wanajeshi wa Tanzania wanaoshiriki katika kikosi cha kimataifa cha kulinda amani mashariki ya Congo, na kuwatembelea wanajeshi waliojeruhiwa wakati wa shambulizi la December  7, 2017.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Beni, Mwinyi ametoa wito wa kudumisha ushirikiano kati ya pande zote zinazoshiriki katika kuleta amani Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Wanajeshi 14 wa Tanzania wa kikosi maalum cha nchi za Kusini mwa Afrika SADC waliuawa na wengine 44 kujeruhiwa wakati wa majibizano ya risasi na waasi wasiojulikana katika kambi yao huko Semulik, karibu na mji wa Beni.
Liberia kupiga Kura 27.12.2017 katika Uchaguzi wa Rais Uliocheleweshwa
Waliberia watamchagua kiongozi mpya Jumanne (27.12.2017) katika uchaguzi wa duru ya pili kati ya makamu wa rais Joseph Boakai na mchezaji kandanda wa zamani maarufu George Weah.

Kura hiyo itaashiria mabadiliko  ya  kwanza  ya uongozi  nchini  humo  tangu  mwaka  1944.
Baada  ya  wiki  saba  za uchelewesho kutokana  na  malalamiko  ya kisheria  yaliyofikishwa  mahakamani  na  chama  tawala  cha Boakai  cha  Unity dhidi  ya  tume  ya  uchaguzi  nchini  humo, vituo vya  kupigia  kura  vinatarajiwa  kufunguliwa  kuanzia  saa  mbili asubuhi  saa  za  Liberia  na  kufungwa majira  ya  saa  12  jioni  kwa ajili  ya  wapigakura  milioni 2.1 waliandikishwa  kupiga  kura
Chama  cha  Weah cha  Muungano  kwa  ajili  ya  mabadiliko  ya kidemokrasi, Coalition for Democratic Change (CDC) kimewataka wapiga  kura  kutokunywa  pombe kupita  kiasi  katika  sikukuu  ya Krismasi na  kuamka  mapema  siku  ya  tarehe  26  kupiga  kura zao  katika  kile  mwenyekiti  wa  tume  ya  uchaguzi  ya  taifa  NEC, Francis Korkoya  alichosema  kuwa  ni "kujitolea  mhanga  kwa  ajili ya demokrasia  yetu  na  nchi  yetu."
Watachagua  mrithi  wa  rais Ellen Johnson Sirleaf, anayetarajiwa kuondoka  madarakani  mwezi  Januari  baada  ya  miaka  12 akiwa katika uongozi  wa  juu  wa  taifa  hilo  la  Afrika  Magharibi, linaloibuka  kutoka  katika  mavumbi  ya  vita  vya  wenyewe  kwa wenyewe,(1989-2003) na pia kushughulikia hatua za kupambana  na mzozo  wa  ugonjwa  wa  Ebola (2014-16).

DW SWAHILI.