Watanzania washinda tuzo ya fasihi ya Kiswahili Afrika
Watanzania wawili wametangazwa washindi wa Tuzo ya Kiswahili ya Mabati-Cornell ya Fasihi ya Afrika kwa mwaka 2017.
Wawili hao watazawadiwa $5,000 kila mmoja katika sherehe ambayo itafanyika jijini Nairobi mwezi ujao.
Dotto Rangimoto alishinda kwenye kitengo cha ushairi kwa mswada wake Mwanangu Rudi Nyumbani naye Ali Hilal Ali akashinda kitengo cha riwaya kwa mswada wake wa Mmeza Fupa.
Waziri wa habari, utamaduni na Sanaa Tanzania Dkt Harrison Mwakyembe amewapongeza wawili hao kwa ushindi huo na kusema ushindi wao "unachagiza juhudi za serikali kuibidhaisha lugha ya Kiswahili."
"Ushindi wa Watanzania hawa ni ushindi wa taifa kwa ujumla," amesema Dkt Mwakyembe kupitia taarifa.
Tuzo hiyo ilianzishwa mwaka 2014 na Dkt Lizzy Attree (Mkurugenzi wa Tuzo ya Caine) na Dkt Mukoma wa Ngugi (Chuo Kikuu cha Cornell, Marekani), kwa lengo la kuthamini uandishi kwa lugha za Kiafrika.
Aidha, tuzo hiyo inakusudiwa kuhimiza sanaa ya tafsiri baina ya lugha za Kiafrika zenyewe kwa zenyewe, na pia kutafsiri maandishi ya lugha nyengine kwa lugha za Kiafrika.
Wengine waliokuwa wanashindania tuzo hiyo ni: Mbaruk Ally - Hali Halisi (ushairi); Hassan Omar Mambosasa - Nsungi (riwaya); Mwenda Mbatiah - Kibweta cha Almasi (riwaya) na Richard Atuti Nyabuya - Umalenga wa Nyanda za Juu (ushairi).
Majaji walikuwa Ken Walibora Waliaula (Mwenyekiti wa Majaji), mwanataaluma na mwandishi; Daulat Abdalla Said, mwanataaluma na mwandishi, anayesomesha Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar; na Ali Attas, mwandishi na mwalimu wa Kiswahili na Kiingereza, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje, Japan.
"Mashairi yaliyomo katika diwani hii yametumiliwa lugha iliyojaa taswira na majazanda yanayowakilisha vyema hisia zinazoelezwa katika dhamira mbalimbali," walisema majaji kuhusu diwani ya Mwanangu Rudi Nyumbani.
"Mshairi amefaulu sana kuzitumia mbinu na miundo kadha wa kadha ili kuyajadili maswala yanayohusu hali na mazingira tafauti tafauti katika maisha ya binadamu. Anayazungumza maswala mazito mazito, lakini kwa namna ambayo hayamuelemei msomaji wake."
Walimsifu pia Bw Ali Hilal na kusema: "Si mno mtu kukutana na riwaya ya Kiswahili ambayo mwandishi wake amejidhihirisha kuwa ni mbuji wa lugha fasaha na ya kisanii, inayotiririka kitabia kwa hiari yake, na bila ya kuonesha dalili zozote kwamba imelazimishwa."
"Licha ya kwamba matukio ya riwaya hii yanatokea katika kisiwa cha kubuni, maswala yanayojadiliwa humu ni miongoni mwa yale maswala sugu yanayoendelea kulisumbua bara la Afrika kisiasa, kijamii na kiuchumi."
Tuzo ya Kiswahili ya Mabati-Cornell ya Fasihi ya Kiafrika, yenye thamani ya jumla ya Dola za Marekani 15,000, hutolewa kila mwaka kwa miswada bora, au kwa vitabu vilivyochapishwa miaka miwili kabla ya mwaka wa kutolewa zawadi, katika fani za riwaya, ushairi, wasifu na riwaya za picha.
Miswada inayoshinda huchapishwa na shirika la uchapishaji vitabu la East African Educational Publishers (EAEP) na shirika la uchapishaji vitabu la Mkuki na Nyota Publishers
Na mswada bora wa ushairi hufasiriwa kwa Kiingereza na kuchapishwa kitabu na shirika la Africa Poetry Book Fund.
Tuzo hii inadhaminiwa na kampuni ya Mabati Rolling Mills, Kenya, na kampuni ya ALAF Limited, Tanzania na pia Ofisi ya Makamu wa Mkuu wa Masuala ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Cornell, na Idara ya Taaluma za Afrika ya Chuo Kikuu cha Cornell, Marekani.
0 comments: