Wednesday, 17 January 2018

Polisi Tanzania yakana taarifa upigaji marufuku vimini



Polisi nchini Tanzania, imekanusha taarifa zilizoenea kwamba imepiga marufuku uvaaji wa nguo fupi au 'miniskirt' na vile vile nguo zinazobana. Kamanda wa polisi Mkoa wa Dar es Salaam Lazaro Mambosasa amesema taarifa hizo ambazo zimeandikwa katika moja ya magazeti nchini sio za kweli, na "zimetengenezwa" na "kuchongwa" kwa lengo la kutafuta umaarufu.

Kutokana na taarifa hizo zilizozagaa katika mitandao ya kijamii, mjadala mkali uliibuka katika mitandao ya kijamii huku baadhi wakihoji, ni kipengele gani cha sheria kitakachotumiwa kukamata watu watakao kuwa wamevaa nguo fupi.

Hata hivyo, ikumbukwe kwamba, nchini Tanzania, kuna utaratibu wa mavazi maalumu hasa katika majengo ya ofisi za serikali, ambapo wafanyakazi na wageni wanatakiwa kufuata muongozi huo.
Kwa mujibu wa menejimenti ya utumishi wa umma, wanawake na wanaume wafanyakazi wa umma hawaruhusiwi kuvaa kaptula kazini.

Picha ya muongozo wa mavazi zinabandikwa katika sehemu za kuingilia majengo ya umma, ili kuelekeza wasimamizi na wageni utaratibu wa sehemu hio. Wengi watakaokosa kufuata uratatibu mara nyingi hurudishwa au huelekezwa kutafuta vazi la kujistiri, kama vile khanga kwa wanawake.
Japo nguo hizi zinaweza kutafsiriwa kama mojawapo za nguo za kitamaduni, haziruhusiwi katika majengo ya umma Tanzania.

Wafanyakazi hawaruhusiwi kuvaa nguo zenye michoro na maandishi au picha ambazo utawala wa utumishi wa umma umeelezea kuwa 'haziendani na shughuli za serikali.' Pamoja na hayo wafanyakazi wa umma wamepigwa marufuku kuvaa nguo zenye maandishi ya chama chochote cha siasa au kuonesha ushabiki wa kitu fulani.
Nguo ambazo zinaacha sehemu ya mwili wazi kama vile kitovu na kifua au zinazoonyesha maungo ya mwili.

Je, unakubaliana na muongozo huu? Je, katika nchi yako kuna utaratibu gani wa mavazi?

Picha :OFISI YA RAIS,MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA, JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

0 comments: