Monday, 15 January 2018

Serikali Yasitisha Uchimbaji Madini Mgodi wa ZEM

Serikali imesitisha kwa muda usiojulikana shughuli za uchimbaji wa madini katika mgodi wa dhahabu wa ZEM uliopo kijiji cha Nyasirori wilaya ya Butiama mkoa wa Mara.

Imesema imechukua uamuzi huo baada ya uongozi wa mgodi huo kushindwa kutekeleza maagizo ya Serikali, ikiwa ni pamoja na kuboresha maslahi ya wafanyakazi.

Uamuzi wa kusitisha uchimbaji wa dhahabu katika mgodi huo umetolewa  Januari 13, mwaka 2018 na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo baada ya kufanya ziara mgodini hapo.

Akiwa mgodini hapo, Nyongo aliutaka uongozi wa mgodi kumkutanisha na wafanyakazi, hasa wachimbaji jambo ambalo lilishindikana baada ya kuzungushwa maeneo mbalimbali bila kuona mfanyakazi yoyote.

 “Mbona muda unazidi kwenda hao wachimbaji hawafiki, hebu twendeni huko huko (chini ya ardhi) nataka niongee nao nione kama mmetimiza maagizo ya Serikali mliyopewa wiki mbili zilizopita," amesema Nyongo.

Baada ya kufika eneo la uchimbaji, naibu waziri huyo aliombwa asubiri kwa maelezo kuwa wachimbaji hao wameitwa, kujikuta akiganda kwa zaidi ya saa moja.

Kufuatia hali hiyo aliutaka uongozi wa mgodi kusitisha shughuli za uchimbaji hadi hapo utakapotekeleza maagizo waliyopewa, kubainisha kuwa ingawa Serikali inasisitiza uwekezaji haipo tayari kuona wananchi wake wakinyanyasika.

Wakati Nyongo akisema kwa mujibu wa taratibu na sheria, wachimbaji hao wanapaswa kulipwa mshahara usiopungua Sh400,000, meneja rasilimali watu wa mgodi huo, Luo Giriquam amesema hawakuwaficha wafanyakazi hao.

“Hatukuwaficha, uongozi uliwatafuta bila mafanikio kwa vile walikuwa ndani ya shimo wakiendelea na shughuli zao,” amesema na kuahidi kutekeleza maagizo ya Serikali.

0 comments: