Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo Januari 17, 2018 amepiga marufuku aina yoyote ya michango katika shule za Serikali za msingi na Sekondari na kuwaagiza Mawaziri Jafo na Ndalichako kusimamia hilo.
Magufuli amepiga marufuku hiyo hiyo leo alipokutana na Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Selemani S. Jafo na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Profesa Joyce L. Ndalichako Ikulu jijini Dar es salaam na kuwataka mawaziri hao kwenda kusimamia jambo hilo na kuhakikisha hakuna michango yoyote wanafunzi au wazazi wanachangishwa kwenye shule za sekondari.
"Tumesema elimu bure, haiwezi ikaja kwa mgongo mwingine ikawa elimu pesa . Tumeweka utaratibu kwamba kuanzia shule ya msingi mpka sekondari form four hakuna kulipa ada yoyote lakini sasa hivi michango ya kila aina, nimewapa maelekezo kwamba kuanzia leo iwe ni marufuku na wakalisimamie hili sitaki kusikia mwanachi yoyote mahali popote akilalamika kwamba mtoto wake amerudishwa shule kwa sababu ya michango na walimu wote popote walipo wasishike mchango wowote wa mwanafunzi" amesema Rais Magufuli.
Aidha Rais Magufuli amesema kuwa kama kutakuwepo na mchango wowote wa mzazi ambaye atajisikia kuchangia jambo lolote kuhusu masuala ya shule basi pesa hizo zipelekwe kwa Mkurugenzi na si kushikwa na mwalimu yoyote yule
0 comments: