Thursday 11 January 2018

Nape Nnauye Aapa Kufia CCM......Adai Magari ya Upinzani Yameanza Kuzama na Haijulikani Yataibuka Lini

Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye (CCM), amesema kuwa hana mpango wa kuhamia chama chochote cha upinzani na ataendelea kubaki ndani ya CCM.

Alisema hawezi kufanya uamuzi wa kuhamia katika vyama vya upinzani , huku akidai magari ya upinzani kwa sasa yanazidi kuzama na haijulikani yataibuka lini.

Kauli hiyo aliitoa mjini Songea wakati akimnadi mgombea Ubunge wa Songea kupitia CCM, DK. Damas Ndumbaro katika mkutano wa kampeni uliofanyika kata ya Bombambili mjini hapa.

Nape ambaye pia aliwahi kuwa katibu Mwnezi wa CCM, alisema kama kuna watu walidhani atakihama chama tawala CCM na kujiunga na upinzani wasahau.

Alisema matatizo ya chama humalizwa ndani ya chama na si kukihama kama walivyofanya wanachama wengine waliokimbia ndani ya CCM.

“Naikubali serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Jemedari DK. John Magufuli pamoja na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa. Ni serikali yenye viongozi imara na mimi naapa kufia CCM na sivinginevyo.

“Nasikia maneno maneno kutoka kwa baadhi ya watu wakisema Nape anataka kuhamia upinzani jambo ambalo siyo la kweli kuanzia leo watu hao waondokane na mawazo hayo,” alisema Nape

0 comments: