Sunday 7 January 2018

Waziri Mkuu awataka mawaziri kutoa taarifa za fedha za miradi ya maendeleo


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka mawaziri, naibu mawaziri, makatibu wakuu, wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi kujenga utamaduni wa kutoa taarifa za fedha  za miradi ya maendeleo kwa wananchi badala ya kusubiri kufanya hivyo katika ziara za viongozi wakuu.

Majaliwa ametoa agizo hilo jana Jumamosi Januari 6,   wakati akizungumza na watumishi na madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Nyasa kwenye kikao kilichofanyika mjini Mbamba Bay, wilayani Nyasa mkoani Ruvuma.

“Kuanzia sasa ninaagiza, viongozi wote wa ngazi za juu wakiwemo mawaziri hadi wakurugenzi na hata ninyi wakuu wa idara mnawajibika kutoa taarifa za fedha tunazopeleka kwenye miradi kwa sababu wananchi wana haki ya kujua utekelezaji wa ahadi za Serikali,” amesema.

Amewataka kila wanapoenda kwenye ziara ya kikazi vijijini, waelezee thamani za kazi zilizofanyika na waeleze ni lini miradi hiyo itakamilika.

“Mnapopata fursa ya kupanda jukwaani, tumieni wasaa huo kueleza kazi kubwa ambazo zimefanywa na Serikali,” amesema na kuongeza,

“Elezeni Serikali imeleta fedha kiasi gani, kwa ajili ya kitu gani na kwa kufanya hivyo, mtasaidia kutoa taarifa za utekelezaji wa ahadi zilizotolewa na Rais John Magufuli wakati wa kampeni.”

Amesema wananchi wana haki ya kupatiwa taarifa za utendaji wa Serikali yao na akawataka viongozi hao wasisubiri ziara za viongozi wa kitaifa.

 “Nendeni mkaongee na wananchi, msiwaachie wakuu wa wilaya au wabunge peke yao ndiyo waseme na wananchi,” amesema.

0 comments: