WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika amesema kuwa, ofisi yake haiungi mkono mfumo wa kazi kwa mikataba.
Waziri Mkuchika ameongeza kuwa, mfumo huo ni gharama kubwa ukilinganisha na kuajiri mfanyakazi kwa ajira ya kudumu na kwamba wizara yake inashughulikia suala hilo na kwamba hivi karibuni taasisi za umma hazitaruhusiwa kuajiri wafanyakazi wapya kwa mfumo wa mikataba.
“Tunataka kila ofisi kuajiri kwa mujibu wa mahitaji, hatutaruhusu mfumo huu wa mikataba kuendelea kwa sababu ni gharama kubwa mno kwa serikali,” alisema.
Kuhusu wafanyakazi wanaokwenda likizo maalum, waziri alisema yeyote atakayekwenda katika likizo ya namna hiyo atatakiwa kuwasilisha nyaraka zake wizarani lini anarudi na wale watakaowasilisha barua kuwa wamerudi wanatakiwa kusubiri jibu la serikali.
“Kama ulikuwa nje ya nchi au ofisi mfano miaka mitano, ni dhahiri kuna mtu alijaza nafasi yako, hivyo unaporudi, unatakiwa kuwasilisha barua na kuipa nafasi serikali kujibu,” alifafanua Waziri Mkuchika.
Ameeleza kwamba, suala la likizo maalum sio jambo jipya katika mfumo wa utumishi wa umma na umekuwa ukitumika katika nchi nyingi duniani
“Hatuna shida nayo, lakini tunataka wafuate taratibu sahihi wanaporudi.”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuchika amesema kuwa, Bodi ya Mishahara na Maslahi (HSRB) iko katika hatua za mwisho za kurekebisha mfumo mzima wa mishahara, utakaondoa tofauti ya uwiano wa mishahara katika taasisi za umma kwa wafanyakazi wenye ujuzi, sifa na uzoefu.
0 comments: