Monday, 25 December 2017

Maamuzi Yasubiriwa toka Kamati ya TFF Dhidi ya Mechi Mbili ambazo Hazikuchezwa

Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) inasubiriwa kutoa maamuzi juu ya mechi mbili za kombe shirikisho ambazo hazikufanyika katika hatua ya 64 Bora kutokana na baadhi ya wachezaji kukosa leseni.

Mechi hizo ni ile ya Abajalo ya Daraja la Kwanza dhidi ya Tanzania Prisons na  Mvuvumwa (Daraja la Kwanza) na JKT Ruvu Ligi Kuu.

Sababu ya kutochezwa kwa michezo hiyo ilitokana na mfumo wa usajili kwa njia ya mtandao wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) maarufu (TMS) kufeli hali iliyosababisha klabu kushindwa kukamilisha usajili kwa wakati kupitia mfumo huo.

Wakati huo huo timu 12 za Ligi Kuu Tanzania Bara, 11 za Daraja la Kwanza, tatu za Daraja la Pili na nne za Ligi ya Mabingwa wa Mikoa zimefuzu hatua ya 32 ya michuano ya Kombe la Shirikisho Tanzania (FA).

Timu za Ligi ya Mabingwa wa mikoa zilizofuzu ni Buseresere FC ya Geita, Majimaji Rangers ya Nachingwea, Lindi, Kariakoo United ya Lindi Mjini na Shupavu FC ya Morogoro. Mabingwa watetezi wa kombe hilo Simba SC ilitupwa nje ya mashindano na Green Worriors ya Dar es salaam Jumamosi iliyopita.

0 comments: