Siku ya Jumatano, pande zinazozozana katika mzozo wa mashariki ya
Ukraine, zilikubaliana kuhusu mpango wa kuweka chini silaha ambao
utatekelezwa katika kipindi cha Krismasi na Mwaka Mpya. Maafisa wa
Ukraine, waangalizi wa kiusalama na washirika wa kimataifa walionya kuwa
uamuzi wa Urusi kujiondoa katika kundi la Urusi na Ukraine la kudhibiti
usitishwaji vita huenda kukaongeza mapigano Mashariki mwa Ukraine.
Katika
taarifa yao ya pamoja, Merkel na Macron wamesema hakuna njia mbadala
kwa makubaliano ya Amani. Wamewataka maafisa wa Urusi kurudi katika jopo
hilo la pamoja la udhibiti na uratibu wa usitishwaji vita. Urusi
iliilaumu Ukraine kwa kuzuia kazi zao na kupunguza uwezo wao kufika
katika maeneo ya vita.
Wakati huo huo, Moscow, Urusi imesema leo
kuwa Marekani inahimiza kile imekitaja kuwa ni umwagikaji upya wa damu
mashariki mwa Ukraine kufuatia uamuzi wake wa kuipa Ukraine silaha
hatari zaidi.
Katika taarifa yenye maneno mazito, naibu waziri wa mambo ya nje wa
Urusi Sergei Ryabkov, ameilaumu Marekani kwa kuvuka mstari na kuchochea
machafuko Mashariki mwa Ukraine, eneo linalofahamika kama Donbass.
Ryabkov
amesema silaha mpya za Marekani zinaweza kusababisha kuwepo kwa
waathiriwa wapya miongoni mwa majirani zao. Naibu mwengine wa waziri wa
mambo ya nje Grigory Karasin amesema hatua ya Marekani itahujumu juhudi
za kutafuta suluhisho la kisiasa nchini Ukraine.
Wizara ya mambo
ya nje ya Marekani ilitangaza Ijumaa kwamba Marekani imeamua kuipa
Ukraine silaha imara zaidi za ulinzi kama sehemu ya juhudi za kuisaidia
Ukraine katika mipango yake ya muda mrefu ya kujiimarisha kiulinzi.
Silaha
hizo mpya zinajumuisha vifaru vilivyoundwa Marekani vya kuzuia
makombora. Ukraine imekuwa ikihitaji vifaru hivyo ili kuimarisha ulinzi
wake dhidi ya vifaru ambavyo vimekuwa vikishambulia mashariki ya Ukraine
wakati wa vita ambavyo vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 10,000
tangu mwaka 2014. Awali, Marekani iliipa Ukraine msaada wa vifaa na
mafunzo na pia imeruhusu makampuni binafsi kuiuzia Ukraine silaha
ndogondogo kama bunduki. Maafisa walioeleza kuhusu mpango huo
hawakuruhusiwa kuuzungumzia na hivyo walitaka wasitambulishwe majina.
Ukraine inailaumu Urusi kwa kutuma vifaru. Marekani pia imedai Urusi
inawapa silaha na mafunzo kando na kusaidia wanaotaka kujitenga.
DW Swahili.
0 comments: