Dar es Salaam. Mahakama Kuu imetupa maombi ya Swabaha Mohamed aliyeangua kilio mbele ya Rais John Magufuli akidai kudhulumiwa mirathi ya mumewe, baada ya kujiridhisha kuwa sababu alizotoa hazikuwa na ukweli.
Katika maombi hayo, Swabaha alitaka ateuliwe kuwa msimamizi wa mirathi.
Mama huyo anayedai ni mjane wa Mohamed Shosi Yusufu wa mkoani Tanga alikuwa akiomba kuongezewa muda wa kukata rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama ya Wilaya Tanga.
Mahakama ya Wilaya Tanga ilitupilia mbali rufaa yake ya kupinga uamuzi wa Mahakama ya Mwanzo Tanga kumteua Saburia Shosi ambaye ni mtoto wa marehemu kuwa msimamizi wa mirathi hiyo badala yake.
Mahakama Kuu katika uamuzi uliotolewa Jumatano na Jaji Amour Khamis, imeyatupa maombi hayo baada ya kuridhika kuwa sababu zake za kuomba kuongezewa muda si za kweli.
Katika uamuzi huo, Jaji Khamis alikubali hoja za Saburia kupitia kwa wakili wake, Abdon Rwegasira kuwa mwombaji (Swabaha) hakutoa sababu za msingi za kustahili kuongezewa muda wa kukata rufaa na kwamba sababu ya ugonjwa na kulazwa aliyoitoa si ya kweli.
Hii ni mara ya pili kwa Swabaha kufungua maombi mahakamani hapo akiomba kuongezewa muda wa kukata rufaa.
Ombi la awali lilitupwa kutokana na kutokuwa na sababu za msingi kisheria za kuchelewa kukata rufaa.
Awali, alifungua maombi mwaka 2016 akidai alichelewa kupata nakala ya mwenendo wa kesi na hukumu aliyokuwa anataka kuikatia rufaa.
Oktoba 2016 Mahakama Kuu katika uamuzi uliotolewa na Jaji Khamis iliyatupilia mbali maombi hayo.
Mapema mwaka huu alifungua tena maombi hayo mahakamani hapo na akatoa sababu nyingine, akidai alichelewa kukata rufaa kwa kuwa alikuwa amelazwa hospitalini kutokana na kuwa mgonjwa.
Aliwasilisha mahakamani kadi ya kuruhusiwa kutoka Tanga Central Health Centre, ikionyesha alilazwa Oktoba 9, 2016 na akaruhusiwa Oktoba 16, 2016.
Wakili Rwegasira aliwasilisha mahakamani barua na kiapo cha mkurugenzi wa kituo hicho aliyejitambulisha kuwa ni Dk H. I. Ngayomela, akikana mama huyo kulazwa hospitalini kwake.
Dk Ngayomela alisema ingawa kadi inaonekana ni ya hospitali yake, lakini hajui aliipataje, huku akisema tarehe ya kulazwa na kuruhusiwa pamoja na namba ya jalada vinavyoonekana katika kadi hiyo ni vya mgonjwa mwingine tena wa kiume.
Alisema mwandiko kwenye kadi haufanani na wa daktari yeyote kituoni kwake, huku akidai haina saini.
Siku chache baadaye, Swabaha aliwasilisha maelezo mengine mahakamani ambayo hata hivyo, yalikuwa yameandikwa kwenye karatasi bila kubainisha kuwa imeandikwa kwa nani, akidai inatoka kwa Dk Ngayomela akikiri kumtambua na kwamba kuna makosa yalifanyika wagonjwa wawili wakapewa namba moja ya jalada.
Maelezo hayo yalisababisha wakili Rwegasira aiombe Mahakama mama huyo afike mahakamani kuhojiwa kuhusu mkanganyiko huo na alishindwa kutoa maelezo ya kuiridhisha Mahakama.
Jaji Khamis katika uamuzi wake alisema amebaini kuwa kuna ufa wa wazi katika madai ya mama huyo ya kuugua na kulazwa, kutokana na kushindwa kutaja hata jina la daktari au muuguzi aliyemhudumia kwa siku saba.
Alisema hata barua ya pili ya Dk Ngayomela inayoeleza kumtambua haiwezi kufafanua na kuondoa shaka ya tuhuma alizotoa mwanzoni kwenye kiapo cha upande wa mjibu maombi.
Jaji Khamis alisema Swabaha katika mahojiano mahakamani hakuweza kufafanua utata huo na kwamba, majibu yake wakati wa madodoso, akihojiwa na wakili Rwegasira yalikuwa ni ya kujikanganya.
“Mwombaji alishindwa hata kutaja majina ya madaktari na wauguzi waliokuwa wakimhudumia kwa muda wa siku saba alizodai alilazwa hospitalini hapo. Alimtaja Dk Ngayomela tu kama anayeweza kumkumbuka katika orodha ya madaktari waliomhudumia katika ugonjwa wake,” alisema.
Jaji Khamis alisema, “Kwangu hili haliwezi kuwa kweli kwa sababu kama angekuwa amemhudumia kama alivyodai asingeweza (Dk Ngayomela) kushindwa kutambua mwandiko wake katika kadi ya kuruhusiwa kutoka hospitalini, kwa kiwango cha kukana uhalali wake kwa kiapo.”
Alisema maombi hayo hayana mashiko hivyo kuyafuta na kuamuru Swabaha kulipa gharama za uendeshaji wa shauri hilo.
0 comments: