Sunday 31 December 2017

Kocha Shedrack Nsajigwa waYanga ameshindwa kuvunja mwiko wa kuifunga Mbao FC uwanja wa CCM Kirumba Mwanza



Kocha Shedrack Nsajigwa waYanga ameshindwa kuvunja mwiko wa kuifunga Mbao FC uwanja wa CCM Kirumba Mwanza

Yanga leo imejikutaikiangukiapuaMjini Mwanzabaadayakupokeakipigo cha mabao 2-0,kutoka kwawenyeji wao Mbao FC, huo ukiwani mchezo waLigi Kuu ya Tanzania Bara mzungukowa 12 ambao umepigwa uwanja wa CCM Kirumba Mwanza.

Kipigo hicho cha leo kimeishuka Yanga kwenye msimamo kutoka nafasi ya tatu ilipokuwahadi nafasi ya nne na kuipisha Singida United kwenye nafasi hiyo huku Simba na Azam zikiendelea kujinafasi kwenye nafasi mbili za juu.
 anga ambayo ilicheza bila nyota wake watano wa kikosi cha kwanza ambao wana matatizo mbali mbali wengine wakiwani majeruhi nawengine matatizo yakifamilia.

Wachezaji Habibu Haji na Boniface Maganga, ndio walipeleka kilio Jangwani na kufanya timu hiyo kuendelea kuwana wakati mbaya inapocheza kwenye uwanja wa CCM Kirumba baada yamsimu uliopita pia kupoteza mechi zote mbili dhidi ya Mbao FC.

Katika kipindi cha kwanza timu zote zilizcheza kwa nguvu na kushambuliana kwa kasi lakini washambuliaji wa timu zote mbili walishindwa kuzitumiavyema nafasi walizozipata  na kufanya matokeo kuwa sare katika dakika 45 za kipindi cha kwanza.

Kipindi cha pili ndipo mambo yalipoanza kubadilika kwa vijana waYanga kushindwa kuhimili kasi ya Mbao FC, na kujikuta wakipachikwa bao la kwanza dakika ya 53 mfungaji akiwa Haji ambaye alifanya kazi nzuri baada ya kupokea pasi kutoka upande wa kushoto.

Bao hilo lilionekana kuwazindua Yanga nakufanya mashablizi mengi kwenye lango la Mbao lakini ulinzi wa kocha Ettienne Ndayiragije ulikuwa makini na kuondosha hatari zote langoni mwao.

Wakati Yanga wanapambana kusawazisha bao hilo walijikuta wakipachikwa bao la pili dakika ya 68, baada yamabeki wake kufanya uzembe ambao ulimfanya Boniface Maganga kuifungia timu yake bao hilo lililoipa ushindi wa pili msimu huu wakiwanyumbani.

Maandamano Makubwa nchini Irani.
Kumeshuhudiwa misururu mibaya ya ghasia kati ya waandamanaji na walinda usalama nchini Iran.

Mikanda ya video iliyowekwa katika mitandao ya kijamii, inaonesha, waandamanaji wawili wakipigwa risasi katika mji wa Dorud- Magharibi mwa taifa hilo.

Huko Ab-har, Kaskazini mwa taifa, waandamanaji waliteketeza bango kubwa iliyo na picha ya kiongozi mkuu wa kidini wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei.

Gari pamoja na pikipiki moja ya polisi, ziliteketezwa moto na waandamanaji huko Mashdad.


    Marekani yaiwekea Iran vikwazo



    Iran yawanyonga 'magaidi' 20



    Marekani yaiwekea Iran vikwazo



Katika mji mkuu Teh-ran, maelfu ya watu waliandamana hadi katika uwanja mmoja wa mkutano, ulioko katikati mwa mji huo, huku wakitoa wito kwa jeshi na polisi kuungana nao.
Mahakama Kuu yatupa ombi la mjane aliyemlilia JPM
Dar es Salaam. Mahakama Kuu imetupa maombi ya Swabaha Mohamed aliyeangua kilio mbele ya Rais John Magufuli akidai kudhulumiwa mirathi ya mumewe, baada ya kujiridhisha kuwa sababu alizotoa hazikuwa na ukweli.

Katika maombi hayo, Swabaha alitaka ateuliwe kuwa msimamizi wa mirathi.

Mama huyo anayedai ni mjane wa Mohamed Shosi Yusufu wa mkoani Tanga alikuwa akiomba kuongezewa muda wa kukata rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama ya Wilaya Tanga.

Mahakama ya Wilaya Tanga ilitupilia mbali rufaa yake ya kupinga uamuzi wa Mahakama ya Mwanzo Tanga kumteua Saburia Shosi ambaye ni mtoto wa marehemu kuwa msimamizi wa mirathi hiyo badala yake.

Mahakama Kuu katika uamuzi uliotolewa Jumatano na Jaji Amour Khamis, imeyatupa maombi hayo baada ya kuridhika kuwa sababu zake za kuomba kuongezewa muda si za kweli.

Katika uamuzi huo, Jaji Khamis alikubali hoja za Saburia kupitia kwa wakili wake, Abdon Rwegasira kuwa mwombaji (Swabaha) hakutoa sababu za msingi za kustahili kuongezewa muda wa kukata rufaa na kwamba sababu ya ugonjwa na kulazwa aliyoitoa si ya kweli.

Hii ni mara ya pili kwa Swabaha kufungua maombi mahakamani hapo akiomba kuongezewa muda wa kukata rufaa.

Ombi la awali lilitupwa kutokana na kutokuwa na sababu za msingi kisheria za kuchelewa kukata rufaa.

Awali, alifungua maombi mwaka 2016 akidai alichelewa kupata nakala ya mwenendo wa kesi na hukumu aliyokuwa anataka kuikatia rufaa.

Oktoba 2016 Mahakama Kuu katika uamuzi uliotolewa na Jaji Khamis iliyatupilia mbali maombi hayo.

Mapema mwaka huu alifungua tena maombi hayo mahakamani hapo na akatoa sababu nyingine, akidai alichelewa kukata rufaa kwa kuwa alikuwa amelazwa hospitalini kutokana na kuwa mgonjwa.

Aliwasilisha mahakamani kadi ya kuruhusiwa kutoka Tanga Central Health Centre, ikionyesha alilazwa Oktoba 9, 2016 na akaruhusiwa Oktoba 16, 2016.

Wakili Rwegasira aliwasilisha mahakamani barua na kiapo cha mkurugenzi wa kituo hicho aliyejitambulisha kuwa ni Dk H. I. Ngayomela, akikana mama huyo kulazwa hospitalini kwake.

Dk Ngayomela alisema ingawa kadi inaonekana ni ya hospitali yake, lakini hajui aliipataje, huku akisema tarehe ya kulazwa na kuruhusiwa pamoja na namba ya jalada vinavyoonekana katika kadi hiyo ni vya mgonjwa mwingine tena wa kiume.

Alisema mwandiko kwenye kadi haufanani na wa daktari yeyote kituoni kwake, huku akidai haina saini.

Siku chache baadaye, Swabaha aliwasilisha maelezo mengine mahakamani ambayo hata hivyo, yalikuwa yameandikwa kwenye karatasi bila kubainisha kuwa imeandikwa kwa nani, akidai inatoka kwa Dk Ngayomela akikiri kumtambua na kwamba kuna makosa yalifanyika wagonjwa wawili wakapewa namba moja ya jalada.

Maelezo hayo yalisababisha wakili Rwegasira aiombe Mahakama mama huyo afike mahakamani kuhojiwa kuhusu mkanganyiko huo na alishindwa kutoa maelezo ya kuiridhisha Mahakama.

Jaji Khamis katika uamuzi wake alisema amebaini kuwa kuna ufa wa wazi katika madai ya mama huyo ya kuugua na kulazwa, kutokana na kushindwa kutaja hata jina la daktari au muuguzi aliyemhudumia kwa siku saba.

Alisema hata barua ya pili ya Dk Ngayomela inayoeleza kumtambua haiwezi kufafanua na kuondoa shaka ya tuhuma alizotoa mwanzoni kwenye kiapo cha upande wa mjibu maombi.

Jaji Khamis alisema Swabaha katika mahojiano mahakamani hakuweza kufafanua utata huo na kwamba, majibu yake wakati wa madodoso, akihojiwa na wakili Rwegasira yalikuwa ni ya kujikanganya.

“Mwombaji alishindwa hata kutaja majina ya madaktari na wauguzi waliokuwa wakimhudumia kwa muda wa siku saba alizodai alilazwa hospitalini hapo. Alimtaja Dk Ngayomela tu kama anayeweza kumkumbuka katika orodha ya madaktari waliomhudumia katika ugonjwa wake,” alisema.

Jaji Khamis alisema, “Kwangu hili haliwezi kuwa kweli kwa sababu kama angekuwa amemhudumia kama alivyodai asingeweza (Dk Ngayomela) kushindwa kutambua mwandiko wake katika kadi ya kuruhusiwa kutoka hospitalini, kwa kiwango cha kukana uhalali wake kwa kiapo.”

Alisema maombi hayo hayana mashiko hivyo kuyafuta na kuamuru Swabaha kulipa gharama za uendeshaji wa shauri hilo.
Serikali Imetoa Tamko Kuhusu Matumiizi ya Fedha za Kigeni Hapa Nchini

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango ametoa maagizo kuhusu matumizi ya fedha za kigeni katika  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kusisitiza kuwa utekelezaji wake uanze  tarehe 1 Januari, 2018.  Maagizo hayo ni kama ifuatavyo: –

    Bei zote hapa nchini zitangazwe kwa shilingi ya Tanzania. Bei hizi zinajumuisha kodi ya nyumba za kuishi na maofisi, bei ya ardhi, gharama za elimu na afya, bei za vyombo vya usafiri na vifaa vya kielektroniki.
    Bei ambazo walengwa wake wakuu ni watalii au wateja wasio wakazi zinaweza kutangazwa kwa fedha za kigeni na malipo yake yanaweza kufanyika kwa fedha za kigeni. Bei hizi zinajumuisha gharama za usafirishaji kwenda nchi za nje kupitia Tanzania, gharama za mizigo bandarini kwenda nchi za nje, gharama za viwanja vya ndege na viza kwa wageni, na gharama za hoteli kwa watalii kutoka nje ya nchi. Walipaji wanaotumia fedha za kigeni watambuliwe kwa vitambulisho vyao kama pasi za kusafiria na nyaraka za usajili kwa makampuni.
    Viwango vya kubadilishana fedha vitakavyotumika katika kuweka hizo bei katika sarafu mbili viwekwe wazi na visizidi vile vya soko. Ifahamike wazi kuwa ni mabenki na maduka ya fedha za kigeni tu yanayoruhusiwa kupanga viwango vya kubadilisha fedha kutokana na ushindani katika soko la fedha za kigeni.
    Mkazi yeyote wa Tanzania asilazimishwe kulipia bidhaa au huduma yeyote hapa nchini kwa fedha za kigeni.

Aidha Dkt. Mpango ameviagiza vyombo vya dola viwachukulie hatua za kisheria wale wote watakaobainika kukiuka maagizo haya ya Serikali.

IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI

WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO


Alichokiandika mke wa Kafulila baada ya kuonana na Tundu Lissu leo
Leo December 30, 2017 Mke wa aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila ambaye pia ni Mbunge wa viti maalum Singida Jesca Kishoa alikuwa Nairobi Kenya ambapo alienda kumjulia hali Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu aliyeshambuliwa kwa risasi akiwa nyumbani kwake Dodoma na watu wasiojulikana.

Kupitia account yake ya Instagram aliandika jumble usemao….”Shauku yake ya kulitetea taifa hili imeongezeka mara 100000000000….. Aisee ni kama kuzima moto kwa petrol… Wasiojulikana wamemfanya awe jasiri zaidi.Glory to the Almighty God.Aluta Continua“


Kanusho la taarifa inayosambazwa kumuhusu Makamu wa Rais
Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inakanusha tangazo linalosambaa katika Mitandao ya Kijamii linalomhusisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan  kuwa atashiriki zoezi la kupanda miti kwenye Chuo Kikuu Cha Dodoma siku ya tarehe 1-1-2018.

Ofisi ya Makamu wa Rais inapenda kuujulisha umma kuwa tangazo hilo si la kweli na Makamu wa Rais hana ratiba ya kupanda miti kwenye chuo hicho kwa tarehe iliyotajwa.

Ikumbukwe kuwa siku ya tarehe 15-12-2017 wakati wa hafla ya kuhamia Makao Makuu ya Nchi, Makamu wa Rais wa  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alitangaza kampeni ya kupanda miti Dodoma ambayo itaratibiwa na Ofisi yake .

Ofisi ya Makamu wa Rais inawataka Wananchi kuzingatia matangazo, taarifa na ratiba zitakazotolewa na Ofisi yake kuhusu programu ya upandaji miti Dodoma.

 Imetolewa na:
Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dodoma

 30 Desemba, 2017.
Mjumbe Wa Halmashauri Kuu Ya Ccm Mkoa Wa Arusha Robert Pjn Kaseko Amjibu Askofu Zacharia Kakobe.
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Kanda ya Kusini, Bw. Ogesa Charles Tale afike eneo la mgodi wa dhahabu wa Namumgo na kuitisha kikao cha wananchi leo (Jumapili) saa 4 asubuhi.

“Sasa hivi natoka kwenda Matambare, twende wote, lakini kesho (leo) saa 4 asubuhi uje hapa Namungo, uitishe mkutano wa hadhara na uwasikilize hawa wachimbaji wadogo na kisha uniletee maelezo ofisini kwangu,” alisema.

Ametoa agizo hilo jana mchana (Jumamosi, Desemba 30, 2017), wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Namungo, wilayani Ruangwa baada ya kupokea mabango mawili kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo. Waziri Mkuu yuko kwenye mapumziko ya mwisho wa mwaka, na ameamua kukagua miradi ya maji, ujenzi wa zahanati na kuzungumza na wananchi katika wilaya hii.

Waziri Mkuu alisema Serikali ya awamu ya tano imejikita kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi na alipomuuliza afisa huyo kama ameshawahi kupata nafasi ya kuwasikiliza wachimbaji wadogo, alijibiwa kwamba hajawahi kufanya hivyo.

“Hawa ndiyo nguvukazi ya mgodi, hawa ndiyo wanaingia kule chini kuchimba udongo, hawa ndiyo wanapata machungu ya kazi ya uchimbaji, kwa hiyo uje uwasikilize na uniletee taarifa kesho mchana,” alisisitiza.

Baada ya kuyasoma mabango yao, Waziri Mkuu aliwaita wakazi ambao waliyaleta mabango hayo na kuwataka waeleze kwa undani ni matatizo gani yanayowakabili. Bango la kwanza lilisema wananchi wananyanyaswa na viongozi kwa maslahi binafsi ya viongozi na la pili lilisema wamekatazwa wasiseme matatizo yao kwenye mkutano huo wa Waziri Mkuu.

Mkazi wa kijiji cha Mtondo, kata ya Nambilanje, Bw. Mussa Omari Kimatilo, alisema wananyanyaswa na uongozi wa kijiji pamoja na uongozi wa wenye machimbo ya dhahabu na kwamba wananyimwa uhuru wa kujieleza kila wanapokutana na viongozi hao.

“Tunanyanyaswa na uongozi wa machimbo, tunanyanyaswa na uongozi wa kijiji na tukilalamika hakuna wa kutusikiliza. Tumekaa na Rajani (mmiliki wa mgodi) amekubali kutulipa lakini wananchi hatuna uhuru wa kujieleza,” alisema.

Alidai hata Naibu Waziri wa Madini alipotembelea mgodi huo mapema mwezi huu, hakupewa fursa ya kukutana na wachimabji wadogo, na badala yake alipitishwa kijijini hapo na kuingizwa mgodini kisha akaondoka.

Naye Bahati Mikael, mkazi wa kijiji cha Namungo alisema kumekuwa na ukiritimba wa kutoa leseni kuhusu mgodi huo na kwamba tangu ilipotolewa rasmi mwaka 2014, bado hawajalipwa malipo yao.

“Hapa pana ukiritimba wa kutoa leseni ya uchimbaji. Mwekezaji amekuwa akichimba kinyemela; tangu mwaka 2006 alikuwa hajapewa leseni hadi mwaka 2014 ndipo alipopewa,” alisema.

Alipoitwa na Waziri Mkuu atoe ufafanuzi juu ya madai ya wakazi hao, Kaimu Afisa Madini wa kanda hiyo alisema eneo wanalodai wakazi hao ni la Mzee Kishor Rajani na inaeleweka hivyo na kwamba miaka ya nyuma walichimba kwa maelewano tu bila mikataba yoyote.

“Yale ya nyuma yalishapita kwa sababu hamkuwa na mkataba naye, mlifanya naye kazi kwa makubaliano ya mdomo tu. Sasa hivi mmeanza kuwekeana mikataba, zamani alikuwa anachukua asilimia kubwa lakini sasa hivi anachukua asilimia 17.5 na inayobaki amewaachia ninyi,” alisema Bw. Tale.

Waziri Mkuu anaendelea na ziara ya jimboni kwake.
Waziri Mkuu amwagiza Ofisa madini aitishe kikao na wananchi.......Ni baada ya kupokea mabango ya wananchi wakidai kunyanyaswa
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Kanda ya Kusini, Bw. Ogesa Charles Tale afike eneo la mgodi wa dhahabu wa Namumgo na kuitisha kikao cha wananchi leo (Jumapili) saa 4 asubuhi.

“Sasa hivi natoka kwenda Matambare, twende wote, lakini kesho (leo) saa 4 asubuhi uje hapa Namungo, uitishe mkutano wa hadhara na uwasikilize hawa wachimbaji wadogo na kisha uniletee maelezo ofisini kwangu,” alisema.

Ametoa agizo hilo jana mchana (Jumamosi, Desemba 30, 2017), wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Namungo, wilayani Ruangwa baada ya kupokea mabango mawili kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo. Waziri Mkuu yuko kwenye mapumziko ya mwisho wa mwaka, na ameamua kukagua miradi ya maji, ujenzi wa zahanati na kuzungumza na wananchi katika wilaya hii.

Waziri Mkuu alisema Serikali ya awamu ya tano imejikita kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi na alipomuuliza afisa huyo kama ameshawahi kupata nafasi ya kuwasikiliza wachimbaji wadogo, alijibiwa kwamba hajawahi kufanya hivyo.

“Hawa ndiyo nguvukazi ya mgodi, hawa ndiyo wanaingia kule chini kuchimba udongo, hawa ndiyo wanapata machungu ya kazi ya uchimbaji, kwa hiyo uje uwasikilize na uniletee taarifa kesho mchana,” alisisitiza.

Baada ya kuyasoma mabango yao, Waziri Mkuu aliwaita wakazi ambao waliyaleta mabango hayo na kuwataka waeleze kwa undani ni matatizo gani yanayowakabili. Bango la kwanza lilisema wananchi wananyanyaswa na viongozi kwa maslahi binafsi ya viongozi na la pili lilisema wamekatazwa wasiseme matatizo yao kwenye mkutano huo wa Waziri Mkuu.

Mkazi wa kijiji cha Mtondo, kata ya Nambilanje, Bw. Mussa Omari Kimatilo, alisema wananyanyaswa na uongozi wa kijiji pamoja na uongozi wa wenye machimbo ya dhahabu na kwamba wananyimwa uhuru wa kujieleza kila wanapokutana na viongozi hao.

“Tunanyanyaswa na uongozi wa machimbo, tunanyanyaswa na uongozi wa kijiji na tukilalamika hakuna wa kutusikiliza. Tumekaa na Rajani (mmiliki wa mgodi) amekubali kutulipa lakini wananchi hatuna uhuru wa kujieleza,” alisema.

Alidai hata Naibu Waziri wa Madini alipotembelea mgodi huo mapema mwezi huu, hakupewa fursa ya kukutana na wachimabji wadogo, na badala yake alipitishwa kijijini hapo na kuingizwa mgodini kisha akaondoka.

Naye Bahati Mikael, mkazi wa kijiji cha Namungo alisema kumekuwa na ukiritimba wa kutoa leseni kuhusu mgodi huo na kwamba tangu ilipotolewa rasmi mwaka 2014, bado hawajalipwa malipo yao.

“Hapa pana ukiritimba wa kutoa leseni ya uchimbaji. Mwekezaji amekuwa akichimba kinyemela; tangu mwaka 2006 alikuwa hajapewa leseni hadi mwaka 2014 ndipo alipopewa,” alisema.

Alipoitwa na Waziri Mkuu atoe ufafanuzi juu ya madai ya wakazi hao, Kaimu Afisa Madini wa kanda hiyo alisema eneo wanalodai wakazi hao ni la Mzee Kishor Rajani na inaeleweka hivyo na kwamba miaka ya nyuma walichimba kwa maelewano tu bila mikataba yoyote.

“Yale ya nyuma yalishapita kwa sababu hamkuwa na mkataba naye, mlifanya naye kazi kwa makubaliano ya mdomo tu. Sasa hivi mmeanza kuwekeana mikataba, zamani alikuwa anachukua asilimia kubwa lakini sasa hivi anachukua asilimia 17.5 na inayobaki amewaachia ninyi,” alisema Bw. Tale.

Waziri Mkuu anaendelea na ziara ya jimboni kwake.

Friday 29 December 2017

Rais Magufuli awasilisha fomu inayotaja mali na madeni yake
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 28 Desemba, 2017 amewasilisha fomu yake ya tamko kuhusu rasilimali na madeni katika ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma iliyopo Mtaa wa Ohio, Wilaya ya Ilala Jijini Dar es Salaam.

Baada ya kuwasilisha fomu hiyo Mhe. Rais Magufuli ameipongeza Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kazi inazofanya na amemtaka Kamishna wa Maadili Jaji Mstaafu Harold Nsekela kutopokea fomu ya kiongozi yeyote ambaye atakuwa hajawasilisha tamko lake ifikapo tarehe 31 Desemba, 2017.

“Mhe. Jaji Nsekela ikifika tarehe 31 Desemba, ambayo ni siku ya mwisho kwa Mujibu wa Sheria, weka mstari na usipokee fomu zingine, halafu tuone sheria itafanyaje, nakutakia kazi njema” amesisistiza Mhe. Rais Magufuli.

Kwa upande wake Mhe. Jaji Mstaafu Harold Nsekela amemshukuru na kumpongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kutekeleza matakwa ya kisheria yanayomlazimu kujaza fomu hizo na amesisitiza kuwa ujazaji wa fomu hizo kwa viongozi wa umma sio ombi.

“Viongozi hawaombwi kujaza fomu hizi, kuna baadhi wanadhani labda kutuletea hilo tamko ni fadhila, hapana, sheria ya nchi inahitaji hivyo na kuna sababu zake za msingi” amesema Mhe. Jaji Mstaafu Nsekela.

Aidha, Mhe. Jaji Mstaafu Nsekela amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kuwasilisha taarifa ya akaunti yake ya benki sambamba na tamko hilo, na amekiri kuwa ameonesha mfano wa kuigwa na viongozi wengine.

Tamko la viongozi wa umma kuhusu rasilimali na madeni linatolewa kwa mujibu wa kifungu cha 9 na cha 11 cha sheria ya maadili ya viongozi wa umma namba 13 ya mwaka 1995.

Rais Wa Jamhuri Ya Muungano Wa Tanzania Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli akiwasili Katika Ofisi Za Sekretarieti Ya Maadili Ya Viongozi Wa Umma Jijini Dar Es Salaam kuwasilisha fomu zake za tamko la Rasilimali na madeni kwa Viongozi wa Umma Disemba 28,2017.
 Rais Wa Jamhuri Ya Muungano Wa Tanzania Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli akisalimiana na Kamishina wa Maadili Jaji Mstaafu Haroild Nsekela alipowasili Katika Ofisi Za Sekretarieti Ya Maadili Ya Viongozi Wa Umma Jijini Dar Es Salaam kuwasilisha fomu zake za tamko la Rasilimali na madeni kwa Viongozi wa Umma Disemba 28,2017.
Rais Wa Jamhuri Ya Muungano Wa Tanzania Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili Katika Ofisi Za Sekretarieti Ya Maadili Ya Viongozi Wa Umma Jijini Dar Es Salaam kuwasilisha fomu zake za tamko la Rasilimali na madeni kwa Viongozi wa Umma Disemba 28,2017.
Rais Wa Jamhuri Ya Muungano Wa Tanzania Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli akihakiki fomu zake kabla ya kuziwasilisha kwa Kamishina wa Maadili Jaji Mstaafu Haroild Nsekela Katika Ofisi Za Sekretarieti Ya Maadili Ya Viongozi Wa Umma Jijini Dar Es Salaam Disemba 28,2017.


  Rais Wa Jamhuri Ya Muungano Wa Tanzania Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli akimshukuru Kamishina wa Maadili Jaji Mstaafu Haroild Nsekela mara baada ya kuwasilisha fomu zake za tamko la Rasilimali na madeni kwa Viongozi wa Umma katika Ofisi Za Sekretarieti Ya Maadili Ya Viongozi Wa Umma Jijini Dar Es Salaam Disemba 28,2017.


Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
28 Desemba, 2017

Thursday 28 December 2017

TAIFA STARS YAPATA UZAMINI MNONO WA JEZI
Shirikisho  la Soka nchini (TFF), limeingia mkataba mnono na Kampuni ya Macron ambayo kuanzia sasa ndiyo mdhamini mkuu wa jezi za timu zote za Taifa; Taifa Stars, Twiga Stars na Serengeti Boys.

Aidha, udhamini huo wa miaka miwili wenye thamani ya Euro 700,000 zaidi ya Sh. bilioni 1.8 za Tanzania umegawanyika katika sehemu kuu mbili ambazo ni jezi na vifaa vingine vya michezo, pamoja na fedha taslimu.

Akizungumza wakati wa utiaji rasmi saini ya makubaliano hayo wakati wa mkutano wa TFF na Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini, Kaimu Katibu Mkuu wa shirikisho hilo, Wilfred Kidau, alisema hiii ni mara ya kwanza kwa timu za Taifa kupata mkataba mnono kama huo.

"Kwa mwaka tutakuwa tukipata euro 150,000 ambapo kwa miaka miwili ni euro 300,000 (takriban Sh. milioni 800) hizo zikiwa ni mbali ya kupewa jezi na vifaa vingine, hii ni mara ya kwanza kwa timu zetu za taifa kupata udhamini wa jezi mkubwa kama huu," alisema Kidau.

Kwa upande wa Rais wa TFF, alisema bado wanaendelea kutafuta wadhamini kwa timu hiyo na ile ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars ambayo haihusiki katika udhamini huo wa Macron.

"Mchakato huu umechukua muda mrefu na walikuwapo washindani wengi, lakini Kampuni ya Macron ndiyo imeshinda, na hatuishii hapo tu bado tunahitaji wadhamini wengine watakaoidhamini pia Kilimanjaro Stars.

"Kuna mengi tutakayofaidika katika mkataba huu, kwani pia tutakuwa tukipata sehemu ya mauzo ya jezi za timu ya Taifa na pia sasa itakuwa ni vigumu kutengenezwa na kuuzwa kiholela," alisema Karia.

Aliongeza kwa kufafanua kuwa awali ilikuwa vigumu kudhibiti watengenezaji na wauzaji holela kwa kuwa hata nembo ya TFF ilikuwa haijasajiliwa jambo ambalo kwa sasa limefanyika kabla ya kukamilisha mchakato huo wa udhamini.

Karia alisema faida ya uuzwaji wa jezi hiyo itaonekana kwa sasa kwa kuwa anaamini kutokana na Rais John Magufuli, kudhibiti uingizwaji uholela wa bidhaa nchini kwa kuimarisha ulinzi mipakani na bandarini, itakuwa ni vigumu kwa wale waliokuwa wakitumia ujanja huo kujinufaisha.
Mkurugenzi Mtendaji CRDB Atangaza Kung'atuka
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk Charles Kimei amesema hatoongeza muda wa kuiongoza taasisi hiyo baada ya mkataba wake kukamilika Mei, 2019.

Mkurugenzi huyo atakayekuwa ameiongoza CRDB kwa miaka 21 atakapostaafu, amesema uamuzi huo anaufanya kupisha damu mpya kuendeleza mafanikio ya benki hiyo kubwa nchini.

“Si vizuri kung’ang’ania madaraka. Tunao wakurugenzi tuliowaandaa kwa muda mrefu ambao wanaweza kuendeleza nitakapoishia. Ninapisha damu changa nami nitaendelea kuwa mwanahisa wa kawaida,” amesema Dk Kimei leo Alhamisi Desemba 28,2017.

Kwa utaratibu wa benki hiyo, mchakato wa kumpata mkurugenzi mtendaji huchukua miezi 18 lakini Dk Kimei ameongeza mwezi mmoja na kuifanya 19 ili kuipa bodi ya wakurugenzi nafasi zaidi ya kukamilisha hatua hizo.

Amesema ingawa upo mfumo mzuri wa kurithishana madaraka ndani ya benki hiyo, lakini mwenyekiti na bodi wana uhuru wa kumchagua mtu mwenye sifa za ziada kutoka nje na kushirikiana na familia ya benki kuendeleza mafanikio.

“Katiba yetu inataka Mtanzania ndiye aiongoze CRDB. Ninaiamini timu niliyoshirikiana nayo tangu niingie hapa. Hata benki nyingine zinazotafuta wakurugenzi watendaji, ningezishauri zije CRDB,” amesema.

Ndani ya muda uliobaki kabla mkurugenzi mpya hajakaribishwa, Dk Kimei amesema angependa kuona inapata faida kama ya mwaka 2015 ilipotengeneza Sh187 bilioni ikiongezeka kutoka Sh148 mwaka 2014.
Mtumishi wa PPF Atiwa mbaroni kwa tuhuma za kusafirisha mirungi
Bab
Polisi mkoani Kilimanjaro inamshikilia mfanyakazi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (PPF) kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah alimtaja mtuhumiwa huyo kuwa ni Anitha Oswald (32).

“Askari wakiwa doria walimkamata Anitha Oswald, ambaye ni mkazi wa Karanga, Manispaa ya Moshi, akiwa anasafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi kilo 216 na gramu 370 kwa kutumia gari lake analomiliki aina ya Toyota Sienta rangi ya silva,” alisema kamanda Issah.

Kamanda Issah alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa eneo la Majengo kwa Mtei Desemba 19 akitokea Njia Panda ya Himo kuchukua mzigo huo.

“Jeshi la polisi mkoani hapa liko makini, operesheni inaendelea na hatutamvumilia mtu yeyote ambaye atabainika kujihusisha na biashara hii”, alisema.

Kamanda huyo alisema polisi wanaendelea kumtafuta dereva wa gari hilo ambaye alikimbia baada ya kulitelekeza lilipogonga mti wakati akiwakimbia askari.
Waziri wa Elimu amkatalia Mbunge kusajili Shule.
Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako amekataa kutoa usajili kwa Shule ya Msingi Njalu iliyopo wilayani Itilima, Mkoa wa Simiyu kutokana na kutokidhi vigezo.

Shule hiyo imejengwa na wananchi kwa kushirikiana na mbunge wa Itilima (CCM), Njalu Silanga.

Akizungumza katika mkutano uliofanyika jana katika shule hiyo iliyopewa jina la Njalu kutokana na mchango wa mbunge huyo katika ujenzi, Profesa Ndalichako alisema shule hiyo haijakidhi vigezo vya usajili.

Mbele ya wakazi wa Kijiji cha Habiya ilipo shule hiyo, waziri Ndalichako alikataa ombi la mbunge huyo kuisajili na kuagiza upungufu uliopo urekebishwe kwanza kabla ya wizara kuisajili shule hiyo ya umma.

Miongoni mwa upungufu huo ni kuwa na vyumba vitano pekee vya madarasa badala ya vinane vinavyohitajika.

Mengine ni matundu ya vyoo, ambayo kati ya 10 yanayohitajika, yapo matano pekee, huku ikiwa na chumba kimoja cha ofisi ya walimu.

Profesa Ndalichako alisema wizara itatoa mifuko 100 ya saruji kusaidia kuondoa upungufu uliopo.

“Tumeona kuna upungufu hatutaweza kutoa kibali cha kuisajili, badala yake mkamilishe yanayohitajika kwa utaratibu wa kisheria wa kufungua shule. Niwahakikishie kuwa, Wizara ya Elimu hatuna urasimu ni lazima tuwe makini kwa kusimamia vigezo hivyo,” alisema Profesa Ndalichako.

Alisema licha ya kuwapo kwa mahitaji ya shule katika eneo hilo ambalo lina wanafunzi wapatao 633, ni lazima kuzingatia vigezo ambavyo vitakaguliwa na wataalamu kutoka idara ya udhibiti ubora wa elimu na ofisi ya ofisa elimu wilaya.

Awali, Silanga alielekeza lawama kwa watumishi wa Serikali na hasa wa idara ya elimu mkoani Simiyu kwa kushindwa kutumia utaalamu wao kuwaelimisha wananchi kuhusu vigezo vinavyotakiwa kabla ya shule kusajiliwa.

“Timu ya wataalamu ishuke itoe maelekezo. Majengo mengi yanavunjwa, wasimamizi tunao lakini hawatekelezi majukumu yao hivyo watimize wajibu wao kuliko kuwakatisha tamaa wananchi katika kuchangia shughuli za maendeleo,” alisema.

Silanga alimwomba Waziri Ndalichako kuwapatia usajili wakati wakiendelea kushughulikia upungufu uliojitokeza kwa kipindi cha muda mfupi kabla ya shule kufunguliwa Januari 8 mwakani ombi ambalo hata hivyo, lilikataliwa.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka alisema hawawezi kuwaadhibu wananchi na mbunge, hivyo ni lazima wahakikishe upungufu uliopo unaondolewa kabla ya Januari 15 mwakani.

Katika kuunga mkono jitihada hizo, Mtaka alitoa mifuko 50 ya saruji; huku mkuu wa Wilaya ya Itilima, Benson Chilangi pia akitoa mifuko 50.

Halmashauri ya Wilaya ya Itilima imeahidi kutoa mabati na mbao zitakazohitajika katika ujenzi.
Wafanyakazi TTCL wajitosa Sakata la AIRTEL
Chama cha Wafanyakazi wa Sekta ya Huduma za Mtandao wa Mawasiliano Tanzania (Tewuta) kimepongeza hatua ya Rais John Magufuli kumtaka Waziri wa Fedha kuanza uchunguzi kubaini ukweli kuhusu ubinafsishwaji wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL).

Katibu Mkuu wa Tewuta, Junus Ndaro amesema chama hicho kinatambua fika kuwepo mchezo mchafu uliosababishwa na Watanzania wachache wenye uchu wa fedha wakisaidiana na wawekezaji kupora rasilimali hiyo ya Taifa.

Ndaro amesema leo Alhamisi Desemba 28,2017 kuwa, kwa muda mrefu chama hicho kimekuwa kikitoa malalamiko kuhusu ufisadi huo serikalini lakini hakikusikilizwa.

“Tunampongeza Rais Magufuli kwa kuthubutu kutamka pasipo shaka kuwa taarifa alizonazo zinaonyesha kampuni ya Airtel ni mali ya TTCL, jambo hili tulilipigia kelele kwa muda mrefu,” amesema.

Ndaro amesema mara zote hawakusita kutamka kuwa Celtel ambayo sasa ni Airtel ni mali ya TTCL iliyoporwa pasipo kulipwa chochote.

“Wafanyakazi tunatambua kuwa TTCL haikuporwa Celtel pekee bali ilinyang’anywa pia Chuo cha Posta na Simu hali iliyosababisha tukose mahali pa kupata mafunzo,” amesema Ndaro.

Kutokana na kuanza uchunguzi wa sakata hilo, Ndaro amesema viongozi wa Tewuta wako tayari kutoa kila aina ya ushirikiano kuhakikisha Serikali inashinda na kuirudisha Airtel mikononi mwa TTCL.

“Tuna ushahidi wa kutosha na tuko tayari kutoa ushirikiano kwa Serikali katika hatua zote kuleta haki iliyopotea ya Kampuni ya Simu Tanzania,” amesema.
Rais Magufuli Aipa Meno Kamati ya Kuhakiki Mali za CCM.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 28 Desemba, 2017 amekutana kwa mara ya kwanza na kamati maalum aliyoiunda kwa lengo la kuhakiki mali za chama hicho, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Kamati hiyo aliitangazwa tarehe 20 Desemba, 2017 Mkoani Dodoma na inaongozwa na Dkt. Bashir Ally.

Katika Mazungumzo hayo Mhe. Rais Magufuli amewataka wajumbe wa kamati hiyo kufuatilia na kuhakiki mali zote za chama, kumhoji mtu yeyote ambaye atahitajika kutoa taarifa juu mali za chama na kubaini thamani ya mali, mahali zilipo, makusanyo ya mapato na wanaozishikilia ama kutumia mali hizo.

Mhe. Rais Magufuli pia ametoa wito kwa wanachama wa CCM na wananchi wengine kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa zote zinazohusu mali za chama kwa kamati hiyo, na watakaoitwa kuhojiwa waitikie wito huo.

“Nataka mali za chama zikinufaishe chama, nataka mkamhoji mtu yeyote, awe kiongozi, awe mwanachama, awe mfanyabiashara, mtu yeyote. Mkazihakiki mali zote ili chama kipate haki yake” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Akizungumza kwa niaba ya kamati hiyo, Dkt. Bashiru Ally amesema kamati imeanza kazi rasmi na ametoa wito kwa wanachama, wananchi na wote wanaozitumia mali za chama kutoa ushirikiano watakapoitwa kuhojiwa.

“Tumezungumza na Mwenyekiti kwa karibu saa mbili, katueleza matarajio yake, sababu za kuunda tume hii, kazi zake na faida zake kwa chama na kwa nchi, kwa hiyo ametukabidhi vitendea kazi na taarifa mbalimbali na ametueleza kazi yetu ni kuhakiki mali zote za chama kwa kushirikiana na wanachama na wale wanaoshirikiana na chama kuzitumia hizo mali kama vile wapangaji, wasimamizi, nakadhalika” amesema Dkt. Bashiru Ally.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
28 Desemba, 2017