Monday, 9 April 2018

TUCTA Nao Wataka Watumishi Darasa la 7 Warudishwe Kazini
Baraza Kuu la Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) jana Jumamosi Aprili 7, 2018 limetoa tamko lenye mambo saba, likiwemo la kupinga uamuzi wa Serikali kuwafuta kazi watumishi wake wenye elimu ya darasa la saba.

Akisoma tamko hilo mbele ya wajumbe wa baraza kuu la Tucta katika mkutano wa baraza hilo uliofanyika mkoani Morogoro mwenyekiti wa Tucta, Tumaini Nyamhokya alisema uamuzi huo wa Serikali si sahihi na hivyo wametaka watumishi hao kurejeshwa kazini.

Alisema baraza limesikitishwa na uamuzi wa kuwaondoa kazini watumishi wa umma na taasisi zinazopokea ruzuku kutoka serikalini.

Nyamhokya alisema uamuzi huo si wa kisheria ikizingatiwa kuwa watumishi hao waliajiriwa kwa kufuata taratibu halali za ajira.

“Kwa hiyo Tucta tunaitaka serikali kutengua uamuzi wake na kuwarudisha watumishi hao kazini bila kupoteza haki zao za kiutumishi kwa kipindi chote,” alisema.

Mambo mengine sita yaliyopo katika tamko hilo wanayotaka yafanyiwe kazi ni; ongezeko la mishahara, kodi ya mishahara (PAYE), kupandishwa madaraja na vyeo kwa watumishi wa umma, malimbikizo ya mishahara kwa wafanyakazi na watumishi kwa baadhi ya taasisi, ucheleweshwaji wa malipo ya wastaafu kwa baadhi ya mifuko ya hifadhi ya jamii na uamuzi wa Serikali kuunganisha mifuko ya hifadhi ya jamii.
Waziri Mkuu Awataka Mabalozi Kutangaza Vivutio Vya Uwekezaji Vilivyopo Nchini
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nchini Urusi na Rwanda kutumia fursa hiyo kwa kutangaza vivutio vilivyopo nchini ili kuwavutia wawekezaji kuja kuwekeza kwenye sekta mbalimbali ikiwemo ya utalii.

Pia amewataka Mabalozi kila mwisho wa mwaka wajifanyie tathmini ya mafanikio waliyoyapata kutokana na uwakilishi wao katika Mataifa ambayo  ni kwa kiasi gani wamechangia kwenye uboreshaji wa maendeleo ya Taifa.

Ametoa maagizo hayo leo (Jumapili, Aprili 8, 2018) wakati akizungumza na Balozi Ernest Mangu anayewakilisha Tanzania nchini Rwanda na Balozi Simon Mumwi anayewakilisha Tazania nchini Urusi, katika ofisi ya Waziri Mkuu mjini Dodoma.

Waziri Mkuu amesema Tanzania ina vivutio vingi vya utalii ikiwa ni pamoja na uwepo wa mbunga za wanyama, hivyo ni vyema wanapoondoka wachukue nyaraka zote zitakazowasaidia katika kutangaza vivutio vya utalii ili kuongeza idadi ya watalii nchini.

Amesema mbali na kutangaza sekta ya utalii, pia watafute wawekezaji kwa ajili ya kuwekeza kwenye sekta nyingine kama vile madini, viwanda na kutafuta masoko ili wafanyabiashara na wakulima wa Tanzania waweze kuuza bidhaa zao nje ya nchi.

“Pia mkajifunze mbinu ambazo wenzetu wanazitumia katika kuboresha sekta mbalimbali ambazo na sisi tunazo hapa nchini kama za viwanda na kisha mje mtueleze namna ya kuziboresha. Kujifunza ni jambo zuri hivyo msisite kufanya hivyo huko muendako.”

Pia Waziri Mkuu amewataka mabalozi hao wakawatambue na kuwaunganisha Watanzania waishio kwenye nchi wanazoiwakilisha ili nao washiriki kwenye ujenzi wa uchumi wa viwanda na wawasisitize wafuate sheria za nchi wanazoishi na wakumbuke nyumbani.

Waziri Mkuu amewasisitiza mabalozi hao kwenda kupunguza gharama za uendeshaji wa Balozi kwa kuzuia matumizi katika mambo yasiyo ya lazima. “Pia maslahi ya nchi lazima mkayasimamie huko muendako hasa katika masuala ya kiuchumi.

Kwa upande wao mabalozi hao  wamesema watahakikisha wanayafanyia kazi maelekezo yote waliyopewa ikiwa ni pamoja na kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na nchi wanazoziwakilisha.

 (mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,

Monday, 26 March 2018

Watu 17 Watambuliwa Kati Ya 26 Waliofariki Katika Ajali Mkuranga
WATU 17 kati ya 26 waliofariki dunia katika ajali ya barabarani iliyotokea Mkuranga Mkoani Pwani ,wametambuliwa majina yao ambapo hatua inayoendelea ni kuwakabidhi kwa ndugu zao kwa ajili ya mazishi.

Aidha watu wengine kumi wamejeruhiwa na wamekimbizwa hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu.

Ajali hiyo imehusisha  gari  ndogo ya abiria aina ya Toyota Hiace yenye namba za usajili T.676 DGK inayofanya safari zake Kimanzichana – Mbagala Rangi na gari nyingine aina ya Lori.

Mganga mkuu wa hospitali ya wilaya ya Mkuranga, Stephen Mwandambo alisema amepokea maiti 25 na majeruhi hao ambapo majeruhi mmoja alifariki njiani wakati wakipelekwa hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Mganga mkuu huyo aliwataja waliofariki na kutambuliwa majina yao ni 17 kati ya 26 waliofariki kuwa ni pamoja na  Selemani Guli (36) mkazi wa Kongowe,Modesta Sheleli (24 ) mkazi wa Vianzi,Doreen Selemani Seleli (5), sheila Hamad Mkuba ( 8 )mkazi wa Vianzi na Mariam Hussein Sadik (15 )mkazi wa Mwarusembe.

“Nassoro Hamis( 48) mkazi wa Jaribu Mpaka, Asha Athumani (24)mkazi wa Songosongo ,Nasma Athuman 22 Songosongo Mwanahawa Athuman (52),Mohammed Saidi (25) mkazi wa Njopeka na Mwajabu Jongo (20)mkazi wa Njopeka”;

Dokta Mwandambo aliwataja wengine ni Mwarami Mbunju(37) mkazi wa Mkamba na Abisaalom Uloga (25)mkazi wa Kimanzichana ,Kijongo Kibwana Jongo(26 )anakaa Jaribu Mpakani na Recho Japhet (16),Mariam Selemani (36)mkazi wa Mbagala  na Melania Kapatwa (38)mkazi wa Jaribu Mpakani.

Inasemekana majeruhi waliopelekwa katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili wengine wamekatika viongo mbalimbali vya mwili.

Aidha dokta Mwandambo alisema wanakabiliwa na changamoto ya kipimo cha X-ray hali inayosababisha kushindwa kuwafanyia uchunguzi majeruhi .

Changamoto nyingine inayowakabili ni chumba cha kuhifadhia maiti kuwa kidogo kwani kina uwezo wa kuhifadhi maiti sita hivyo maiti 26 zipo nje ya uwezo wao.

Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia machi 25 mwaka huu katika eneo la Kitonga kata ya Mwalusembe wilaya ya humo.
Chanzo cha ajali inadaiwa mwendo kasi wa dereva wa lori katika kilima na kusababisha ajali hiyo mbaya.

Simanzi zimetawala katika wilaya hiyo ,ambapo mbunge wa jimbo la Mkuranga, Abdallah Ulega ,aliishukuru serikali ya wilaya chini ya mkuu wa wilaya ya Mkuranga Filberto Sanga kwa juhudi zake za kusaidia majeruhi na marehemu kupelekwa hospitalini .

Ulega alitoa pole kwa wafiwa na majeruhi na kuwaasa madereva waache kuendesha kwa mwendo kasi kwani husababisha ajali zembe.

“Naishukuru pia hospitali ya wilaya kwa juhudi zao baada ya kupokea marehemu na majeruhi kuhangaikia kuokoa maisha yao.” alieleza Ulega.

Thursday, 22 March 2018

Waziri Ummy Awashauri Wananchi Kwenda Vituo Vya Tiba Haraka Pindi Wanapogundua Dalili Za Ugonjwa Wa Dengue




WAZIRI wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amewashauri wananchi kwenda vituo vya tiba haraka mara baada ya kugundua kuwa wana dalili za ugonjwa wa dengue.

Hayo ameyasema wakati alipotoa tamko juu ya kuingia kwa ugonjwa wa dengue hapa nchini mara baada ya kufunga Mkutano wa 65 wa Jumuiya ya Mawaziri wa Afya wa Nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini ECSA jana  jijini Dar es salaam.

“Kuna dalili za Ugonjwa Dengue zikiwemo homa ya ghafla, kuumwa kichwa hususan sehemu za macho, maumivu ya viungo na uchovu. Dalili hizi huanza kujitokeza kati ya siku 3 hadi 14 tangu mtu alipoambukizwa virusi vya homa ya Dengue hivyo Wizara inashauri kuwa wananchi wasiwe na hofu, bali mara tu wanapoona dalili za ugonjwa waende katika vituo vya tiba " alisema Waziri Ummy.

Aidha Waziri Ummy amesema kuwa Wakati mwingine dalili za ugonjwa huu zinaweza kufanana sana na dalili za malaria hivyo basi wananchi wanaaswa kuwa, wakipata homa wahakikishe kuwa wanapima ili kugundua kama wana vimelea vya malaria au Dengue, au sababu nyingine, ili hatua stahiki zichukuliwe.

Waziri Ummy amesema kuwa ili kujikinga na ugonjwa huo ni lazima Kuangamiza mazalio ya mbu kwa kufukia madimbwi ya maji yaliyotuama au nyunyuzia dawa ya kuua viluwiluwi vya mbu kwenye madimbwi hayo pamoja na Kujikinga na kuumwa na mbu kwa  kuvaa nguo ndefu muda wote hasa nyakati za mchana.

Aidha Waziri Ummy amesema kuwa Wizara itaendelea Kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa nchi nzima kwa kutumia mfumo uliopo wa ukusanyaji wa taarifa (IDSR), ambapo tunaendelea kupata taarifa za kila siku juu ya mwenendo wa ugonjwa huu na Kutoa elimu kwa jamii kupitia vyombo vya habari.

Mbali na hayo Waziri Ummy amesisitiza kuwa  hakuna vikwazo vyovyote vilivyowekwa kwa ajili ya wasafiri wanaoingia na wanaotoka nchini na  Wizara itaendelea kushirikiana na wadau na sekta mbalimbali katika kufuatilia na kudhibiti ugonjwa huo.

Homa ya Dengue ni ugonjwa unaosababishwa na virusi vinavyoenezwa na mbu wa aina ya Aedes ambao ni weusi wenye madoa madoa meupe yenye kung’aa.

Wednesday, 21 March 2018

Amuua Mkewe na Kuificha Maiti Kwenye Mbuyu kwa Miaka 8


Mwanaume  mmoja aliyejulikana kwa jina Bernard Shumba mkazi wa Singida anashikiliwa na jeshi la polisi mkoani humo kwa kumuua mke wake miaka minane iliyopita kisha kuuficha mwili wa marehemu kwenye mbuyu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Deborah Magiligimba, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema mtuhumiwa baada ya kukamatwa alikiri kutenda kosa hilo na kwenda kuonyesha mwili wa marehemu aliokuwa ameuhifadhi ndani ya mbuyu ambapo jeshi hilo kushirikiana na wananchi limefanikiwa kupata mabaki yake.

Inadaiwa kuwa mnamo Julai 10, 2010 katika Kijiji cha Yulansoni Kata na Tarafa ya Kinyangiri Wilaya ya Mkalama mkoani Singida, Tabu Robert (28) ambaye kwa kabila ni Mnyiramba, mkulima wa Yulansoni, aliuawa na mume wake aitwae Bernard Shumba Siza (47), Mnyiramba na mkulima wa Yulansoni.

Baada ya Mmuhumiwa kufanya tukio hilo aliuchukua mwili wa marehemu na kwenda kuuficha kwenye mti wa mbuyu ambao una tundu kubwa na kisha aliripoti polisi kituo kidogo cha Kinampanda Mkalama kuwa mke wake ametoroka na alianza kumtafuta hadi tarehe Machi 17, 2018 ambapo taarifa zilipopatikana kuwa alimuua.

Baada ya mtuhumiwa kukamatwa na kuhojiwa alikiri kufanya kitendo hicho na kuonyesha sehemu alipouficha mwili huo Machi 18, mwaka huu majira ya saa 10:00 jioni.

Mkuu wa polisi kituo cha  Mkalama na timu yake ya makachero walifika eneo la tukio na kufanikiwa kupata mabaki ya mifupa yakiwa ndani ya mti huo. Baadhi ya mifupa imechukuliwa kwa ajili ya kupelekwa kwa mkemia wa serikali na iliyobakia ndugu wamekabidhiwa kwa ajili ya mazishi.




Serikali yatoa neno kushambuliwa afisa wa Syria

Baada ya kuwepo kwa taarifa kupitia mitandao ya kijamii kuhusu kushambuliwa kwa afisa wa ubalozi wa Syria nchini Tanzania na watu watatu wasiojulikana na kupigwa ikiwa pamoja na kuporwa pesa, simu na gari aliyokuwa akiitumia kwa shughuli za ubalozi.

Kufuatia taarifa hizo Msemaji Mkuu wa Serikali Dk. Hassan Abasi amefunguka na kukiri kupata taarifa hizo na kudai kuwa serikali inafuatilia suala hilo na itatoa taarifa kamili kuhusu jambo hilo.

"Umma unaarifiwa kuwa vyombo vya dola vinafuatilia taarifa za Afisa Ubalozi wa Syria nchini kushambuliwa, kuporwa. Taarifa kamili itatolewa" alisema Abasi

Aidha katika taarifa za awali zinadai kuwa afisa huyo amelazwa katika hospitali ya Agha Khan akipatiwa matibabu kufuatia shambulio hilo