Wednesday, 3 January 2018

Ubovu Magari Mapya Ya Polisi Waishitua Wizara Mambo Ya Ndani

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imebaini madudu katika utekelezaji wa mkataba wa uagizaji wa magari 777 kwa ajili ya Jeshi la Polisi yaliyoagizwa kwa gharama za dola za Marekani milioni 29.77 (Sh. bilioni 66.288).

Kutokana na hali hiyo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, amemwagiza katibu Mkuu wa wizara hiyo, Meja Jenerali Projest Rwegasira, kuunda kamati maalum ya kuchunguza mkataba wa uagizaji wa magari hayo.

Vilevile, ameagiza kamati hiyo ambayo itahusisha wataalamu kutoka taasisi mbalimbali, kupitia upya mkataba ulioingiwa mwaka 2013 kati ya serikali na Kampuni ya Ashok Leyland inayoingiza magari hayo nchini.

Masauni aliyabainisha hayo jijini Dar es Salaam jana, muda mfupi baada ya kufanya ziara ya kukagua magari 53 ya jeshi hilo yaliyotolewa bandarini kwa agizo la Rais John Magufuli alilolitoa Novemba 26, mwaka jana, huku naibu waziri huyo akibaini matano yana hitilafu.

Rais Magufuli alifanya ziara bandarini siku hiyo na kukuta magari hayo 53 ya Jeshi la Polisi na magari mengine 50 ya kubebea wagonjwa yakiwa yamekaa hapo tangu Juni, 2016 bila kutoka na kuagiza kutolewa mara moja.

Jana, Masauni alikuta magari hayo yameshatolewa na kuwekwa katika Chuo cha Polisi Kurasini huku Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa) wakiyafanyia ukaguzi kabla ya kuyakabidhi kwa Jeshi la Polisi kwa ajili ya ukaguzi zaidi.

Masauni pia alitembelea bandarini na kubaini kuwa magari mengine 119 ya Jeshi la Polisi yameshawasili huku malori yakiwa ni mengi kuliko idadi ya magari madogo ambayo yanahitajika zaidi kwa shughuli za jeshi hilo.

“Tumeamua kuunda hii kamati itueleze kitaalamu kwanini magari haya yanakuja malori zaidi ilhali tuna uhitaji mkubwa wa magari madogo katika vituo vyetu vya polisi nchini na je, mkataba ulielezaje na kama unafuatwa,” alisema Masauni.

Kuhusu hitilafu zilizobainika kwenye baadhi ya magari, Masauni alisema kamati hiyo ichunguze sababu za magari hayo kuharibika ilhali waliagiza magari mapya na siyo yaliyotumika.

Naibu Waziri huyo pia alibainisha kuwa ukaguzi wa awali umebaini moja ya magari kusomeka limeshatembea zaidi ya kilometa 1,000 na kwamba suala hilo pia, litapatiwa ufumbuzi kwa kuwa serikali iliagiza magari mapya na si yaliyotumika.

Masauni alisema kamati itakayoundwa itahusisha pia wataalamu kutoka Chuo cha Usafirishaji (NIT) na Temesa, ili kuchunguza kwa kina magari hayo.

Jeshi la Polisi limekuwa likikumbwa na changamoto za kuwa na utekelezaji wenye utata wa baadhi ya mikataba yake iliyowahi kuingiwa siku za nyuma, huku ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2014/15 ikibainisha kuwa jeshi hilo na Shirika la Umeme (Tanesco) ni miongoni mwa taasisi zinazoongoza kwa madeni na manunuzi makubwa.

0 comments: