Watumishi
12 kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) jana walitumia zaidi ya saa
sita kumhoji Askofu Mkuuwa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship
(FGBF), Zachary Kakobe.
Mwandishi
wetu ambaye alipiga kambi nje ya kanisa hilo lililopo Mwenge, Dar es
Salaam kuanzia saa tano asubuhi, alishuhudia kuwasili kwa watumishi
ambao mara baada ya kushuka katika magari na kutaka kuingia ndani,
walizuiwa na wahudumu wa kanisa hilo kwa takribani dakika 15.
Baada
ya kuingia ndani, watumishi hao walitoka saa 11:48 jioni kwa staili ya
aina yake. Tofauti na walivyowasili kwa magari saba, wakati wa kuondoka
walijibana katika magari mawili yaliyoingia ndani ya kanisa hilo
kuwachukua, huku mengine yakiondoka tupu.
Tukio
la idadi kubwa ya watumishi kuonekana katika kanisa hilo imekuja zikiwa
zimepita siku tano tangu Kamishna wa TRA, Charles Kichere kueleza nia
ya mamlaka hiyo kuanza mchakato wa kufuatilia ulipaji kodi wa Askofu
Kakobe.
Kichere alisema uamuzi huo unatokana na kiongozi huyo wa kiroho kutokuwamo katika kumbukumbu za ulipaji kodi za mamlaka hiyo.
Alitoa
kauli hiyo baada ya kusambaa kwa picha za video zikimuonyesha Askofu
Kakobe akiwa katika mahubiri kwenye kanisa hilo, akisema kiwango cha
fedha alichonacho si tu ni zaidi ya kile cha Serikali, bali pia anaweza
kuwakopesha fedha hata mawaziri.
Kiongozi
huyo wa kiroho alirejea kauli yake hiyo katika ibada ya Jumapili
iliyopita, safari hii akibainisha kuwa ana fedha nyingi kuliko Serikali
zote duniani na kuwataka watu wakimsikia anazungumza, watafakari kwanza
kabla ya kumkabili.
Mwandishi
alipotaka kupata ufafanuzi kwa Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa
Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo kama watumishi hao waliokuwa kwa
Askofu Kakobe ni wa mamlaka hiyo, alishindwa kukubali au kukataa.
Alisema ingawa mamlaka hiyo iliahidi kwenda kumhoji hana uhakika kama hao walikuwa maofisa wa TRA au la.
Hata
hivyo, mtendakazi wa kanisa hilo, Natus Mwita alipoulizwa kuhusu ujio
wa maofisa hao alisema walipokea barua ya TRA tangu Desemba 30, mwaka
jana.
“Walileta
barua yao kutaka kuonana na Askofu Desemba 30, sasa hatujajua labda leo
wamekuja kuchukua mujibu yao, kwa sasa hamuwezi kuingia ndani labda
msubiri nje ndiyo mtaweza kuonana nao watakapokuwa wakitoka,” alisema
Mwita.
Jitihada
za mwandishi wetu kuzungumza na watumishi hao ziligonga mwamba kutokana
na kutotoka nje baada ya kumaliza mahojiano hayo kwani waliingia ndani
ya magari hayo wakiwa ndani ya kanisa na kutoka katika mwendo wa kasi.
Wakati
wakiwa ndani ya kanisa hilo, magari yenye namba za STK na STL yalikuwa
yakipita mara kwa mara nje ya kanisa hilo lililopo kando ya Barabara ya
Sam Nujoma.
Katikati
ya mazungumzo hayo, Askofu Kakobe alitoka kwenye chumba cha mahojiano
na kuelekea jengo jingine kanisani hapo. Baada ya kutoka baadhi ya
watumishi hao wa TRA nao walitoka kwenye chumba hicho na kuonekana
wakizungumza nje. Walirejea ndani baada ya askofu huyo kurudi.
Wakati wote wa mahojiano hayo, shughuli mbalimbali za kanisa zilikuwa zikiendelea huku waumini wakionekana kuingia na kutoka.
Mmoja
wa waumini hao, Janet Mathew alisema, “Nimekuja kwa ajili ya huduma ya
maombezi na maombi kwa kweli hakuna shida yotote nimepata huduma
vizuri.”
Alipoulizwa
kama aliona tofauti yoyote na siku nyingine alisema, “Sijui
kinachoendelea ni sawa na siku zote sijaona tofauti yoyote.”
Credit: Mwananchi
0 comments: