Friday 19 January 2018

Waziri Mkuu Asimamisha Uuzaji Wa Mali Za KNCU......Walitangaza Kuuza Shamba ili Benki Yao Isifungwe na Beki Kuu-BoT

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Bibi Anna Mghwira asitishe uuzwaji wa mali za Chama cha Ushirika cha Kilimanjaro (KNCU).

Ametoa agizo hilo jana jioni (Jumatano, Januari 17, 2018) wakati akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Serengeti, wilayani Tarime.

Hatua hiyo imekuja baada ya KNCU kutangaza kuuza shamba lake kwa ajili ya kuiwezesha benki yake ya KCBL  kutimiza sharti la mtaji la Benku Kuu ya Tanzania (BoT).

Benki hiyo ya KCBL inatakiwa kutimiza sharti la kuwa na mtaji kamili unaotosha wa shilingi bilioni  tano (5) katika kipindi cha miezi sita tangu kutolewa kwa tangazo hilo.

Waziri Mkuu alisema ni marufuku kuuza mali za Ushirika huo, hususan katika kipindi hiki ambacho Serikali inafanya uhakiki wa mali za vyama mbalimbali vya Ushirika nchini.

Alisema Serikali imedhamiria kuimarisha Ushirika nchini na sasa inafanya uhakiki wa mali za vyama vya Ushirika na watakaobainika kuhusika na ubadhilifu watachukuliwa hatua.

Januari 4, 2018 BoT ilizipa miezi sita benki tatu ili ziweze kuongeza kiwango cha mtaji unaohitajika kutokana na matakwa ya kisheria ya kuwa na mtaji kamili wa kutosha.

Benki hizo ni Kilimanjaro Co-Operative Bank Limited, Tanzania Women Banki Plc na Tandahimba Community Bank Limited, zitakaposhindwa kutekeleza agizo zitachukuliwa hatua.

BoT ni itazifutia leseni na kusimamisha shughuli za kibenki chini ya ufilisi, iwapo benki hizo zitashindwa kutekeleza agizo hilo ihadi kufikia Juni 30, 2018.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
Hatima ya waliofukuzwa kwa vyeti feki, Wenye Vyeti vya Darasa la 7 na Kuhhusu Kupandishwa Madaraja

HATIMA ya mafao ya wafanyakazi wa serikali walioondolewa kwenye ajira kutokana na kubainika kuwa na vyeti feki itajulikana kabla ya Bunge la Bajeti, imefahamika.

Hatua hiyo inatokana na serikali kujibu hoja nane za Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) na kwamba suala la kulipwa au kutolipwa haki zao litafahamika Machi au Aprili, mwaka huu.

Hoja zingine ni ajira ya waliomaliza darasa la saba, kupandishwa madaraja, madeni ya wafanyakazi, nyongeza za mishahara, kutofanyika vikao vya bodi, kujua idadi ya taasisi zilizoundwa na kuunganishwa kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

Katibu Mkuu wa Tucta, Dk. Yahya Msigwa, alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa mamlaka mbalimbali zinamalizia kulifanyia kazi suala la vyeti feki na kwamba kabla ya Mei Mosi, mwaka huu, hatima yao itakuwa imepatikana.

“Unajua kilichofanyika ni kosa la jinai na la kinidhamu, hivyo sisi Tucta tunaendelea kuiomba serikali angalau wapatiwe kifuta machozi,” alisema.

Alisema ajira kwa waliomaliza darasa la saba Serikali ilitoa waraka unaosema watumishi wa umma wanapaswa kumaliza elimu ya kidato cha nne kuanzia Mei, 20, 2004.

Pia alisema baada ya hapo, walitakiwa kujiendeleza ili kuwa na vigezo vya kuendelea kuwa watumishi wa umma iwapo zipo baadhi ya idara zinawahitaji na kujenga hoja.

Kuhusu kupandishwa madaraja,
Dk. Msigwa alisema watumishi wengi hawajapandishwa kutokana na uhakiki wa vyeti, hivyo serikali imetenga fedha kwa ajili ya mpango huo kwa kutegemea bajeti ijayo.

Alisema malipo yataanza tangu siku ya kupata barua ili kupunguza madeni ambayo inadaiwa na kwamba kimsingi katika hilo, yako madeni ya mishahara na isiyo ya mishahara.

Kuhusu madeni, kwa mujibu wa Dk. Msigwa, serikali imesema imemaliza uhakiki na imeanza kulipa lakini itakuwa vigumu kulipa watu wote kwa mkupuo bali watazingatia uhakiki ya madeni yenyewe.

Kwa upande wa nyongeza ya mishahara, alisema Rais John Magufuli hakuahidi wakati wa sherehe za Mei Mosi bali nyongeza hiyo italolewa mwaka huu.

Aidha, Dk. Msigwa alisema hoja ya kuunganishwa kwa mifuko ya hifadhi ya jamii kuwa na mifuko miwili, mmoja wa binafsi na mwingine wa umma, imetokana kauli za wafanyakazi wenyewe kwenye sherere za Mei Mosi.

Alisema rasimu iliyotegenezwa si mbaya licha upungufu uliopo na wanaendelea kutoa maoni kabla muswada haujawasilishwa Bungeni.
Simba Yaichapa Singida United 4G Mbele ya Kocha Mpya Mzungu.

Klabu ya Simba leo imeichapa klabu ya Singida United bao 4- 0 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania bara ambao umechezwa katika uwanja wa Taifa na kushuhudiwa na kocha Mkuu mpya wa Simba Mfaransa Pierre Lechantre.

Katika kipindi cha kwanza cha mchezo mshambuliaji mahiri Kichuya aliweza kuwaamsha mashabiki wa Simba ndani ya dakika ya tatu ya mchezo kwa goli la kwanza la kuongoza ambalo aliweza kulifunga kwa mtindo wa sarakasi na kumpoteza goli kipa wa Singida United Manyika Jr.

Mchezo uliendelea kuwa wa kasi na Simba kuonekana kutawala mchezo na kupelekea kuongeza furaha ya mashabiki wa klabu hiyo baada ya Beki wa Simba Asante Kwasi kuifunga goli la pili Singida United katika dakika ya 23 ya mchezo.

Mpaka wanakwenda mapumziko Simba tayari walikuwa wametangulia kwa goli 2-0 dhidi ya Singida United, katika kipindi cha pili cha mchezo Simba walionyesha uhai na nguvu zaidi ya mashambulizi na kupelekea mshambuliaji wa Kimataifa Emmanuel Okwi kuitandika goli ya tatu Singida United katika dakika ya 75.

Okwi aliongeza goli lake la pili katika mchezo huo katika dakika ya 82 ya mchezo na kupelekea klabu yake kuibuka na ushindi wa bao 4-0 dhidi ya Singida United

Thursday 18 January 2018

Dar Young African SC Yashikwa Shati na Mwadui.

Mabingwa watetezi wa ligi kuu soka Tanzania Bara klabu ya Yanga wamelazimishwa suluhu na Mwadui FC kwenye mchezo wa raundi ya 13 uliomalizika jioni hii uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam.

Yanga chini ya kocha Mzambia George Lwandamina kwa mara ya kwanza tangu arudi kutoka kwao, imeshindwa kupata ushindi hivyo kubaki katika nafasi ya tano. Mwadui FC yenyewe imefikisha alama 13 na kupanda hadi nafasi ya 9.

Hii ni mechi ya pili Yanga inashindwa kupata ushindi ambapo mechi ya raundi ya 12 Disemba 2017, ilikubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Mbao FC ya Mwanza.

Yanga imefikisha alama 22 hivyo kushindwa kuifikia Mtibwa Sugar yenye alama 23 katika nafasi ya nne baada ya wikiendi iliyopita kushinda mechi yake ya raundi ya 13 dhidi ya Lipuli FC.

Kesho kutakuwa na michezo miwili ambapo vinara wa ligi Simba SC watakuwa wenyeji wa Singida United wakati Azam FC inayoshika nafasi ya pili itakuwa ugeneini mjini Ruvuma kucheza na Majimaji FC.
Kiongozi wa CCM(UVCCM) Iringa Achomewa Nyumba.
Nyumba ya Katibu wa Umoja wa Vijana Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wa Mkoa wa Iringa, Alphonce Muyinga iliyopo maeneo ya Kihesa njiapanda ya Kwabeda imechomwa moto na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia leo.

Ambapo kikosi cha Zima Moto kilifanikiwa kufika katika nyumba hiyo na kujaribu kuzima moto huo ambao tayari ulikuwa umeshaleta athari ndani ya nyumba hiyo kwa mali mbalimbali zilizokuwepo ndani.

Pia aliyekuwa Diwani wa kata ya Mwangata, Iringa kwa tiketi ya Chadema na baadaye kujiuzulu nafasi yake hiyo, Anjelus Mbogo naye amefanyiwa uharibifu katika nyumba ambayo alikuwa akijenga baada ya watu wasiojulikana kuibomoa nyumba hiyo.

Anjelus amedai kuwa tukio hilo linawezekana kuwa limetokea kutokana na matamko ya uchochezi yaliyotolewa na Mbunge kwa wananchi.

“Kauli ya Mbunge ndiyo inaweza kuwa chanzo cha uchochezi kwa wananchi kuja kubomoa nyumba hizi kwa sababu yeye aliwaambia wananchi kama atajiuzulu wabomoe nyumba yake hata gari yake ichomwe moto nadhani wananchi wakachukua hilo kwani wananchi unapowashawishi ndivyo unavyomuaminisha kuja kufanya hivi huo ndiyo ukweli. Na mimi sisemi mambo mengi kwa kuwa jambo hilo bado linaendelea na upelelezi lakini naamini wameniaminisha kuwa hatabaki mtu” amesema Anjelus Mbogo

Aidha amesema hawezi kuongea mengi zaidi kwani swala hilo linafanyiwa upelelezi kubaini watu hao wasiojulikana.

Wednesday 17 January 2018

Watanzania washinda tuzo ya fasihi ya Kiswahili Afrika

Watanzania wawili wametangazwa washindi wa Tuzo ya Kiswahili ya Mabati-Cornell ya Fasihi ya Afrika kwa mwaka 2017.

Wawili hao watazawadiwa $5,000 kila mmoja katika sherehe ambayo itafanyika jijini Nairobi mwezi ujao.

Dotto Rangimoto alishinda kwenye kitengo cha ushairi kwa mswada wake Mwanangu Rudi Nyumbani naye Ali Hilal Ali akashinda kitengo cha riwaya kwa mswada wake wa Mmeza Fupa.

Waziri wa habari, utamaduni na Sanaa Tanzania Dkt Harrison Mwakyembe amewapongeza wawili hao kwa ushindi huo na kusema ushindi wao "unachagiza juhudi za serikali kuibidhaisha lugha ya Kiswahili."

"Ushindi wa Watanzania hawa ni ushindi wa taifa kwa ujumla," amesema Dkt Mwakyembe kupitia taarifa.

Tuzo hiyo ilianzishwa mwaka 2014 na Dkt Lizzy Attree (Mkurugenzi wa Tuzo ya Caine) na Dkt Mukoma wa Ngugi (Chuo Kikuu cha Cornell, Marekani), kwa lengo la kuthamini uandishi kwa lugha za Kiafrika.

Aidha, tuzo hiyo inakusudiwa kuhimiza sanaa ya tafsiri baina ya lugha za Kiafrika zenyewe kwa zenyewe, na pia kutafsiri maandishi ya lugha nyengine kwa lugha za Kiafrika.

Wengine waliokuwa wanashindania tuzo hiyo ni: Mbaruk Ally - Hali Halisi (ushairi); Hassan Omar Mambosasa - Nsungi (riwaya); Mwenda Mbatiah - Kibweta cha Almasi (riwaya) na Richard Atuti Nyabuya - Umalenga wa Nyanda za Juu (ushairi).
Majaji walikuwa Ken Walibora Waliaula (Mwenyekiti wa Majaji), mwanataaluma na mwandishi; Daulat Abdalla Said, mwanataaluma na mwandishi, anayesomesha Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar; na Ali Attas, mwandishi na mwalimu wa Kiswahili na Kiingereza, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje, Japan.

"Mashairi yaliyomo katika diwani hii yametumiliwa lugha iliyojaa taswira na majazanda yanayowakilisha vyema hisia zinazoelezwa katika dhamira mbalimbali," walisema majaji kuhusu diwani ya Mwanangu Rudi Nyumbani.

"Mshairi amefaulu sana kuzitumia mbinu na miundo kadha wa kadha ili kuyajadili maswala yanayohusu hali na mazingira tafauti tafauti katika maisha ya binadamu. Anayazungumza maswala mazito mazito, lakini kwa namna ambayo hayamuelemei msomaji wake."

Walimsifu pia Bw Ali Hilal na kusema: "Si mno mtu kukutana na riwaya ya Kiswahili ambayo mwandishi wake amejidhihirisha kuwa ni mbuji wa lugha fasaha na ya kisanii, inayotiririka kitabia kwa hiari yake, na bila ya kuonesha dalili zozote kwamba imelazimishwa."

"Licha ya kwamba matukio ya riwaya hii yanatokea katika kisiwa cha kubuni, maswala yanayojadiliwa humu ni miongoni mwa yale maswala sugu yanayoendelea kulisumbua bara la Afrika kisiasa, kijamii na kiuchumi."

Tuzo ya Kiswahili ya Mabati-Cornell ya Fasihi ya Kiafrika, yenye thamani ya jumla ya Dola za Marekani 15,000, hutolewa kila mwaka kwa miswada bora, au kwa vitabu vilivyochapishwa miaka miwili kabla ya mwaka wa kutolewa zawadi, katika fani za riwaya, ushairi, wasifu na riwaya za picha.

Miswada inayoshinda huchapishwa na shirika la uchapishaji vitabu la East African Educational Publishers (EAEP) na shirika la uchapishaji vitabu la Mkuki na Nyota Publishers

Na mswada bora wa ushairi hufasiriwa kwa Kiingereza na kuchapishwa kitabu na shirika la Africa Poetry Book Fund.

Tuzo hii inadhaminiwa na kampuni ya Mabati Rolling Mills, Kenya, na kampuni ya ALAF Limited, Tanzania na pia Ofisi ya Makamu wa Mkuu wa Masuala ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Cornell, na Idara ya Taaluma za Afrika ya Chuo Kikuu cha Cornell, Marekani.
Polisi Tanzania yakana taarifa upigaji marufuku vimini


Polisi nchini Tanzania, imekanusha taarifa zilizoenea kwamba imepiga marufuku uvaaji wa nguo fupi au 'miniskirt' na vile vile nguo zinazobana. Kamanda wa polisi Mkoa wa Dar es Salaam Lazaro Mambosasa amesema taarifa hizo ambazo zimeandikwa katika moja ya magazeti nchini sio za kweli, na "zimetengenezwa" na "kuchongwa" kwa lengo la kutafuta umaarufu.

Kutokana na taarifa hizo zilizozagaa katika mitandao ya kijamii, mjadala mkali uliibuka katika mitandao ya kijamii huku baadhi wakihoji, ni kipengele gani cha sheria kitakachotumiwa kukamata watu watakao kuwa wamevaa nguo fupi.

Hata hivyo, ikumbukwe kwamba, nchini Tanzania, kuna utaratibu wa mavazi maalumu hasa katika majengo ya ofisi za serikali, ambapo wafanyakazi na wageni wanatakiwa kufuata muongozi huo.
Kwa mujibu wa menejimenti ya utumishi wa umma, wanawake na wanaume wafanyakazi wa umma hawaruhusiwi kuvaa kaptula kazini.

Picha ya muongozo wa mavazi zinabandikwa katika sehemu za kuingilia majengo ya umma, ili kuelekeza wasimamizi na wageni utaratibu wa sehemu hio. Wengi watakaokosa kufuata uratatibu mara nyingi hurudishwa au huelekezwa kutafuta vazi la kujistiri, kama vile khanga kwa wanawake.
Japo nguo hizi zinaweza kutafsiriwa kama mojawapo za nguo za kitamaduni, haziruhusiwi katika majengo ya umma Tanzania.

Wafanyakazi hawaruhusiwi kuvaa nguo zenye michoro na maandishi au picha ambazo utawala wa utumishi wa umma umeelezea kuwa 'haziendani na shughuli za serikali.' Pamoja na hayo wafanyakazi wa umma wamepigwa marufuku kuvaa nguo zenye maandishi ya chama chochote cha siasa au kuonesha ushabiki wa kitu fulani.
Nguo ambazo zinaacha sehemu ya mwili wazi kama vile kitovu na kifua au zinazoonyesha maungo ya mwili.

Je, unakubaliana na muongozo huu? Je, katika nchi yako kuna utaratibu gani wa mavazi?

Picha :OFISI YA RAIS,MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA, JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
Japan yaonya kuhusu urafiki ambao umeonekana kutoka Korea Kaskazini
Japan imeuambia mkutano wa kimataifa kuhusu Korea Kaskazini kuwa dunia isifumbwe macho na urafiki amabo umeanza kuonekana kutoka kwa Korea Kaskazini.

Matamshi ya waziri wa mashauri ya nchi za kigeni Taro Kono huko Canada, yanakuja huku Korea Kaskazini na Kusini wakijadili mipango ya Korea Kaskzini kushiriki mashindano ya msimu wa baridi nchini Korea Kusini.

Mawaziri 20 wa mashauri ya nchi za kigeni huko Vancouver walikubaliana kuongeza shinikizo didi ya Korea Kaskazini.

Lakini waliunga mkono mazungumzo yanayoendelea kati ya Korea Kaskazini na Kusini.
Kwa miaka miwili iliyopita Korea Kaskazini kwa haraka iliboresha programu yake ya makombora licha ya kuwepo vikwazo vya kimataifa.

Jaribio la mwisho la kombora la masafa marefu la tarehe 28 Novemba lilizua awamu mpya ya vikwazo kutoka kwa Umoja wa Mataifa ambavyo vililenga uagizaji wa mafuta na usafiri.

Lakini kiongozi wa Korea Kim Jong-un mapema Januari alisema kuwa yuko tayari kwa mazungumzo na Korea Kusini na kupendekeza kutuma timu kwa mashindano huko Pyeongchang mwezi ujao.
TETESI ZA SOKA ULAYA LEO 17.01.2018


TETESI ZA SOKA ULAYA JUMATANO 17.01.2018

Chelsea wamezungumza na West Ham kuhusu kumsajili Andy Carroll, 29, kwa mkataba wa kudumu. (Telegraph)

West Ham wapo tayari kusikiliza dau la kuanzia pauni milioni 20 ili kumuuza Andy Carroll. (Sky Sports)

Kiungo wa kimataifa wa Armenia Henrikh Mkitaryan, 28, anataka kuongezewa mshahara kwanza ili kuhama kutoka Manchester United kwenda Arsenal. (Mirror)

Alexis Sanchez alikuwa na wasiwasi na sera za kuchezesha kwa zamu za Pep Guardiola kabla Manchester City haijabadili mawazi ya kumsajili. (Manchester Evening News)

Zinedine Zidane amemtaka rais wa Real Madrid Florentino Perez kumsajili winga wa Manchester City Raheem Sterling kuziba pengo la Gareth Bale. (Don Balon)

Matumaini ya Real Madrid ya kumsajili Eden Hazard yanategenea iwapo Chelsea wataweza kumsajili Alexis Sanchez. (Don Balon)

Everton wanakaribia kumsajili winga wa Arsenal Theo Walcott, 28, siku ya Jumatano. (Liverpool Echo)

Mshambuliaji wa kimataifa wa Gabon Pierre-Emerick Aubameyang, 28, ameiomba Borussia Dortmund kumuachia ajiunge na Arsenal. (Mirror)

Baba yake Pierre-Emerick Aubameyang, ambaye pia ni wakala wake anasafiri kwenda London kuzungumza na Arsenal, kuhusu uhamisho wa mwanaye, huku Dortmund wakisubiri kuona kama wataweza kumpata Mitchy Batshuayi. (Bild)

Real Madrid wapo tayari kuapnda dau la euro milioni 70 kumsajili Pierre-Emerick Aubameyang kutoka Dortmund. (Don Balon)

Kiungo wa Arsenal Jack Wilshere, 26, ambaye mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu lazima afanye vipimo vya afya na kukubali kukatwa mshahara kwa asilimia 20 kama anataka mkataba mpya Emirates. (Sun)

Juventus wanajiandaa kupanda dau la kumsajili beki wa kulia wa Arsenal Hector Bellerin. (Calciomercato)

Kiungo wa Liverpool Marko Grujic, 21, ananyatiwa na Middlesbrough na Cardiff City. (ESPN)

Aleix Vidal huenda akaondoka Barcelona na kuelekea EPL mwezi huu baada ya Sevilla kuacha kumfuatilia. (Estadio Deportivo)

Simon Mignolet anafikiria kuondoka Liverpool huku Napoli wakifikiria kupanda dau la euro milioni 20. (Het Niewsblad)

Chelsea wanataka kumsajili beki wa kushoto wa Roma Emerson Palmieri mwezi huu. (Gianluca Di Marzio)

Meneja wa Manchester United Jose Mourinho anasisitiza kuwa Maroanne Fellaini lazima abakie Old Trafford. (Sun)

Mshambuliaji wa Southampton Manolo Gabbiadini, 26, huenda akarejea katika klabu yake ya zamani Bologna. (Sky Italia)

Tottenham ni miongoni mwa timu zinazomnyatia kiungo wa Norwich James Maddison, 21. (Evening Standard)

Barcelona wamekataa dau la pauni milioni 22.2 kutoka Inter Milan la kumtaka kiungo Rafinha, 24. Barca wanataka pauni milioni 35.5. (Mundo Deportivo)

Zinedine Zidane huenda akaondoka Real Madrid baada ya kupewa nafasi ya kuwa meneja wa timu ya taifa ya Ufaransa. (Diario Gol)

Tetesi nyingine kesho tukijaaliwa. Uwe na siku njema
Rais Magufuli Akutana na Waziri wa TAMISEMI, Selemani Jafo Na Kupiga Marufuku Michango Yote Shuleni
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo Januari 17, 2018 amepiga marufuku aina yoyote ya michango katika shule za Serikali za msingi na Sekondari na kuwaagiza Mawaziri Jafo na Ndalichako kusimamia hilo.

Magufuli amepiga marufuku hiyo hiyo leo alipokutana na Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Selemani S. Jafo na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Profesa Joyce L. Ndalichako Ikulu jijini Dar es salaam na kuwataka mawaziri hao kwenda kusimamia jambo hilo na kuhakikisha hakuna michango yoyote wanafunzi au wazazi wanachangishwa kwenye shule za sekondari.

"Tumesema elimu bure,  haiwezi ikaja kwa mgongo mwingine ikawa elimu pesa . Tumeweka utaratibu kwamba kuanzia shule ya msingi mpka sekondari form four hakuna kulipa ada yoyote lakini sasa hivi michango ya kila aina, nimewapa maelekezo kwamba kuanzia leo iwe ni marufuku na wakalisimamie hili sitaki kusikia mwanachi yoyote mahali popote akilalamika kwamba mtoto wake amerudishwa shule kwa sababu ya michango na walimu wote popote walipo wasishike mchango wowote wa mwanafunzi" amesema Rais Magufuli.

Aidha Rais Magufuli amesema kuwa kama kutakuwepo na mchango wowote wa mzazi ambaye atajisikia kuchangia jambo lolote kuhusu masuala ya shule basi pesa hizo zipelekwe kwa Mkurugenzi na si kushikwa na mwalimu yoyote yule