Monday, 26 March 2018

Wanafunzi Vyuo Vikuu Watajwa Kuongoza kwa Matusi Mitandaoni
Serikali imesema wanafunzi wa vyuo vikuu wanaongoza  kutukana na kutumia lugha zisizo na maadili kwenye mitandao ya kijamii.

Angalizo hilo limetolewa na naibu waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha  Jumamosi Machi 24, 2018 katika hafla fupi ya uzinduzi wa Unilife Compus iliyopo Mkoa wa Kilimanjaro uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Mwenge na kuvikutanisha vyuo vikuu vyote vya mkoa huo.

Alisema  yapo mambo matatu ambayo yanachangia wanafunzi kutofanya vizuri, yakiwamo matumizi mabaya ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), anasa na starehe zilizopitiliza na kujiingiza kwenye siasa ambazo zinawanyima fursa ya kusoma vizuri.

“Serikali imebaini mambo yanayochangia kufifisha na kudidimiza jitihada za elimu tunayoitoa kuonekana bure. Kuna vitu ambavyo siyo vizuri  vinaendelea katika vyuo vyetu, ndizo changamoto tunatakiwa kukabiliana nazo. Chuoni unaweza kutengeneza au kuharibu maisha yako,” alisema.

Naye mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira alisema  wanafunzi wengi hawataki kujifunza  kwa kutumia muda vizuri kwa kusoma vitabu.

"Tunabaki kuwa waigaji wa dhana za wenzetu wa magharibi, hatutaki kujifunza vitu vipya bali vilevile vya wenzetu vinatumika hadi leo. Wasomi wa Tanzania tunajishusha kwa sababu ya kushindwa kuleta mawazo mapya kwenye sekta ya elimu na afya," alisema  Mghwira.

Thursday, 18 January 2018

Kiongozi wa CCM(UVCCM) Iringa Achomewa Nyumba.
Nyumba ya Katibu wa Umoja wa Vijana Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wa Mkoa wa Iringa, Alphonce Muyinga iliyopo maeneo ya Kihesa njiapanda ya Kwabeda imechomwa moto na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia leo.

Ambapo kikosi cha Zima Moto kilifanikiwa kufika katika nyumba hiyo na kujaribu kuzima moto huo ambao tayari ulikuwa umeshaleta athari ndani ya nyumba hiyo kwa mali mbalimbali zilizokuwepo ndani.

Pia aliyekuwa Diwani wa kata ya Mwangata, Iringa kwa tiketi ya Chadema na baadaye kujiuzulu nafasi yake hiyo, Anjelus Mbogo naye amefanyiwa uharibifu katika nyumba ambayo alikuwa akijenga baada ya watu wasiojulikana kuibomoa nyumba hiyo.

Anjelus amedai kuwa tukio hilo linawezekana kuwa limetokea kutokana na matamko ya uchochezi yaliyotolewa na Mbunge kwa wananchi.

“Kauli ya Mbunge ndiyo inaweza kuwa chanzo cha uchochezi kwa wananchi kuja kubomoa nyumba hizi kwa sababu yeye aliwaambia wananchi kama atajiuzulu wabomoe nyumba yake hata gari yake ichomwe moto nadhani wananchi wakachukua hilo kwani wananchi unapowashawishi ndivyo unavyomuaminisha kuja kufanya hivi huo ndiyo ukweli. Na mimi sisemi mambo mengi kwa kuwa jambo hilo bado linaendelea na upelelezi lakini naamini wameniaminisha kuwa hatabaki mtu” amesema Anjelus Mbogo

Aidha amesema hawezi kuongea mengi zaidi kwani swala hilo linafanyiwa upelelezi kubaini watu hao wasiojulikana.

Wednesday, 17 January 2018

Rais Magufuli Akutana na Waziri wa TAMISEMI, Selemani Jafo Na Kupiga Marufuku Michango Yote Shuleni
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo Januari 17, 2018 amepiga marufuku aina yoyote ya michango katika shule za Serikali za msingi na Sekondari na kuwaagiza Mawaziri Jafo na Ndalichako kusimamia hilo.

Magufuli amepiga marufuku hiyo hiyo leo alipokutana na Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Selemani S. Jafo na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Profesa Joyce L. Ndalichako Ikulu jijini Dar es salaam na kuwataka mawaziri hao kwenda kusimamia jambo hilo na kuhakikisha hakuna michango yoyote wanafunzi au wazazi wanachangishwa kwenye shule za sekondari.

"Tumesema elimu bure,  haiwezi ikaja kwa mgongo mwingine ikawa elimu pesa . Tumeweka utaratibu kwamba kuanzia shule ya msingi mpka sekondari form four hakuna kulipa ada yoyote lakini sasa hivi michango ya kila aina, nimewapa maelekezo kwamba kuanzia leo iwe ni marufuku na wakalisimamie hili sitaki kusikia mwanachi yoyote mahali popote akilalamika kwamba mtoto wake amerudishwa shule kwa sababu ya michango na walimu wote popote walipo wasishike mchango wowote wa mwanafunzi" amesema Rais Magufuli.

Aidha Rais Magufuli amesema kuwa kama kutakuwepo na mchango wowote wa mzazi ambaye atajisikia kuchangia jambo lolote kuhusu masuala ya shule basi pesa hizo zipelekwe kwa Mkurugenzi na si kushikwa na mwalimu yoyote yule 


Monday, 15 January 2018

WATU 12 WAFARIKI KWA AJALI YA BARABARANI.
Watu 11 wamefariki dunia na wengine watano kujeruhiwa kutokana na ajali ya gari aina ya hiece kugongana na malori matatu katika kijiji cha Mubigera kata ya Nyantakara wilaya ya biharamulo mkoani kagera.

Gari hilo lilikuwa linasafiri kutoka wilaya ya kibondo kuelekea kahama mkoani Shinyanga

    Daktari mkuu wa hospitali teule ya Biharamulo Dr Grasmus Sebuyoya amethibitisha kupokea miili ya watu hao na majeruhi sita na kwamba kati ya majeruhi hao wawili hali zao ni mbaya na waliofariki wa jinsia ya kiume ni saba na jinsia ya kike ni watatu
Awali Mwenyekiti wa kijiji cha Mubigera Bw Mapunda Kayuki amesema ajali hiyo imetokea jana majira ya Saa 11 jioni ambapo hiece ilitaka kukwepana na roli kwenye barabara ya biharamulo kwenda kahama kwenye kijiji hicho na kugongana ambapo dereva wa hiece na utingo wake ni miongoni mwa waliofariki.

Bw Kayuki amesema hiece hiyo ilikuwa ikitokea kibondo kwenda kahama ambapo malori yaliyohusika kwenye ajali hiyo yako chini ya usalama wa jeshi la polisi kwa uchunguzi zaidi.

Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Kagera Agustino Olomi amesema hajakamilisha taarifa kamili ya tukio hilo ikiwa ni pamoja na kutambua majina ya waliopoteza maisha mpaka ajiridhishe na taarifa zitatolewa kwa umma bila kutia mashaka ili ndugu wa marehemu waweze kujua na kufuatilia kwa uhakika

Sunday, 14 January 2018

Dr. Ndumbaro Ashinda Ubunge Songea
Mgombea Ubunge jimbo la Songea Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dr. Damas Ndumbaro ameshinda Uchaguzi kwa kupata kura 45162 sawa na 97% akifuatiwa kwa mbali na mgombea Wa CUF aliyepata kura 608.

Matokeo rasmi yametangazwa na mkurugenzi wa uchaguzi jimbo la Songea mjini.

Thursday, 11 January 2018

Rais Magufuli amemteua aliyekuwa Katibu Mkuu Ikulu, Bw. Alphayo Kidata kuwa Balozi
Rais John Magufuli ameteua mabalozi wapya wawili ambao ni Alphayo Kidata na Meja Jenerali Mstaafu, Simoni Mumwi.

Taarifa iliyotolewa leo Alhamisi na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa imesema kuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi amesema uteuzi wa Kidata umeanza jana Jumatano Januari 10.

Kabla ya uteuzi huo Kidata alikuwa Katibu Mkuu, Ikulu.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa mabalozi hao wateule watapangiwa vituo vyao vya kazi na kuapishwa baada ya taratibu kukamilika.