Tuesday, 2 January 2018

Taarifa Ya Serikali Kuhusu Mwenendo Wa Hali Ya Uchumi Na Utekelezaji Wa Bajeti Ya Serikali Kwa Mwaka 2017/18



­­­
UTANGULIZI
Nashukuru sana kupata fursa nyingine ya kuzungumza nanyi leo tunapokaribia mwisho wa mwaka 2017. Lengo la Serikali ni kuwapatia Watanzania taarifa rasmi kuhusu (i) mwenendo wa uchumi wa Taifa kwa kipindi cha Januari hadi Juni 2017 na kwa miezi ya hivi karibuni pale ambapo tunazo takwimu, (ii) utekelezaji wa bajeti ya Serikali 2017/18 hadi sasa, (iii) changamoto zilizopo mbele yetu na matarajio mpaka Juni 2018. Aidha, nitatoa ufafanuzi kwa lugha nyepesi katika baadhi ya maeneo ambayo yamekuwa hayaelezwi ipasavyo au yanapotoshwa hususan katika mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo ya habari.

1.   MWENENDO WA UCHUMI WA TAIFA
Tunapozungumzia mwenendo wa uchumi tunaangalia viashiria mbalimbali. Niruhusuni nieleze baadhi ya viashiria muhimu kama ifuatavyo:
1.1        Ukuaji wa Uchumi
Kiashiria kimojawapo kinachotumika sana kimataifa kupima mwenendo wa uchumi ni ukuaji wa Pato la Taifa. Ukuaji wa Pato la Taifa ni badiliko (katika asilimia) la thamani ya bidhaa na huduma zilizozalishwa kutokana na shughuli mbalimbali za kiuchumi katika nchi zilizofanyika katika kipindi husika ikilinganishwa na kipindi sawia cha nyuma. Shughuli za kiuchumi zinajumuisha kilimo cha mazao, misitu, ufugaji na uvuvi; uzalishaji viwandani; biashara; ujenzi wa nyumba na barabara; huduma za fedha; habari na mawasiliano; usafiri na usafirishaji; huduma za utalii; na utoaji wa huduma nyingine kwa jamii ikiwa ni pamoja na afya, elimu na maji. Kiashiria hiki ni cha msingi kwa sababu kina uhusiano wa moja kwa moja na viashiria vingi vya mwenendo wa uchumi.
Katika nusu ya kwanza ya mwaka 2017 (Januari - Juni), Pato la Taifa (kwa bei za mwaka husika) liliongezeka na kufikia shilingi milioni 25,535,852 ikilinganishwa na shilingi milioni 23,915,750 katika kipindi kama hicho mwaka 2016. Hata hivyo, katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2017, Pato la Taifa lilikua kwa asilimia 6.8 ikilinganishwa na asilimia 7.7 katika kipindi kama hicho mwaka 2016.
Ufafanuzi: (a) Ukuaji wa uchumi hauendi wima au katika mstari ulionyooka. Mara zote huenda kama wimbi lenye ukubwa tofauti tofauti hasa pale ambapo uzalishaji wa bidhaa au huduma unapokuwa wa msimu (mfano msimu wa mavuno ya mazao ya kilimo au utalii). Hivyo wale wanaodhani ukuaji wa uchumi unatakiwa uongezeke katika kila kipindi wanakosea. (b) Aidha, pale ambapo kasi chanya ya ukuaji wa uchumi imepungua, haimaanishi kuwa uchumi umeporomoka. La hasha! Uchumi unakuwa umeporomoka kama unakua kwa kiwango hasi (negative GDP growth). Kasi ya ukuaji wa uchumi inaweza kufananishwa na mwendo wa gari. Gari linalokwenda mwendo kasi maana yake gari hilo hutumia muda mfupi kufika mwisho wa safari lakini kama gari hilo litakwenda kwa mwendo mdogo haina maana kwamba haliendi mbele au linarudi nyuma bali litachukua muda zaidi kufika. (c) Pamekuwepo hoja kuwa kasi hii kubwa ya ukuaji wa uchumi ni ya kitakwimu tu na haiakisi hali halisi ya maisha ya watu. Hili ni suala pana kidogo. Kwanza, ili kasi kubwa ya ukuaji wa uchumi iweze kuwanufaisha wananchi wengi sharti wananchi wengi wawe wanafanya kazi katika sekta zinazokua haraka ili kujipatia kipato. Lakini ilivyo hapa nchini kwa sasa wananchi wengi wanaishi vijijini na wanategemea kilimo ambacho kasi ya ukuaji wake bado ni ndogo (asilimia 2.1 mwaka 2016) kutokana na tija ndogo na kutegemea mvua. Sekta zinazokua haraka (Ujenzi 13%, Habari & Mawasiliano 13%, Usafirishaji na Uhifadhi wa Mizigo 11.8%, Uchimbaji wa Madini na Mawe 11.5%, Shughuli za Fedha & Bima 10.7%) haziajiri wananchi wengi.  Kwa maneno mengine kasi kubwa ya ukuaji wa Pato la Taifa utawagusa wananchi wengi kutegemea na mgawanyo wa hilo Pato la Taifa. Pili, kasi ya ongezeko la watu hapa nchini ni kubwa (2.7%) na hivyo inatengeneza idadi kubwa ya watu kugawana Pato dogo la Taifa. Tatu, pamoja na changamoto hizo nilizoeleza, napenda nisisitize kuwa kasi kubwa ya ukuaji wa uchumi ndiyo msingi wa kuboresha hali ya maisha katika nchi. Hili halina mbadala. Kama uchumi haukui, kipato hakiwezi kuongezeka!
Pamoja na kasi ya ukuaji wa uchumi kupungua kidogo katika kipindi cha nusu ya kwanza ya 2017 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2016, bado Tanzania ndiyo nchi iliyokuwa na kiwango kikubwa cha ukuaji wa uchumi ukilinganisha na nchi nyingine wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (Jedwali Na. 1).
NB: Chanzo cha takwimu hizi ni Benki ya Dunia ambao hivi majuzi Mwakilishi wake hapa nchini alikiri kuwa Tanzania ni moja ya nchi za Afrika yenye takwimu bora.
Jedwali Na. 1: Ukuaji wa Pato la Taifa Katika Baadhi ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kipindi cha nusu mwaka (%)
NCHI
2016
2017
Kenya
5.9
4.9
Rwanda
8.1
2.9
Tanzania
7.7
6.8
Uganda
3.8
4.9
Ethiopia
10.5
7.5
Democratic Republic of the Congo
8.5
9.0
Cote d’Ivoire
7.7
7.5
Mozambique
7.3
7.3
Chanzo: Ofisi ya Taifa ya Takwimu; na CIA World Factbook
Hata kwa bara la Afrika na dunia kwa ujumla, Tanzania inabaki kuwa miongoni mwa nchi 10 bora kwa kuwa na kasi kubwa ya ukuaji wa uchumi. Kwa mwaka mzima wa 2017, uchumi unatarajiwa kukua kwa asilimia 7.0 na kuendelea kukua kwa wastani wa asilimia 7.4 katika kipindi cha muda wa kati.
1.2        Mfumuko wa bei
Mfumuko wa bei ni kiashiria kinachopima mabadiliko ya wastani wa bei za bidhaa na huduma zinazotumiwa na kaya nchini. Mfumuko wa bei ukiwa mkubwa gharama za maisha zinapanda haraka sana. Napenda kuwajulisha Watanzania kuwa mfumuko wa bei umeendelea kubaki katika kiwango kizuri cha tarakimu moja (wastani wa asilimia 5.4) tangu Januari hadi Novemba 2017. Kwa mwezi Novemba mfumuko wa bei ulipungua hadi asilimia 4.4. Maana yake ni kuwa bei za wastani za bidhaa na huduma kwa mlaji zimekuwa zikiongezeka lakini kwa kasi ndogo. Hali hii imewezekana kutokana na utekelezaji madhubuti wa sera za bajeti na za fedha; kutengamaa kwa bei za bidhaa katika soko la dunia, hasa bei ya mafuta; utulivu wa thamani ya Shilingi; na upatikanaji mzuri wa mazao ya chakula katika soko la ndani na la nchi jirani. Bidhaa za chakula na mafuta kwa ujumla wake huchangia asilimia 45.8 ya bidhaa na huduma zote zinazotumika wakati wa ukokotoaji wa mfumuko wa bei, hivyo kukiwa na usambazi hafifu wa bidhaa hizo katika nchi husababisha ongezeko kubwa la kasi ya upandaji wa bei. Serikali inaendelea kufanya jitihada za kuimarisha sekta ya kilimo kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa uhakika wa chakula kwa kuendeleza maboresho ya miundombinu ya umwagiliaji, kuongeza upatikanaji wa pembejeo za kilimo, kuongeza huduma za ugani, kuboresha upatikanaji wa miundombinu ya hifadhi na masoko - yote hayo yakiwa na lengo la kutengamaza bei za mazao ya chakula.
Kwa upande wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Wastani wa mfumuko wa bei kwa ujumla uliendelea kubakia katika wigo wa tarakimu moja, Tanzania ikiwa na kiwango cha chini zaidi cha asilimia 5.4 na Kenya ikiwa na kiwango cha juu zaidi cha wastani wa asilimia 8.3 (Jedwali Na. 2).
Jedwali Na. 2: Mwenendo wa Mfumuko wa Bei kwa Baadhi ya Nchi za Afrika Mashariki (Asilimia)
Chanzo: Ofisi ya Taifa ya Takwimu
1.3        Thamani ya shilingi
Thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya Dola ya Kimarekani katika kipindi cha mwaka 2017 iliendelea kuwa imara, ikipungua thamani kwa kiwango kisichozidi asilimia 3. Katika kipindi cha mwezi Oktoba 2017, dola moja ya Marekani ilibadilishwa kwa wastani wa Shilingi 2,238.03 ikilinganishwa na wastani wa Shilingi 2,175.49 katika kipindi kama hicho mwaka 2016. Utulivu katika soko la fedha za kigeni ulitokana na kuimarishwa kwa usimamizi, utekelezaji wa sera thabiti za bajeti na za fedha (prudent fiscal and monetary policies) pamoja na mwenendo mzuri wa urari wa mapato ya fedha za kigeni. Ni dhahiri kuwa shilingi ya Tanzania hivi sasa ina heshima! Napenda kuipongeza kwa dhati Benki Kuu ya Tanzania kwa usimamizi makini wa sera za fedha.
1.4        Akiba ya Fedha za Kigeni
Akiba ya fedha za kigeni imeongezeka kufikia USD 5,911.2 milioni ambazo zinaiwezesha nchi kununua bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi cha miezi 5.4 ikilinganishwa na USD 4,093.7 milioni zilizofikiwa mwaka 2015. Kiasi hiki cha sasa cha akiba ya fedha za kigeni hakijawahi kufikiwa kwa zaidi ya miaka 10 na Kiko juu yao lengo lililowekwai na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki la kuwa na akiba ya fedha za kigeni inayokidhi kuagiza bidhaa na huduma nje ya nchi kwa miezi 4.5.
1.5        Mwenendo wa Sekta ya Kibenki
Mwenendo wa sekta ya kibenki katika mwaka 2017 uligubikwa na (i) kuongezeka kwa mikopo chechefu kutoka asilimia 9.1 mwishoni mwa mwezi Septemba 2016 hadi asilimia 12.5 mwezi September 2017 ikiwa ni juu ya wastani unaokubalika na Benki kuu wa asilimia 5; (ii) kupungua kwa kasi ya utoaji wa mikopo kwa sekta binafsi; na (iii) kupungua kwa faida itokanayo na uwekezaji kwenye rasilimali na mitaji (return on assets and equity). Faida itokanayo na uwekezaji kwenye rasilimali ilifikia asilimia 2.0 mwishoni mwa mwezi Septemba 2017 ikilinganishwa na 2.5% Septemba 2016. Faida itokanayo na uwekezaji wa mitaji ilipungua kufikia asilimia 8.7 ikilinganishwa na asilimia 12.1 mwaka 2016. Hali hii ilichangiwa zaidi na kupungua kwa kasi ya utoaji mikopo, kuongezeka kwa gharama za ukwasi (funding costs) pamoja na kuongezeka kwa mikopo chechefu.
Hatua zilizochukuliwa katika kukabiliana na changamoto hizo ni:
                     i.        Kuhamasisha benki za biashara kuongeza matumizi ya mfumo wa kuhifadhi na kutoa taarifa za wakopaji (credit reference system);
                    ii.        Benki Kuu kutoa mikopo ya muda mfupi kwa benki za biashara;
                  iii.        Benki Kuu kushusha riba (discount rate) kutoka asilimia 16.0 hadi asilimia 12.0 mwezi Machi 2017 na hatimaye asilimia 9.0 mwezi Agosti 2017;
                  iv.        Benki Kuu kupunguza kiwango cha chini cha amana kinachotakiwa kuwekwa Benki Kuu na benki za biashara (Statutory Minimum Reserve Requirement (SMR)) kutoka asilimia 10.0 hadi asilimia 8.0  kuanzia mwezi Aprili 2017; na
                    v.         Serikali kuendelea kulipa malimbikizo ya madai yaliyohakikiwa kwa lengo la kupunguza kiwango cha mikopo chechefu na kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi.
                  vi.        Benki kuu ilipunguza riba inayotozwa Serikali inapokopa kutoka Benki Kuu ya Tanzania kutoka asilimia 6.5 hadi asilimia 3.0 kuanzia tarehe 12 Desemba 2017 ili kuchochea utoaji wa mikopo
Kufuatia hatua hizo, ukwasi kwenye benki za biashara uliongezeka na kusaidia kupunguza riba ya mikopo baina ya mabenki (the interbank cash market rate) na kufikia wastani wa asilimia 3.53 mwezi Novemba 2017 kutoka wastani wa asilimia 14.93 kwa nusu ya kwanza ya mwaka 2016/17. Vile vile, riba za dhamana za Serikali zilishuka kutoka wastani wa asilimia 15.56 katika nusu ya kwanza ya mwaka 2016/17 hadi kufikia asilimia 8.76 mwezi Novemba 2017. Ni matarajio ya Serikali kuwa kasi ya ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi itaanza kuimarika.
Pamoja na changamoto hizo, Serikali inapenda kuwahakikishia wananchi kuwa kwa ujumla sekta ya kibenki imeendelea kuwa imara, salama na yenye kutengeneza faida, ikiwa na mitaji na ukwasi wa kutosha: Mwenendo wa viashiria mbalimbali unathibitisha ukweli huu:
                     i.        Uwiano wa mtaji wa msingi kwa rasilimali za benki (core capital to total risk weighted assets and off-balance sheet exposures) ulifikia asilimia 18.9 mwezi Septemba 2017, ukiwa juu ya kiwango kinachohitajika kisheria cha asilimia 10.0, na asilimia 18.6 iliyofikiwa mwezi Septemba2016.
                    ii.        Uwiano wa rasilimali kwa amana zinazoweza kubadilishwa kwa muda mfupi kuwa fedha taslimu (liquid assets to demand liabilities) ulifikia asilimia 37.9, ikilinganishwa na kiwango kinachohitajika kisheria cha asilimia 20. Hata hivyo, zipo benki (hasa community banks) ambazo zina viwango chini ya uwiano unaoelekezwa na sharia. Benki kuu inafuatilia kwa karibu ili kulinda utulivu wa sekta ya fedha na amana za wateja.
Aidha, napenda Watanzania waelewe kuwa changamoto zilizoikumba sekta ya fedha kuanzia mwaka 2016 ikiwemo upungufu wa ukwasi katika mabenki ya kibiashara na kuongezeka kwa kiwango cha mikopo chechefu siyo kwa Tanzania pekee. Kwa mfano mwezi Septemba 2017 Benki ya Taifa ya Rwanda ilitangaza kuwa kiwango cha mikopo chechefu katika soko lake kiliongezeka kutoka asilimia 6.2 mwezi Machi 2016 hadi asilimia 8.1 mwishoni mwa mwezi Juni 2017. Vivyo hivyo, nchini Kenya kiwango cha mikopo chechefu kiliongezeka kutoka asilimia 5.4 mwezi Septemba 2012 hadi asilimia 9.5 mwezi Machi 2017. Kwa nchi ya Uganda kiasi cha mikopo chechefu kiliongezeka kutoka asilimia6.2 hadi asilimia10.5. Mwenendo huu umejitokeza katika nchi nyingine kama Ghana, Nigeria n.k. Aidha, napenda pia nisisitize kuwa yale yanayosemwa mtaani kuwa “vyuma vimebana” Watanzania wajue kuwa ni vile vyuma vyenye kutu!! yaani vipato vyote visivyo halali vilivyotokana au kuchochewa na ukwepaji kodi, biashara haramu ya madawa ya kulevya, rushwa, ubadhirifu, na posho au mishahara isiyowiana na kazi. Ni lazima Watanzania wote turudi kwenye utaratibu wa kuishi ndani ya uwezo wetu yaani vyanzo halali vya mapato ya kazi zetu (kilimo, ufugaji, uvuvi, biashara safi, uwekezaji au kazi za kuajiriwa na kujiajiri).
1.6        Deni la Taifa
Hadi kufikia mwishoni mwa Septemba, 2017 deni la Taifa lilifikia shilingi bilioni 47,823.1 ikilinganishwa na shilingi bilioni 42,552.4 katika kipindi kama hicho mwaka  2016. Kati ya kiasi hicho, Shilingi bilioni 13,417.5 ni deni la ndani shilingi bilioni 34,405.6 ni deni la nje. Deni la ndani ni sawa na asilimia 28.1 ya deni lote na deni la nje ni asilimia 71.9. Nisisitize hapa kuwa ongezeko la deni la Taifa lilitokana na kupatikana kwa mikopo mipya ya nje na ndani kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo. Baadhi ya miradi iliyogharamiwa na mikopo hiyo ni:
                     i.        Ujenzi wa Mradi wa umeme (Kiwira Coal Mine);
                    ii.        Miradi ya uboreshaji wa huduma za maji;
                  iii.        Mradi wa kuzalisha umeme wa Kinyerezi (150MW); na
                  iv.        Ujenzi na ukarabati wa Viwanja vya ndege
Tathmini ya uhimilivu wa deni iliyofanyika mwezi Novemba 2017 inaonesha kuwa uwiano wa deni kwa Pato la Taifa ni asilimia 32.5 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 56. Hii ina maana kuwa deni la Taifa lipo chini ya ukomo wa hatari na ni himilivu katika kipindi cha muda wa kati na muda mrefu.
Serikali inapenda kusisitiza tena kwamba hakuna dhambi kwa nchi kukopa kwa busara (prudently). Mambo ya muhimu ya kujiridhisha nayo ni kuwa  mikopo hiyo itumike kujenga uwezo zaidi wa kuzalisha mali (productive capacity) na kurejesha mikopo hiyo kwa kuzingatia uwezo wa uchumi kuhimili mzigo wa madeni (debt sustainability).
2.   MWENENDO WA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA SERIKALI
                       (JULAI – SEPTEMBA 2017)
2.1        Mwenendo wa Mapato ya Ndani
Mapato ya ndani yaliongezeka kwa asilimia 1.0 kufikia shilingi bilioni 4,067.4 ikilinganishwa na shilingi bilioni 4,033.1 zilizokusanywa katika kipindi kama hicho mwaka 2016/17.  Hata hivyo, kiasi kilichokusanywa kilikuwa asilimia 15 pungufu ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 4,793.0 katika kipindi hicho. Kati ya makusanyo hayo, mapato ya kodi yalikuwa shilingi bilioni 3,564.0 ikiwa ni asilimia 86 ya lengo la shilingi bilioni 4,161.4; mapato yasiyo ya kodi yalikuwa shilingi bilioni 378.7 sawa na asilimia 84.9 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 445.9; na mapato ya Halmashauri yalikuwa shilingi bilioni 124.7 ikiwa ni asilimia 67.2 ya lengo la shilingi bilioni 185.7.
a)   Mwenendo wa Vyanzo vya Mapato ya Kodi
Makusanyo ya kodi za ushuru wa forodha yalikuwa shilingi bilioni 1,037.0 sawa na asilimia 83 ya lengo (shilingi bilioni 1,246.8). Aidha, mapato haya yako chini kwa asilimia 2 ilinganishwa na kiasi kilichokusanywa katika kipindi kama hicho 2016.
Kodi za Ndani
Makusanyo halisi kutokana na kodi za mauzo ya ndani yaliongezeka kwa asilimia 7.0 katika kipindi cha robo Julai hadi Septemba 2017 kufikia shilingi bilioni 845.0 kutoka shilingi bilioni 789.4 katika kipindi kama hicho mwaka 2016. Mapato hayo yalifikia asilimia 88 ya lengo la shilingi bilioni 961.8.
Makusanyo ya kodi ya mapato yalikuwa shilingi bilioni 1,182.7 ikiwa ni asilimia 86 ya lengo la shilingi bilioni 1,381.6. Makusanyo haya ni ukuaji wa asilimia 2.6 ikilinganishwa na kipindi kama hicho kwa mwaka 2016. 
b)   Mapato yasiyotokana na kodi
Makusanyo ya mapato yasiyo ya kodi yalikuwa shilingi bilioni 378.7 ambayo ni asilimia 84.9 ya lengo (shilingi bilioni 445.9). Kutofikiwa kwa malengo kulitokana na upungufu wa vitendea kazi na vifaa kwa baadhi ya Wizara, Idara na Wakala kwa ajili ya shughuli za ukusanyaji mapato na baadhi ya MDAs kuendelea kutumia stakabadhi za malipo (ERVs) katika kukusanya mapato. Makusanyo ya mapato yasiyo ya kodi yaliongezeka kwa asilimia 16.9 ikilinganishwa na makusanyo ya mwaka 2016 katika kipindi kama hiki. Ongezeko hili limechangiwa na kuongezeka kwa matumizi ya mifumo ya malipo ya kielectroniki kwa baadhi ya MDAs na kuboreshwa kwa usimamizi wa mapato yasiyo ya kodi. Makusanyo ya Halmashauri yalikuwa shilingi bilioni 124.7 sawa na asilimia 67.2 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 185.7.
Kwa mwezi Oktoba peke yake, mapato ya ndani ukijumuisha mapato ya halimashauri yalifikia shilingi bilioni 1,465.9 sawa na asilimia 90.6 ya makadirio ya shilingi bilioni 1,617.9 kwa kipindi hicho. Kati ya kiasi kilichokusanywa kwa mwezi Oktoba 2017, mapato ya kodi yalikuwa shilingi bilioni 1,264.4 (sawa na asilimia 92.0 ya lengo); mapato yasiyo ya kodi yalikuwa shilingi bilioni 158.1 (asilimia 86.7) na mapato ya halmashauri shilingi bilioni 43.402 (asilimia 71.6).
Uhalisia wa Maoteo ya Ukusanyaji wa Mapato
Wapo wadau wanaodai kwamba maoteo yetu ya ukusanyaji wa mapato hayana uhalisia (unrealistic) na kupelekea kulundikana kwa madai (accumulation of arrears). Serikali kwa upande wake inaamini kuwa malengo ya ukusanyaji wa mapato tuliyojiwekea yanaweza kabisa kufikiwa hususan kwa kufanya jitihada kubwa zaidi kuziba mianya ya uvujaji wa mapato, kuongeza matumizi ya njia za kielektroniki katika ukusanyaji (ikiwemo EFDs na scanners za mizigo bandarini), kupanua wigo wa wa kodi na mapato yasiyo ya kodi. Kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato kutoka wastani wa shilingi 850 bilioni kwa mwezi wakati wa serikali ya awamu ya tano hadi wastani wa shilingi 1.2 trilioni kwa mwezi hivi sasa pamoja na uwepo bado wa mianya ya uvujaji wa mapato na vyanzo vingine vikubwa vya mapato ambavyo bado havijatozwa ipasavyo (mfano: uvuvi baharí kuu, kodi ya ardhi, tozo kwenye rasilimali za misitu, kodi ya majengo mijini, sekta isiyo rasmi, tozo za mifugo n.k), ni ushahidi dhahiri kuwa bado ipo nafasi ya kukusanya mapato zaidi ya Serikali. Haya ndiyo maeneo ambayo marafiki zetu wanapaswa kujielekeza kutusaidia kwa maana ya vifaa na utaalam katika ukusanyaji wa mapato badala ya kubishania tarakimu za maoteo.
c)   Misaada na Mikopo Yenye Masharti Nafuu
Takwimu zinaonyesha kuwa mchango wa misaada na mikopo ya masharti nafuu katika bajeti ya Serikali umekuwa ukipungua. Katika mwaka 2017/18, jumla ya shilingi bilioni 3,971.1 ziliahidiwa na Washirika wa Maendeleo kwa ajili ya utekelezaji wa bajeti (sawa na asilimia 12.5 ya bajeti yote). Hadi kufikia mwisho wa mwezi Septemba, jumla ya shilingi bilioni 325.9 zilitolewa na Washirika wa Maendeleo kwa ajili ya utekelezaji wa bajeti. Hii ni sawa na asilimia 62.3 ya lengo la kipindi hicho cha robo mwaka. Kati ya fedha zilizotolewa hadi kufikia mwezi Septemba 2017, shilingi bilioni 58.02 zilipokelewa kupitia mifuko ya pamoja, ikiwa ni sawa na asilimia 50.6 ya makadirio yaliyowekwa na shilingi bilioni 267.9 zilizotolewa kupitia miradi ya maendeleo, sawa na asilimia 65.7 ya makadirio ya bajeti ya robo mwaka iliyowekwa. Hata hivyo, hakuna fedha za misaada ya kibajeti zilizopokelewa kwa kipindi hicho na hii ni kuendana na mtiririko wa fedha (cash flow) ambapo hakuna fedha zilizotarajiwa kwa kipindi hicho.
Kutokana na kutotabirika kwa fedha za misaada na mikopo nafuu, Serikali imeongeza jitihada katika ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kuondokana na utegemezi. Kufuatia jitihada hizo, utegemezi (Misaada na mikopo nafuu) umepungua kutoa asilimia 16.8 ya bajeti halisi ya mwaka 2014/15 hadi asilimia 12.5 kwa mujibu wa makadirio ya bajeti ya mwaka 2017/18. Rai yangu: Kila Mtanzania awajibike kulipa kodi ili ajipatie uhalali wa kudai haki ya kufaidi huduma zinazotolewa na Serikali. Serikali inawashukuru kwa dhati Wananchi wote ambao wameendelea kulipa kodi kwa uzalendo mkubwa na tunawaomba waendelee hivyo.
d)   Mikopo ya ndani
Katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2017, Serikali iliweza kukopa jumla ya shilingi bilioni 1,655.3 kutoka katika soko la ndani sawa na asilimia 96.6 ya lengo la kukopa shilingi bilioni 1,714.3.  Kati ya kiasi hicho shilingi bilioni 1,107.1 zilikuwa kwa ajili ya kulipia Hati Fungani na Dhamana za Serikali zilizoiva (Roll over) na shilingi bilioni 548.2 zilikuwa mikopo mipya kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo. Mwenendo wa mikopo ya ndani ulikuwa wa kuridhisha ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2016.
e)   Mikopo ya Kibiashara
Serikali ilipanga kukopa mikopo yenye masharti ya kibiashara kiasi cha shilingi bilioni 1,595.0 kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo. Hadi Septemba 2017, jumla ya shilingi bilioni 224.6 zilipatikana kutoka katika benki ya Credit Suisse. Majadiliano na taasisi   nyingine   za   fedha yameendelea kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali.
2.2        Mwenendo wa Matumizi
Utoaji wa Fedha
Katika kipindi cha kuanzia Julai – Novemba, 2017 jumla ya shilingi bilioni 10,494.4 zilitolewa kwa Wizara, Idara za Serikali zinazojitegemea, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa Tanzania Bara. Kati ya kiasi hicho kilichotolewa, shilingi bilioni 8,450.7 zilitolewa kwa ajili ya matumizi ya kawaida (ikijumuisha makusanyo ya Halmashauri shilingi bilioni 119.1), shilingi bilioni 2,043.7 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo (ikijumuisha makusanyo ya Halmashauri shilingi bilioni 80.6). Utoaji wa fedha za maendeleo za ndani na nje ulikuwa kidogo kwa sababu baadhi ya mikopo ya masharti nafuu na yale ya kibiashara iliyotarajiwa haikuweza kupatikana kwa wakati ikiwa ni pamoja na kuchelewa kwa mikopo na misaada kutoka kwa Washirika wa Maendeleo.
Aidha, fedha za matumizi ya kawaida zinajumuisha shilingi bilioni 2,711.2 zilizotolewa kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa Serikali, shilingi bilioni 4,121.7 zilizotolewa kwa ajili ya Deni la Taifa na shilingi bilioni 1,617.8 zilitolewa kwa ajili ya matumizi mengineyo. Vile vile fedha za Maendeleo zilizotolewa zinajumuisha fedha za ndani shilingi bilioni 1,822.2 na fedha za nje shilingi bilioni 221.5.
Katika utoaji wa fedha hizo, kuna mahitaji yaliyopewa kipaumbele zaidi kwenye fedha za matumizi ya kawaida na fedha za maendeleo kwa kipindi cha Julai – Novemba, 2017 kama ifuatavyo:
(i)           Malimbikizo ya madai (arrears) shilingi bilioni 369.8;
(ii)          Mfuko wa barabara shilingi bilioni 328.3;
(iii)        Madai ya wakandarasi wa barabara shilingi bilioni 282.2;
(iv)        Mikopo kwa wanafunzi Elimu ya juu shilingi bilioni 253.9. Kwa mara ya kwanza wanafunzi wamepelekewa hela zao hata kabla ya vyuo kuanza kufunguliwa;
(v)          Usambazaji wa umeme vijijini (REA) shilingi bilioni 135.7;
(vi)        Elimu bila malipo shilingi bilioni 78.5;
(vii)       Mfuko wa Reli shilingi bilioni 69.9;
(viii)      Mfuko wa maji shilingi bilioni 64.6; na
(ix)        Ununuzi wa madawa ya binadamu.
2.3        Ulipaji wa Madai mbalimbali
Mwaka 2016/17, jumla ya shilingi bilioni 963.5 za malimbikizo ya madai mbalimbali yaliyohakikiwa zililipwa. Aidha, katika kipindi cha Julai – Novemba 2017, fedha zilizotolewa kwa ajili ya ulipaji wa malimbikizo ya madai mbalimbali ya wakandarasi, watoa huduma na watumishi ni shilingi bilioni 652.0. Madeni ya Serikali na taasisi zake yanatokana na sababu mbalimbali zikiwemo: Ufinyu wa mapato ya Serikali usiokidhi mahitaji halisi; Kuingia mikataba na wazabuni bila kuzingatia Sheria ya Fedha na Sheria ya Ununuzi wa umma; na Kutozingatia miongozo inayotolewa na Mlipaji Mkuu wa Serikali kuhusu usimamizi na utekelezaji wa bajeti.
Serikali inaendelea na zoezi la kulipa madai yaliyohakikiwa sambamba na kuimarisha jitihada za kuzuia madai mapya.
3.   CHANGAMOTO
Pamoja na mafanikio hayo, changamoto kadhaa zilijitokeza zikiwemo:-
(i)           Baadhi ya wafanyabiashara na wananchi ya kutolipa kodi stahiki  hususan kutumia mashine za kielektroniki;
(ii)          Ukusanyaji dhaifu wa mapato unaofanywa na MDAs na LGAs;
(iii)        Kutopatikana kwa wakati kwa mikopo yenye masharti nafuu na ile ya kibiashara kutoka nje;
(iv)        Kuongezeka kwa malimbikizo ya madai; na
(v)          Wafadhili kupendelea zaidi kufadhili miradi moja kwa moja badala ya utaratibu wa kupitia bajeti ya Serikali (GBS) unaoiwezesha Serikali kupanga matumizi kulingana na vipaumbele vyake.
4.   MAMBO MENGINE MUHIMU
4.1        Mashauriano Kati ya Serikali na Sekta Binafsi
Serikali ya awamu ya tano inaamini kuwa maendeleo endelevu yatapatikana kwa haraka zaidi katika mazingira ambapo kuna ushirikiano wa kweli na wa dhati kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi. Hii inatokana na ukweli kwamba Sekta ya Umma na Sekta Binafsi vinategemeana sana. Kama shughuli za Sekta Binafsi zikidorora, hakika shughuli za serikali nazo zitadorora. Aidha, mafanikio ya Sekta ya Umma yanategemea uchangamfu na kasi ya ukuaji wa sekta Binafsi na vivyo hivyo, mafanikio ya sekta binafsi yanategemea uwepo wa sera na sheria nzuri pamoja na mfumo wa uratibu wenye ufanisi ambavyo vinasimamiwa na sekta ya umma. Kwa mantiki hii, Sekta ya umma na Sekta Binafsi hazina budi kufanya kazi kwa kushirikiana kwa karibu, tena kwa kuaminiana kwa faida ya sekta zote mbili na kwa maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
Kutokana na ushirikiano huo, Serikali imekuwa ikifanya mikutano ya mashauriano ya mara kwa mara na sekta binafsi ili kujenga kuaminiana  na kupokea maoni yao kuhusu sera, sheria (hasa za kodi) na kero zinazokwamisha biashara na uwekezaji nchini kwa lengo la kuzitatua. Lengo ni kujenga mazingira rafiki kwa sekta binafsi kushamiri ikiwa pamoja na uwepo wa sera zinazotabirika na mfumo-rekebu mzuri. Tayari Serikali imeandaa mpango kazi (Blueprint) ambao utekelezaji wake utawezesha kupunguza au kuondoa kabisa kero zinazoikabili sekta binafsi.
4.2        Matumizi ya Fedha za Kigeni Katika Uchumi (Dollarization)
Suala la matumizi ya fedha za kigeni sambamba na shilingi ya Tanzania hapa nchini linasimamiwa na (a) Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Kigeni ya Mwaka 1992 (The Foreign Exchange Act, 1992), (b) Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya Mwaka 2006, na (c) Tamko la Serikali la mwaka 2007 kuhusu matumizi ya fedha za kigeni kulipia bidhaa na huduma katika soko la ndani.
Matumizi ya fedha za kigeni sambamba na shilingi ya Tanzania wakati wa kufanya miamala mbalimbali yanaweza kuwa na athari kiuchumi ikiwa ni pamoja na kudhoofisha thamani ya shilingi. Sheria iliyopo kwa sasa haikatazi jambo hili bali inasisitiza kuwa sarafu ya Tanzania ndiyo fedha halali na mtu au taasisi yoyote itakayekataa kupokea malipo kwa shilingi za Tanzania atachukuliwa hatua za kisheria. Hata hivyo, suala hili limeendelea kuwa kero kwa wananchi kutokana na ugumu wa kusimamia matakwa ya sheria. Inafahamika kuwa baadhi ya wateja wanapewa kiwango cha thamani ya kubadilisha fedha ambacho kiko juu kuliko thamani halisi iliyoko kwenye soko na hivyo kinamuumiza zaidi mteja husika. Hivyo, suala hili linahitaji kufanyiwa marekebisho ya Sheria husika. Ili kukabiliana na kero kama hizo wakati utaratibu wa kurekebisha sheria unaendelea,  Serikali inaagiza yafuatayo yatekelezwe kuanzia tarehe 1 January 2018:
(i)         Bei zote hapa nchini zitangazwe kwa shilingi ya Tanzania. Bei hizi zinajumuisha kodi ya nyumba za kuishi na maofisi; bei ya ardhi; gharama za elimu na afya; be iza vyombo vya usafiri na vifaa vya kielektroniki;
(ii)        Bei ambazo walengwa wake wakuu ni watalii au wateja wasio wakazi zinaweza kutangazwa kwa fedha za kigeni na malipo yake yanaweza kufanyika kwa fedha za kigeni. Bei hizi zinajumuisha gharama za usafirishaji kwenda nchi za nje kupitia Tanzania; gharama za mizigo bandarini kwenda nchi za nje; gharama za viwanja vya ndege na visa kwa wageni; na gharama za hoteli kwa wtalii kutoka nje ya nchi. Walipaji wanaotumia fedha za kigeni watambuliwe kwa vitambulisho vyao kama pasi za kusafiria na nyaraka za usajili kwa makampuni;
(iii)       Viwango vya kubadilishana fedha vitakavyotumika katika kuweka hizo bei katika sarafu mbili viwekwe wazi na visizidi vile vya soko. Ifahamike wazi kuwa ni mabenki na maduka ya fedha za kigeni tu yanayoruhusiwa kupanga viwango vya kubadilisha fedha kutokana na ushindani katika soko la fedha za kigeni;
(iv)       Mkazi yeyote wa Tanzania asilazimishwe kulipia bidhaa au huduma yeyote hapa nchini kwa fedha za kigeni; na
(v)         Vyombo vya dola viwachukulie hatua za kisheria wale wote watakaobainika kukiuka maagizo haya ya Serikali.
5.   MWELEKEO NA MATARAJIO HADI JUNI 2018
Kwa kuzingatia mwenendo wa ukuaji wa uchumi kwa kipindi cha Januari hadi Juni 2017 na mapitio ya viashiria muhimu vya kiuchumi, matarajio ni kwamba kasi ya ukuaji wa uchumi kwa mwaka 2017 unatarajiwa kufikia asilimia 7.0 ukitegemewa na uwekezaji mkubwa katika miundombinu hususan ujenzi wa reli mpya ya kati (SGR), bomba la mafuta kutoka Uganda, mradi wa umeme Stigler’s gorge, mradi wa umeme Kinyerezi, Jengo la III la abiria JNIA, ujenzi wa barabara mbalimbali na uwekezaji wa sekta binafsi kwenye viwanda na huduma mbalimbali hususan utalii, biashara, usafirishaji wa mizigo kwenda nchi jirani na huduma za fedha. Aidha, mfumuko wa bei unatarajiwa kuendelea kubaki kwenye tarakimu moja na thamani ya shilingi kuendelea kuimarika kutokana na hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania.
Matarajio haya ya kuimarika kwa ukuaji wa uchumi yatategemezwa na miradi mikubwa ambayo baadhi imeshaanza kutekelezwa au iko katika hatua za awali. Baadhi ya miradi hiyo ni:
     i.        Ujenzi wa bwawa kubwa na mtambo wa kufua umeme katika bonde la Mto Rufiji (sehemu inayojulikana kama Stigler’s Gorge) litakalokuwa na uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 2,100. Utekelezaji wa mradi huu unatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha 2018/19. Aidha, kuna miradi mingine ya kuzalisha umeme Kinyerezi (150 MW) na Kiwira;
    ii.        Ujenzi wa reli mpya ya kati kwa kiwango cha standard gauge kati ya Dar es Salaam na Morogoro ambao tayari umeanza na mkataba wa ujenzi wa kipande cha Morogoro hadi Makutopora umeshasainiwa.
   iii.        Ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima (Uganda) hadi bandari ya Tanga pamoja na ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya barabara mbalimbali nchini zikiwemo barabara za juu (flyover) TAZARA na Ubungo;  na uimarishaji wa viwanja vya ndege ikiwemo jengo la abiria Na. III katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere ambao ujenzi wake unakaribia kukamilika;
   iv.        Kasi kubwa ya ujenzi wa viwanda mbalimbali unaofanywa na sekta binafsi na vingine kwa ubia na sekta ya umma katika mikoa mbalimbali nchini na kufufua viwanda vilivyobinafsishwa. Aidha zinafanyika jitihada za kuanzisha na kuendeleza maeneo ya viwanda (Industrial parks) na maeneo ya Teknolojia (Technological Parks); Kupanua na Kuimarisha Shughuli za Shirika la Viwanda Vidogo – SIDO; na kutumia taasisi za umma katika kusukuma mageuzi ya viwanda nchini; na
    v.        Kuimarisha kilimo kwa ajili ya upatikanaji wa uhakika wa chakula na malighafi za viwanda, kuendeleza maboresho ya miundombinu ya umwagiliaji, kuongeza upatikanaji wa pembejeo za kilimo, kuboresha utafiti wa kilimo na mbegu bora, kuboresha huduma za ugani, kuboresha usindikaji wa mazao na upatikanaji wa miundombinu ya hifadhi na masoko.
Kipaumbele kikuu cha Serikali kitaendelea kuwa kujenga uchumi wa viwanda ili kupanua fursa za ajira, kuboresha upatikanaji na ubora wa huduma za jamii (maji, afya, elimu) na kupunguza umasikini. Aidha Serikali itaendeleza mapambano dhidi ya rushwa na biashara haramu ya madawa ya kulevya, kuimarisha ulinzi wa rasilimali za umma na kudhibiti zaidi matumizi mabaya ya rasilimali zote za umma ikiwemo rasilimali fedha. Kwa upande wa mapato, Serikali inakusudia kuendelea kuchukua hatua zaidi kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani (kodi na maduhuli) ili kuongeza uwezo wa ndani wa kugharamia matumizi ya kawaida ya Serikali na miradi ya maendeleo na kupunguza utegemezi kwa wahisani.
Dhamira ya Serikali ya awamu ya tano ni kuibadili Tanzania na kuifanya kuwa kitovu na na nguvu kubwa ya kiuchumi katika ukanda huu wa bara la Afrika ndani ya kipindi cha miaka 8 ijayo. Lakini ili lengo hili litimie sharti WATANZANIA TUFANYE KAZI KWA NIDHAMU ya hali ya juu.
Mwisho kabisa, napenda nirudie kusisitiza kuwa, takwimu rasmi zinazotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu ndiyo takwimu sahihi. Wapo watu ambao wanavunja sheria na kutoa takwimu za kichochezi. Hawa watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria. Ninawasihi wana habari muache kuokotaokota takwimu za mitaani ambazo siyo sahihi. Yeyote atakayesambaza takwimu za uongo, ajue sheria itachukua mkondo wake. Epukeni kutumia vyanzo vya takwimu ambavyo siyo sahihi. Tanzania ni nchi ya pili barani Afrika kwa kuwa na takwimu bora zaidi na haya siyo maneno yangu bali yanatoka kwa wenzetu wa Benki ya Dunia na IMF ambao wamefanya utafiti wa kina na kuja na matokeo hayo.
NAWATAKIA WOTE HERI YA MWAKA MPYA 2018
ASANTENI KWA KUNISIKILIZA

0 comments: