Monday, 1 January 2018

Prof. Lipumba ataka Mjadala juu ya Hali ya Uchumi.

Mtaalamu wa Uchumi, Profesa Ibrahim Lipumba amesema kuna haja ya kuwa na mjadala wa kitaifa kuhusu uchumi na mustakabali wa Taifa.

Profesa Lipumba ameyasema hayo leo Jumapili Desemba 31,2017 wakati wa mahojiano na kituo cha televisheni cha Azam kujadili hali ya uchumi kwa mwaka 2017.

Amesema kuna haja ya kujadili sera za kiuchumi, namna ya kujenga uchumi unaoongeza ajira kwa wananchi na kutafuta suluhisho la matatizo yanayowakabili Watanzania.

“Tuitishe mjadala wa kitaifa tuje kujadili, tutazame upya sera za kiuchumi, namna ya kujenga uchumi unaoongeza ajira utakaoleta manufaa kwa wananchi wote. Tujadili kimsingi na tutoke na sera ambazo tunaweza kuishauri Serikali nini cha kufanya,” amesema Profesa Lipumba.

Katika mjadala huo, Profesa Lipumba amesema Serikali haiwezi kufanikisha mapinduzi ya viwanda kama haijafanikisha ya kilimo kwa sababu ukuaji wa kilimo ndiyo ukuaji wa sekta nyingine za kiuchumi.

Amesema robo tatu ya Watanzania wanategemea kilimo lakini ukuaji wa sekta hiyo ni mdogo kutokana na Serikali kukiacha nyuma kilimo na kukumbatia sekta nyingine.

Profesa Lipumba amesema kuna changamoto kubwa kwenye kilimo ambazo zinatokana na ukweli kwamba, Serikali haijawekeza vya kutosha kwenye utafiti wa kilimo, mafunzo kwa wakulima na usambazaji wa pembejeo.

“Tujifunze kwa nchi za Asia kama vile China, India na Malaysia, wao wamewekeza kwa wakulima wadogowadogo,” amesema Profesa Lipumba.

Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe aliyeshiriki mjadala huo, amesema mfumo wa elimu wa sasa wa Tanzania unamwandaa mtu kuwa tegemezi badala ya kujitegemea kama ilivyokuwa zamani.

Amesema kuna umuhimu wa kufumuliwa upya kwa mfumo huo tegemezi ili kujenga utakaowafanya vijana wajifunze kujitegemea au ujasiriamali.

Bashe amesema Tanzania ni nchi ya pili Afrika kwa idadi kubwa ya mifugo lakini hakuna dira ya wazi ni wapi pajengwe viwanda.

Akichangia mada ya hali ya uchumi, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala (KIU), Dk Bravious Kahyoza amesema Tanzania haijazalisha ajira za kutosha kwa wananchi kwa sababu ya kusinyaa kwa uchumi.

Amesema Serikali imekuwa ikishindana kukopa na sekta binafsi jambo lililosababisha sekta binafsi kubaki nyuma na kushindwa kuajiri watu wengi kwa sababu ya hali ngumu ya kiuchumi.

Ametaka kuwepo uwiano kati ya sera za kifedha na zile za kibajeti ili kuleta matokeo mazuri kwenye uchumi.

“Wataalamu wetu wanapaswa kukaa chini na kuangalia kama tuko kwenye njia sahihi kuelekea mpango wa maendeleo wa miaka mitano na uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025. Kama hatuko sahihi basi ni vyema tukabadilisha mbinu tunazotumia kufika huko,” amesema.

0 comments: