MAPATO kutokana na mauzo ya korosho katika msimu wa 2017/2018 katika mikoa minne ya Lindi, Mtwara, Pwani na Ruvuma yamepanda na kufikia sh. trilioni 1.08 ikilinganishwa na misimu miwili iliyopita.
Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Bw. Hassan Jarufu alitoa taarifa hiyo Jumapili, Desemba 31, 2017 wakati akitoa ufafanuzi juu ya uzalishaji na mauzo ya zao la korosho nchini hadi kufikia mwisho wa mwaka 2017.
“Ukiangalia msimu wa mwaka 2015/2016, utaona kuwa korosho zilizozalishwa zilikuwa kidogo zaidi. Msimu huo ziliuzwa kilo 155,244,645 zikiwa na thamani ya sh. 388,474,530,906.00 ikilinganisha na msimu wa 2016/2017 ambapo jumla ya kilo 265,237,845.00 ziliuzwa zikiwa na thamani ya sh. 871,462,989,284.00,” alisema.
Alisema katika minada 10 ya msimu wa 2017/2018, mauzo ya korosho yamefikia kilo 285,828,205 zenye thamani ya sh. 1,082,200,383,581.00. “Mnada wa 10 ulikuwa tarehe 21 Desemba, 2017 na minada bado inaendelea kwa msimu wa 2017/2018,” alisema.
Akitoa ufafanuzi wa mauzo hayo kwa kila mikoa hadi kufikia mnada wa 10, Bw. Jarufu alisema Mkoa wa Mtwara umeongoza kwa kuuza tani 178,165.741 zenye thamani ya sh. 701,674,466,366.00 ukifuatiwa na mkoa wa Lindi ambao umeuza tani 68,687.504 zenye thamani ya sh. 247,163,294,296.00.
“Mkoa wa Ruvuma umeuza tani 19,545.613 zenye thamani ya sh. 76,173,400,063.00 na mkoa wa Pwani umeuza tani 19,429.347 zenye thamani ya sh. 57,189,224,856.00 na kufanya mapato yote kwa mwaka huu kufikia sh. trilioni 1.082,” alisema.
Bw. Jarufu alitoa ufafanuzi huo mara baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuzindua kampeni ya kitaifa ya upandaji mikorosho bora na mipya milioni 10 kwa msimu wa 2017/2018 mjini Ruangwa, mkoani Lindi. Kaulimbiu ya kampeni hiyo ni: “Korosho ni dhahabu ya kijani, tuitunze, itutunze”.
Bw. Jarufu alimweleza Waziri Mkuu kwamba Bodi ya Korosho Tanzania kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Naliendele, Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri za wilaya, imeendelea kutekeleza mpango wa miaka mitatu wa kupanda mikorosho 10,000,000 kila mwaka.
“Katika mpango huu, wastani wa mikorosho 5,000 inatarajiwa kupandwa katika kila kijiji au mikorosho 30 kwa kaya kwa mwaka, sawa na ekari 330,000 kwa mwaka kwa nchi mzima. Lengo la mpango huu ni kuongeza kiasi cha korosho kinachozalishwa nchini kwa kuongeza wigo wa halmashauri zinazozalisha korosho na kupanda miche inayotokana na mbegu bora zenye uzalishaji mkubwa na zenye ukinzani dhidi ya magonjwa na wadudu,” alisema.
Alisema katika msimu wa 2017/2018, Bodi ya korosho inaratibu uzalishaji wa jumla ya miche 14,001,820 ambayo imetokana na tani 100 (kilo100, 000) zilizozalishwa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Naliendele.
“Mchanganuo wake ni kama ifuatavyo: kilo 31,170 za mbegu zitapandwa shambani moja kwa moja ambazo zitatoa jumla ya miche 2,181,900; kilo 68,830 zitazalisha jumla ya miche 11,819,920 kati ya miche hiyo isiyobebeshwa ni 9,636,200 na miche itakayobebeshwa ni 2,183,720.
“Ni matumaini yetu kuwa ifikapo mwishoni mwa mwezi Februari 2018, miche yote itakuwa tayari imezalishwa, kugawanywa na kupandwa katika mashamba ya wakulima,” aliongeza.
Mkurugenzi huyo alisema, katika msimu huu eneo la utekelezaji wa mradi limeongezeka kutoka Halmashauri 51 za msimu uliopita 2016/2017 hadi kufikia Halmashauri 90 nchi nzima ikiwemo mikoa mipya iliyothibitishwa kustawi zao la korosho hapa nchini.
Sherehe hizo zilihudhuriwa na wakuu wa mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Pwani na wajumbe wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT). Wakuu wa Wilaya, baadhi ya Wenyeviti wa Halmashauri na wataalamu kutoka kituo cha utafiti cha Naliendele walishiriki uzinduzi huo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
0 comments: