Polisi
Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imetembelea Mkoa wa Rufiji katika
utaratibu wa kawaida wa jeshi hilo wa kuimarisha ujirani mwema na
kubadilishana uzoefu.
Makamanda
wa polisi wa mikoa inayounda Kanda Maalumu ya Dar es Salaam wakiongozwa
na Kamanda wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa walifika Mkoa wa Kipolisi wa
Rufiji leo Jumanne Januari 2,2018 na kupokewa na kamanda wa mkoa huo,
Onesmo Lyanga.
Msafara
wa Kamanda Mambosasa ulibeba zawadi za sikukuu kwa ajili ya askari
ambao wapo katika operesheni maalumu katika eneo hilo ambalo siku za
nyuma liligubikwa na matukio ya mauaji ya wananchi wasio na hatia na
askari.
Akizungumza
na baadhi ya askari waliopo Rufiji, Kamanda Mambosasa amewapongeza kwa
kufanya kazi kwa uzalendo na kwa kufuata kiapo chao licha ya mazingira
ya kazi si rafiki.
"Hakuna
asiyejua hali iliyokuwepo Rufiji mpaka wananchi wakakata tamaa na
wengine walihama lakini kamanda mwenzangu ameniambia hali sasa ni
shwari, Dar es Salaam tuko pamoja na ninyi na tunathamini kazi
mnayoifanya. Usalama wa Dar es Salaam unategemea kwa kiasi kikubwa
usalama wa hapa pia," amesema Kamanda Mambosasa.
Amesema
hali ya usalama Dar es Salaam ni shwari na askari hawajalala wapo imara
kama walio kwenye operesheni hiyo kwa kuwa wahalifu wanaobanwa Pwani na
kukimbilia Dar es Salaam hawabaki salama.
"Hatukuja
Boxing day (siku ya kufungua zawadi) lakini leo tumewaletea ndafu,
kidogo, kilo 200 za mchele, sukari, maji na mafuta, ninyi endeleeni
kupeperusha bendera ya Jeshi la Polisi na haya mambo yatakwenda lakini
baadaye yataisha,” amesema.
Kwa
upande wake, Kamanda Lyanga amesema wamekuwa wakitembelewa na viongozi
na watu wengine wengi, hivyo morali ya askari waliopo katika operesheni
iko juu na wanafanya kazi kwa weledi na mpaka sasa hakuna malalamiko
yoyote ya wananchi jambo ambalo linaashiria kuwa sheria zinafuatwa.
"Baada
ya kuwa tumewafikia wahalifu sasa wananchi wanawapenda askari wao,
wanatoa taarifa hawaogopi tena kama zamani," amesema Kamanda Lyanga.
0 comments: