Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 04 Januari, 2018 amepokea barua kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni iliyowasilishwa na Mjumbe Maalum Mhe. Sam Kutesa ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda.
Pamoja na kupokea barua hiyo Mhe. Rais Magufuli amefanya mazungumzo na Mhe. Sam Kutesa, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Baada ya mazungumzo hayo Mhe. Sam Kutesa amesema Mhe. Rais Museveni amemtumia Mhe. Rais Magufuli na Watanzania wote salamu za heri ya mwaka mpya na pia wamezungumzia masuala yahusuyo uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda.
Mhe. Sam Kutesa amesema Uganda inafurahishwa na kuridhishwa na uhusiano na ushirikiano mzuri na wa kindugu uliopo kati yake na Tanzania na kwamba mazungumzo ya leo yalijikita kuuimarisha zaidi kwa manufaa ya wananchi wa nchi zote mbili.
“Tumezungumza namna tutakavyoimarisha na kukuza zaidi uhusiano wetu katika maeneo mbalimbali, kama unavyojua kuna miradi ya maendeleo ya ushirikiano ukiwemo mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga hapa Tanzania, na miradi mingine na masuala mbalimbali ya ushirikiano” amesema Mhe. Sam Kutesa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
04 Januari, 201
0 comments: