Hatima
ya mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi maarufu Sugu
anayeshtakiwa kwa kosa la kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John
Magufuli itajulikana kesho.
Sugu
na Katibu wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Masonga
wanakabiliwa na kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya ambayo
kesho Februari 26,2018 itatoa hukumu.
Washtakiwa
wanadaiwa kutenda kosa hilo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika
Desemba 30,2017 eneo la Uwanja wa Shule ya Msingi Mwenge jijini Mbeya.
Hakimu
Mkazi Mfawidhi, Michael Mteite anatarajiwa kutoa hukumu baada ya upande
wa mashtaka na ule wa utetezi kukamilisha ushahidi Februari 9,2018.
Jamhuri
iliwasilisha mashahidi watano na kielelezo kimoja cha sauti iliyodaiwa
kurekodiwa na shahidi wa tano, Inspekta Joram Magova.
Upande wa utetezi uliwasilisha mashahidi sita wakiwamo Sugu na Masonga waliokana kutamka maneno wanayoshtakiwa kuyatoa.
Washtakiwa
walitetewa na mawakili Sabina Yongo, Boniface Mwabukusi na Hekima
Mwasipu kabla ya kujitoa na sasa wanawakilishwa na Peter Kibatala.
Kwa
mara ya kwanza, Sugu na Masonga walifikishwa mahakamani Januari 16 na
kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali Mkuu, Joseph Pande aliyeeleza
upelelezi ulikuwa umekamilika na walikuwa tayari kuendelea na
usikilizaji.
0 comments: