Zikiwa
zimepita siku tatu tangu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es
Salaam iwahukumu kifungo cha mwaka mmoja jela wahamiaji haramu 77 kutoka
Ethiopia, wengine 83 wamedakwa mkoani Iringa huku dereva aliyekuwa
akiwasafirisha akifanikiwa kutoroka.
Wahamiaji hao walikamatwa wilayani Kilolo mkoani hapa wakiwa safarini kupelekwa Malawi kisha Afrika Kusini.
Hata hivyo katika harakati za kukamatwa kwao, dereva wa lori mali ya mkazi wa Tukuyu mkoani Mbeya alitoroka.
Raia
hao wa Ethiopia walikamatiwa katika Kijiji cha Mbigili ambapo Kamishna
Msaidizi Mwandamizi wa Uhamiaji Mkoa wa Iringa, Hope Kawawa alisema
walikamatwa juzi saa kumi na moja jioni karibu na bomba la mafuta la
Tazama.
Alisema
wahamiaji hao walipelekwa kituo cha polisi cha Lugalo na kwamba,
kukamatwa kwao kunatokana na taarifa iliyofikishwa Uhamiaji na wananchi.
Alisema
maofisa wa Uhamiaji kwa kushirikiana na polisi walipowakamata baadhi
yao waliwakuta hali zao ni mbaya kutokana na kukosa chakula kwa siku
tatu na pia kuathiriwa na joto kutokana na bodi la lori walilokuwa
wakisafiria kuwa la bati.
“Wahamiaji
hawa walikuwa wanasafiri kwenye lori mali ya mkazi wa Tukuyu mkoani
Mbeya, dereva alikimbia na hajapatikana lakini uchunguzi unaendelea,”
alisema.
Aliongeza kuwa wahamiaji hao watafikishwa mahakamani kesho kujibu mashtaka yanayowakabili.
“Naomba
niwaambie madalali wanaosafirisha hawa wahamiaji kuwa mkoa wa Iringa si
mahala salama kuwapitisha kwa kuwa tuko makini saa 24 na tukiwabaini
hatua kali zitachukuliwa dhidi yao,” alisema.
Alitoa
wito kwa wananchi kutoa taarifa pindi wanapohisi baadhi ya watu si raia
wa Tanzania na wanapowaona watu wasiowatambua. Mtanzania aliyekamatwa
akihusishwa na usafirishaji wa wahamiaji hao, Hassan Mwalusanjo alisema
hana anachofahamu.
Alisema
aliomba lifti katika gari hilo kutoka Tukuyu kwenda Dar es Salaam
kununua vifaa vya gari wakati gari hilo lilipokuwa likisafirisha ndizi.
Mwalusajo alisema baada ya kushusha ndizi eneo la Mabibo jijini Dar es
Salaam, dereva aliondoka na aliporeja alipanda kurejea Tukuyu.
Alisema walipofika Ilula alishuka kula ndipo dereva alipoondoka na gari na aliporejea alimuomba amsaidie kusafisha gari.
“Sielewi
chochote nilishangaa kuwekwa chini ya ulinzi baada ya dereva kuniambia
nimsaidie kusafisha gari ambako nilikuta makopo ya maji na mifuko ya
mikate,” alisema akiwa chini ya ulinzi.’’
0 comments: