Bunge
limeitaka serikali kuhakikisha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) anafanya ukaguzi wa kiuchunguzi na kiufanisi katika
mikataba yote inayohusu mradi wa Mlimani City na kuwasilisha ripoti
bungeni, baada ya kubaini dosari kubwa kwenye uendeshaji wa mradi huo.
Agizo hilo limetolewa ikiwa ni wiki mbili baada ya chombo hicho cha kutunga sheria kuukagua mradi huo jijini Dar es Salaam.
Katika
ukaguzi wake, Bunge liligundua mbia wa mradi huo unaokihusisha Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) amewekeza mtaji wa Dola za Kimarekani 75
(Sh. 150,000) kutoka mfukoni kwake.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Naghenjwa
Kaboyoka, ndiye alitoa agizo kwa CAG kukagua mradi huo alipowasilisha
bungeni mjini hapa jana taarifa ya shughuli za kamati yake kwa mwaka
2017.
Alisema
upungufu uliobainika katika mradi huo unainyima serikali mapato stahiki
na hivyo kuwa eneo mojawapo lenye matumizi mabaya ya fedha za umma.
Kaboyoka
alisema kamati yake imebaini dosari kutokana na mradi wa ujenzi wa
Mlimani City ulioanza Oktoba mosi, 2004 ukitakiwa kukamilika Septemba
mosi, 2006 kwa makubaliano ya mkodishwaji na mkodishaji, kwa maana ya
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Kampuni ya Mlimani Holding Limited
(MHL), kutokamilika mpaka sasa.
Alisema
uchambuzi wa kamati yake katika ripoti ya CAG pamoja na mahojiano na
uongozi wa UDSM, umebaini dosari kubwa katika usimamizi na uendeshaji wa
mradi huo, hali ambayo inaipa serikali hasara.
Alizitaja
dosari hizo kuwa ni pamoja na Dola 75 ambazo zilionyeshwa kama mtaji wa
MHL ambao ni kinyume cha Sheria ya Uwekezaji ya Mwaka 1977 inayoelekeza
kwamba, ili kibali cha uwekezaji kitolewe lazima mwekezaji awe na mtaji
wa kutosha.
Mbunge
huyo wa Same Mashariki (Chadema) alisema kamati yake pia imebaini
Turnstar Holding Limited ni miongoni mwa wanahisa wa MHL na anamiliki
hisa moja na kwamba kampuni hiyo imetoa mikopo kwa MHL jumla ya Dola za
Marekani 49,027,840.
"Kamati
ilipata mashaka kuhusu nia hiyo ya mbia huyu kwa kuwa MHL ana hisa 900
ambazo hazijauzwa na hivyo angenunua badala ya kukopesha. Kamati inaona
mbia huyu ana lengo lake la kujinufaisha zaidi kwa kutoa mikopo kwa vile
riba anayolipwa inatolewa kwenye mapato ghafi kabla ya kugawana faida,"
alisema.
Kaboyoka
pia alibainisha kuwa kwa miaka 13 tangu mkataba huo uingiwe, mradi wa
ujenzi wa hoteli ya nyota tatu yenye vyumba 100 bado haujaanza, kinyume
cha makubaliano, hivyo kuongeza gharama za kumalizika kwa mradi. Pia
mradi wa utengenezaji wa bustani ya wanyama na mimea (Botanical Garden)
uliopaswa kwenda sawia na hoteli hiyo haujatekelezwa.
Aliongeza
kuwa kumekuwapo ukiukwaji wa malipo ya pango la ardhi ya chuo ambapo
vifungu cha 1.1(j) na 10.1 vya mkataba vinaeleza kuwa UDSM itapata
asilimia 10 ya pango la mapato ghafi, lakini MHL imekuwa ikifanya malipo
ya pango kwa chuo baada ya kutoa gharama za uendeshaji, hivyo
kuikosesha serikali mapato stahiki kinyume cha mkataba.
Pia
alisema wamebaini kukiukwa kwa kifungu cha 12.2(l) cha hati ya
makubaliano ya mpangaji kinachomtaka MHL kutopangisha mtu yeyote ambaye
hajathibitishwa na mpangishaji (UDSM).
Alisema
ukaguzi wao umethibitisha kuwa MHL amekuwa akipangisha wapangaji
wengine bila kupata kibali cha chuo hivyo kusababisha chuo kukosa
taarifa sahihi za mapato ya kodi kutoka kwa wapangaji wake.
Kaboyoka
alisema kamati hairidhishwi na mazungumzo yanayoendelea kati ya UDSM na
MHL kwa kuwa mwekezaji huyo amekuwa akiyakataa mapendekezo yote yenye
maslahi kwa pande zote mbili badala yake amekuwa akishikilia mapendekezo
yenye maslahi kwake tu.
"Wakati huo MHL ameongeza eneo la maduka na maegesho ya magari ambayo hayakuwamo katika mkataba.
Kama
hiyo haitoshi, mwekezaji ameshindwa kuanza utekelezaji wa ujenzi wa
hoteli na Botanical Garden ambavyo vipo kwa mujibu wa mkataba," Kaboyoka
alisema.
Kigogo
wa PAC huyo alisema mapitio ya mkataba yamebainisha kuwa hauelezi hali
ya ugawanaji mali pindi mkataba utakapomalizika (miaka 50 au 85) kwa
kuwa hakuna makubaliano rasmi yanayoeleza mgawanyo wa mali na
miundombinu itakayokuwapo pindi mkataba utakapoisha.
Alibainisha
kuwa athari ya jambo hilo ni kuwa kuna uwezekano mkubwa kutokea mvutano
wa kisheria pindi mkataba huo utakapofika ukomo.
Kaboyoka
alisema dosari nyingine ni kuhusu ushiriki wa serikali kupitia Kituo
cha Uwekezaji (TIC) ambapo kituo hicho na MHL wamekuwa wakibadilisha
muda wa utekelezaji wa mradi mara kwa mara kwa kumwongeza mwekezaji muda
wa kukamilisha mradi bila kukihusisha chuo.
"Kwa
mfano, mkataba wa kwanza ulisainiwa Februari 27, 2006 na kumwongeza
mwekezaji kipindi cha utekelezaji wa mradi hadi Oktoba 30, 2009. Mkataba
wa pili ulisainiwa Julai 13, 2007 kwa kuongeza muda wa utekelezaji hadi
Novemba 30, 2013 na mkataba wa tatu ulisainiwa Desemba 10, 2014 ambao
uliongeza muda wa utekelezaji wa mradi huo hadi Desemba 31, 2019," alisema.
Kaboyoka
pia alisema mkataba unaonyesha kuwa zilitakiwa kujengwa nyumba 50 za
kuishi (house estate/villas) lakini kamati yake ilipotembelea mradi huo
zilizonekana nyumba 45 na nyumba moja yenye vyumba viwili
vilivyotenganishwa na milango miwili.
Kutokana
na dosari hizo, Kaboyoka alisema mradi wa Mlimani City unapaswa
uangaliwe kwa kina kuanzia mkataba wa kwanza hadi hapo ulipofika sasa.
0 comments: