KIPA chaguo la kwanza wa Simba, Aishi Manula amekabidhiwa tuzo ya
Mchezaji Bora wa mwezi wa Wekundu wa Msimbazi katika sherehe fupi
iliyofanyika juzi nyumbani kwa Balozi wa Uturuki, Ali Davotuglu.
Manula, ambaye pia ni kipa chaguo la kwanza la timu ya Taifa (Taifa
Stars) alishinda tuzo hiyo baada ya kuonyesha kiwango kizuri katika
mechi nne zilizopita za ligi hiyo inayotarajiwa kuingia kwenye raundi ya
pili kuanzia leo.
Mbali na Manula, wachezaji wengine waliopata tuzo katika sherehe hiyo
pamoja na nahodha na mshambuliaji aliye kwenye kiwango cha juu, John
Bocco na kiungo, Said Ndemla.
"Hizi ni tuzo ambazo zinatolewa na klabu yetu katika kuhamasisha
wachezaji wafanye vizuri katika kila mechi wanayocheza na vile vile
kusaidia kuipa timu ushindi," alisema Mkuu wa Idara ya Habari na
Mawasiliano wa klabu hiyo, Haji Manara.
Aliongeza kuwa katika hafla hiyo ambayo ilihudhuriwa na viongozi wa
klabu hiyo pamoja na mwekezaji na bilionea, Mohamed Dewji "Mo",
walifanya mazungumzo mbalimbali na kubadilishana mawazo ili kuifanya
timu ifikie malengo yake msimu huu.
"Tunaamini hatua hii tuliyofika, itakuwa na matokeo chanya kwa sababu tutaimarisha mahusiano," Manara aliongeza.
0 comments: