Friday, 2 February 2018

Wakili: Afya ya Rugemarila, Seth zinatia mashaka

MAHAKAMA  ya Hakimu Mkazi Kisutu imeelezwa kuwa afya ya mmiliki wa IPTL, Harbinder Singh Sethi na mfanyabiashara James Rugemarila zinaendelea kuwa za mashaka.


Hayo yameelezwa leo mapema na Wakili wa utetezi, Respicius Didas baada ya Mwendesha Mashtaka kutoka Taasisi ya kizuia na kupambana na Rushwa (Takukuru) Leornad Swai kudai kuwa upelelezi katika  kesi hiyo bado haujakamilika.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shahidi Wakili Swai ameomba kesi hiyo iahirishwe na kwamba walienda Magereza kuchukua maelezo ya Seth lakini ilishindika kwa sababu afya yake haikuwa nzuri.

Kutokana na taarifa hiyo, Wakili Didas alidai kuwa wakati afya za washtakiwa zikiendelea kuwa za mashaka wanauomba upande wa mashtaka ukamilishe upelelezi.

Amesema ni vema kila kesi hii inapoahirishwa baada ya siku 14 kuwe na kitu kipya kuhusu hatua zilizochukuliwa, lakini inavyoonekana upande wa mashtaka unachukulia kawaida kuahirishwa kwa kesi hiyo.

"Upande wa mashtaka unacheza na mamlaka, utambue hali za washtakiwa ni mbaya, hivyo ukamilishe upelelezi" amesema Wakili Didas.

Swai alidai, Serikali inajitahidi kuangalia afya za washtakiwa kwani hata mara ya mwisho Serikali ilizungumzia afya ya Seth ambaye alidai anataka madaktari wake wawepo wakati akifanyiwa upasuaji.

Kuhusu upelelezi, Swai amedai ni kweli unachukua muda mrefu ila upo katika hatua za mwisho na kitu kinachochelewesha ni upelelezi mwingine kuwa nje ya nchi (Malysia)

Mshtakiwa Rugemarila aliieleza Mahakama kuwa hajawahi kupelekwa Hospital ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya matibabu, pia anahisi ana Cancer kwa sababu ya uvimbe alionao, pia Swai amesema daktari wake alisema hana cancer, "anabahati amefiwa angekuja Mahakamani kusema kwamba nina cancer,"

Hakimu Shaidi amesema Mahakama hiyo haina mamlaka ya kutoa amri wakatibiwe nje ya nchi na alishatoa amri kwamba watibiwe Muhimbili na kama inahitajika wakatibiwe nje ya nchi serikali ndio itasimamia.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Februari 16, mwaka huu

Kwa pamoja washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi, utakatisha fedha na kuisababisha Serikali hasara ya USD 22, 198,544.60 na Sh.Bil 309.

0 comments: