Katika
uwanja wa ndege wa Mwanza Mhe. Rais Magufuli amepokelewa na Mkuu wa
Mkoa wa Mwanza Bw. John Mongella aliyeongozana na Naibu Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula na Mwenyekiti wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Antony Dialo.
Akiwa
uwanjani hapo Mhe. Rais Magufuli amezungumza na wafanyakazi wa uwanja
wa ndege wa Mwanza ambao wamemuomba asaidie kutatua changamoto
mbalimbali zinazoukabili uwanja huo zikiwemo mahitaji ya jengo la abiria
kutokana na jengo lililopo kuwa dogo, mahitaji ya ujenzi wa uzio wa
kuzunguka uwanja na ndege zinazobeba minofu ya samaki kutotumia uwanja
wa Mwanza na badala yake kutumia viwanja vya nchi jirani kutokana na
ongezeko la tozo ya kodi kwa ndege hizo.
Katika
majibu yake Mhe. Rais Magufuli ameahidi kuwa Serikali itafanyia kazi
mahitaji ya kujengwa kwa jengo la abiria pamoja na ujenzi wa uzio ili
uwanja wa Mwanza uwe na hadhi ya kimataifa na hivyo kuiwezesha nchi
kupata mapato zaidi.
Kuhusu
changamoto ya ndege za kubeba minofu ya samaki kutotumia uwanja wa
Mwanza Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali itafanyia kazi jambo hilo na
kulitafutia ufumbuzi haraka ili ndege hizo zitumie uwanja huo na
kuiingizia nchi mapato.
Aidha,
Mhe. Rais Magufuli amesema anasubiri ripoti ya Wizara ya Ardhi kuhusu
wananchi waliovamia uwanja wa ndege wa Mwanza lakini amebainisha kuwa
Serikali haiwezi kukimbilia kuondoa kaya zaidi ya 1,900 zinazodaiwa
kuvamia eneo hilo na badala yake itaangalia njia bora ya kufanya.
Hata hivyo ametaka wananchi waliopo katika eneo hilo wasiendeleze makazi yao wakati uamuzi wa Serikali unasubiriwa.
“Bahati nzuri Naibu Waziri wa Ardhi upo hapa, kafanyieni kazi changamoto hii na mnipe ripoti” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Baada ya kutoka uwanja wa ndege wa Mwanza Mhe. Rais Magufuli ameelekea nyumbani kwake Chato Mkoani Geita kwa mapumziko.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Mwanza
24 Februari, 2018
0 comments: