Wednesday, 17 January 2018

Wanaotuhumiwa Kujiunganishia Bomba La Mafuta Wafikishwa Mahakamani

Watu saba akiwemo aliyekuwa fundi wa bomba la mafuta la Tazama, Samwel Nyakirang'ani (63) wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka saba ya uhujumu uchumi kwa kujiunganishia bomba la mafuta.

Nyakirang'ani anashtakiwa pamoja na Mwalimu wa Shule ya Msingi ya Ufukoni, Nyangi Matoro (54), Mfanyabiashara Farijia Ahmed (39), Malaki Mathias (39), Kristomsi Angelusi(25), Henry Fredrick (38) na fundi ujenzi Pamfili Nkoronko(40).

Washtakiwa walisomewa mashtaka yao jana mahakamani hapo na Wakili wa Serikali  Tulumanywa Majigo akisaidiana na Wakili wa Serikali Mkuu Peter Maugo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu,Thomas Simba.Wanadaiwa kutenda makosa yanayowakabili chini ya sheria ya uhujumu uchumi.

Akiwasomea hati ya mashtaka, Wakili Majigo alidai kuwa kosa la kwanza ni kujiunganishia isivyo halali katika bomba la mafuta ya Dizeli.

Imedaiwa, washtakiwa wote  katika tarehe tofauti kati ya mwaka 2015 na Januari 8, mwaka huu, huko maeneo ya Tungi Muungano katika Wilaya ya  Kigamboni jijini Dar es Salaam walijiunganishia bomba la upana wa inchi moja kwenye bomba la inchi 24 la  diesel material yasiyoshika kutu bila kuwa na kibali cha Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).

Katika shtaka jingine la kuharibu miundombinu ( kifaa kinachotumika kwa ajili ya utoaji huduma muhimu)  imedaiwa katika tarehe na maeneo hayo hayo, washtakiwa kwa pamoja walitoboa na kuharibu bomba la Inchi 24 linalotumika kusambaza mafuta ya Dizeli mali ya TPA.

Washtakiwa hao wanadaiwa pia kuwa, kati ya 2015 na January 8, 2018 maeneo ya Tungi Kigamboni, walitoboa bomba la inchi 28 la mafuta linalotumika kwa ajili ya usambazaji wa  Crude Oil likiwa ni mali ya TPA.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Wakili Majigo alidai Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) amewasilisha hati ya kuzuia dhamana kwa washtakiwa hao.

Washtakiwa hawaruhusiwi kujibu lolote kwa kuwa kesi inayowakabili ni ya uhujumu Uchumi ma imeahirishwa hadi Januari 30,2018. Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, upelelezi bado haujakamilika, washtakiwa walirudishwa rumande.
Je, Jose Mourinho Ataongezewa Mkataba??

Klabu ya Manchester United inakaribia kufikia makubaliano na kocha wake Jose Mourinho wa kuongeza mkataba mpya.

Mazungumzo kati ya pande hizo mbili yanaendelea vyema na ni suala la muda tu kabla ya Mourinho hajaongeza mkataba mpya klabuni hapo na mkataba wake wa sasa unafikia ukingoni mwaka 2019.

Taarifa za ndani ya klabu zinaeleza kuwa kama kocha huyo atasaini mkataba mpya utamuweka klabuni hapo mpaka mwaka 2021.

Licha ya kulaumiwa na wachambuzi wengi wa soka pamoja na washabiki wa klabu ya Man kuwa timu hiyo inacheza mchezo wa kujilinda bado viongozi wa United wanaona kuwa Mourinho anaweza ibeba timu hiyo katika kuipa mataji makubwa barani ulaya.

Mourinho alijiunga na United mwaka 2016 kuchukua mikoba ya Luis Van Gaal, ameisadia Man United kutwaa ubingwa mwa kombe la Europa na Lile la EfL Carabao.
Anthony Joshua Ampuuza Joseph Parker

Antony Joshua mwanamasumbwi nguli mtajika kwa sasa, amepuuilizilia mbali kwa kicheko cha mfa maji haishi kutapa tapa baada ya madai ya utumizi wa dawa za kuongeza nguvu yaliyotolewa na bondia mwenziwe Joseph Parker na kumbatiza jina la mfalme wa utumizi wa dawa za kuongeza nguvu.

Haya yanatukia kukitarajiwa pambano baina ya mabondia nguli na mashuhuri Joshua na Parker, pambano linalotarajiwa mwishoni mwa mwezi wa tatu mwaka huu, hii ni mara ya kwanza katika historia kwa mabondia hawa wenye uzito wa juu duniani kukutana nchini Uingereza.

Joshua ana umri wa miaka 28, akiwa na umri huo tayari anashikilia mikanda miwili ya IBF na WBA wakati bondia mwenziwe kutoka New Zealand Parker ni bingwa wa WBO.

Joshua anasema ameshasikia maneno mengi mabaya mno dhidi yangu kiasi hakuna jipya tena, ninajua rekodi zangu, ndiyo maana sijishughulishi na tambo zisizo na tija.
Joshua aliongeza kuwasema kuwa maneno ya kashfa yapo tele kwenye ndondi sasa kama ni jambo la kawaida hupaswi kuayatumia kama zana za kuuzia pambano.

Shutuma za Parker alizivurumisha wakati alipokuwa akihojiwa na redio moja nchini New Zealand baada ya kuthibitishwa kwa tarehe ya pambano.

Hata hivyo, wakati alipokuwa akizungumza na BBC redio 5 mapema wiki hii, Parker alikubali alizungumza maneno yasikyokuwa na maana yoyote, sidhani kama anauraibu huo.

Joshua ambaye anatuhumiwa , naye alipokuwa na mahojiano na BBC katika kipindi cha Graham Norton mwishoni mwa wiki iliyopita alimwita mpinzani wake mfalme wa pai.

Mabondia wote hawa wawili wanatarajiwa kupanda ulingoni kutetea rekodi ya kutopigwa, ikumbukwe kwamba michuano ya Olimpiki ya mwaka 2012 bondia Joshua alishinda michuano yote 20.
Kambi ya mpinzani wake Parker inajiandaa kwa kumpa mbinu za kushambulia kidevu dhaifu cha Joshua kwa kutumia mbinu ya Wladimir Klitschko mwaka jana kama ushahidi kabla Yoshua alipotetea hadhi yake tena kuwa bingwa wa dunia wa WBA katika uwanja wa Wembley.

Kama mara tatu niliumizwa ama kusita kwenye pambano anasema Joshua,wakati alipokuwa na mkutano na waandishi habari na kusema kuwa amejifunza kupitia matatizo na dhoruba na kujinasibu kuwa hakuna binaadamu yeyote ulimwenguni atakaye sitisha safari yangu.
Parker hajawahi kushindwa katika mapambano yake 24 ya kimataifa ulingoni yakiwemo 18 aliyoshinda kwa KO.Anavimba kwa kusema kuwa amekuwa akimuangalia Joshua kwa muda mrefu sana. Najua uwezo wake, na yeye ananijua pia. Naujua udhaifu wake naye anadhani anaujua udhaifu wangu

Naamini nitalenga kidevu chake na kumtoa kwenye pambano kwa KO.
RONALDINHO astaafu kucheza Soka.

Nyota wa zamani wa timu ya taifa ya Brazil na vilabu vya Psg, Barcelona na Ac Milan Ronaldo de Assis Moreira Maarufu kama Ronadinho Gaucho amestaafu soka.

Licha ya Ronadinho kutocheza soka la kiushindani toka mwaka 2015 amekua akicheza michezo ya mabonanza

Kaka na wakala wa mchezaji huyo Roberto Assis amethibitisha kuwa umefika mwisho kwa fundi huyo wa kibrazil kucheza soka.

Ronaldinho alianzia soka lake katika klabu ya Gremio ya nchini kwao kabla ya kujiunga na Paris St-Germain mwaka 2001 na baadae kujiunga na Barcelona alikongara sana.

Katika msimu wa 2010 -2011 alijiunga na Ac Milan ya Italia kabla ya kurudi kwao na kujiunga na Flamengo mwaka 2011. Kisha alichezea vilabu vya Atletico Mineiro, na Queretaro ya nchini Mexico na kurudi tena kwao Brazil katika klabu ya Fluminense.
Utafiti: Mbwana Samatta, Salim Kikeke wana ushawishi mkubwa Tanzania
Mchezaji wa soka kutoka Tanzania Mbwana Samatta amechaguliwa kuwa kijana mwenye ushawishi mkubwa nchini Tanzania kulingana na kura ya maoni iliofanywa na chombo cha habari cha Avance media.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 25 anaichezea klabu ya Genk na timu ya taifa ya soka nchini humo taifa Stars.

Nahodha huyo wa Tanzania alishinda tuzo ya mchezaji bora wa shirikisho la soka barani Afrika Caf miongoni mwa wachezaji wanaosakata kandanda barani Afrika 2016 baada ya kuisaidia timu yake ya TP Mazembe kushinda kombe la ligi ya Afrika.
Naye mtangazaji wa habari wa BBC Swahili Salim Kikeke alikuwa wa saba katika kura hiyo akimshinda msanii wa bongo fleva Diamond Platinumz.
Matokeo ya kura hiyo nchini Ghana na Nigeria yalitolewa mapema mwaka huu.
Mchezaji Victor Moses alichaguliwa kuwa mtu mwenye ushawishi mkubwa huku wakili wa rais wa Ghana Kow Essuman akichaguliwa mtu mwenye ushawishi mkubwa nchini humo.

Tazama orodha kamili ya vijana walio na ushawishi mkubwa Tanzania:


MAREKANI YASITISHA MSAADA WA FEDHA KWA WAPALESTINA.
Utawala wa Rais Donald wa Marekani umesitisha zaidi ya nusu ya fedha zake ilizokuwa ikizitoa kwa Shirika la Umoja wa Mataifa linalosaidia Wapalestina.

Marekani imesema itatuma kiasi cha dola milioni 60 ya malipo yake ya kwanza ya mwaka huu, lakini itazuia dola milioni 65 kwa kile ilichosema ''..kufikiria mustakabali ujao''.

Maafisa wa Marekani wamesema shirika hilo la Umoja wa Mataifa linahitaji kufanyiwa tena tathmini.

Washngton imekuwa ikitoa karibu asilimia 30 ya bajeti yake, kutoa huduma za afya, elimu na huduma za jamii.

Awali Rais Donald Trump alisema nchi yake itakata msaada iwapo Wapalestina wanapinga juhudi za amani na Israel.

Kwa upande wake Afisa mmoja wa Umoja wa Mataifa amesema hatua hiyo ita haribu matokeo mazuri ya maelfu ya Wapalestina wasio na maisha bora yenye usalama.
Naye Afisa wa Palestina Wasel Abu Youssef amesema uamuzi huo unathibitisha kwamba Marekani inaendelea kuangamiza haki za Wapalestina.

Hata hivyo msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani amesema uamuzi huo haukukusudia kumuadhabisha yeyote yule.

Jumapili iliyopita Rais wa Wapalestina, Mahmoud Abbas alimshutumu Rais Trump na kwa kuvuruga juhudi za kupayikana kwa amani Mashariki ya kati, Amesema kwamba hatakubali mpango wowote wa amani kutoka Marekani baada ya nchi hiyo kuutambua mji wa Jerusalem kama mji mkuu wa Israel.

Ameilaumu Israel kwa kuuweka penmbeni mkataba wa Oslo wa mwaka 1994, ambao ndio ulianzisha mpango huo wa kupatikana kwa amani.
Daktari wa White House asema afya ya akili ya Trump ni nzuri
Rais Trump hajaonyesha dalili zozote za matatizo ya kiakili kufuatia uchunguzi wa kiafya na yuko la afya nzuri, daktari wa White House amesema.

"Sina wasi wasi wowote kuhusu afya ya akili ya Trump," Ronny Jackson alisema Jumanne.

Wiki iliyopita Trump alifanyiwa uchunguzi wa afya wa saa tatu, ambao ni wake wa kwanza tangu awe rais wa Marekani.
Hii ni baada ya kutolewa kitabu chenye utata kulichoeneza uvumi kuhusu afya ya kiakili ya Rais Trump.

Akiongea na waandishi wa habari wakati wa mkutano huko White House, Dkt Jackson alisema kuwa kwa jumla afya ya rais ni nzuiri.

"Anaendelea kufurahia moyo wenye afya na afya yote kwa jumla kutokana na kutovuta sigara na kutokunywa pombe," aliongzea.
Hata hivyo Dkt Jakcson alisema kuwa Bw Trump, 71, atanufaika kwa kupunguza vyakula vyenye mafuta na mazoezi zaidi.

Siku ya Ijumaa rais alichunguzwa na madaktari wa kijeshi katika kituoa cha afya cha Walter Reed huko Bethesda, Maryland katika uchunguzi uliotajwa kuwa uliofanikiwa.
Kulingana na Michael Wolf ambaye ni mwandishi wa kitabu cha Fire and Fury: Inside the Trump White House, ni kuwa wafanyakazi wote wa White House walimuona Trump kama mtoto.

Trump alijibu kwa kusema kwa kitabu hicho kimejaa uongo huku naye waziri wa mashauri ya nchi za kigeni akikana madai kuwa afya ya rais ilikuwa inafeli.