Monday, 26 March 2018

Watu 37 wafariki katika mkasa wa moto jumba la Kemerovo, Urusi

Watu 37 wamethibitishwa kufariki baada ya moto kuzuka katika jumba moja kubwa la kibiashara katika mji maarufu kwa uchimbaji wa mkaa wa mawe wa Kemerovo, eneo la Siberia nchini urusi.

Watu zaidi ya 64 hawajulikani walipo, wakiwemo watoto 41.

Baadhi ya maeneo ya jumba hilo kubwa yanadaiwa kuwa kwenye hatari ya kuporomoka.

Moto huo ulianza katika ghorofa ya juu katika jumba Winter Cherry.

Inadaiwa wengi wa waliofariki walikuwa kwenye kumbi za sinema.

Video zilizopakiwa mitandao ya kijamii zinawaonesha watu wakiruka nje kupitia madirisha kujaribu kujinusuru kutoka kwa moto huo uliozuka Jumapili.

Wazima moto zaidi ya 660 wametumwa kusaidia juhudi za uokoaji.

Chanzo cha moto huo hakijabainika lakini maafisa wameanzisha uchunguzi.

Kemerovo, ni eneo maarufu sana kwa uchimbaji wa mkaa wa mawe.

Ni mji unaopatikana takriban kilomita 3,600 mashariki mwa mji mkuu Moscow.

Kansela wa Austria Sebastian Kurz ametuma salamu zake za rambirambi kwa jamaa na marafiki wa waathiriwa, sawa na Waziri wa mambo ya nje wa Latvia Edgars Rinkēvičs.
 

0 comments: