Mamilioni ya watu waliandamana katika miji mbalimbali ulimwenguni kote siku ya Jumamosi kushinikiza mageuzi katika sheria zinzohusu umiliki wa bunduki.
Kilele cha maandamano hayo yaliyopewa jina la March for our lives, ulikuwa ni mkutano uliohudhuriwa na takriban watu nusu milioni katika mji mkuu wa Marekani, Washington DC.
Maandamano hayo yalipangwa na shule ya upili ya Marjorie Stoneman Douglas mjini Parkland, jimbo la Florida, ambako watu wapatao 17, wakiwemo wanafunzi 14 walipoteza maisha yao kufuatia shambulizi la bunduki kwenye shule hiyo mapema mwaka huu.
Zaidi ya maandamano 800 yalikuwa yamepangwa kufanyika katika miji kadhaa ya Marekani na sehemu nyingine duniani kote, sambamba na yale ya mjini Washington DC.
Mashambulizi ya kutumia bunduki zenye nguvu, hususan kwenye shule Marekani yamezua mjadala mkali, huku wanasiasa wakitofautiana kuhusu hatua za kudhibiti matukio hayo.
Wanaharakati na wasanii maarufu walihudhuria maandamano hayo, wakiwemo wanamuziki Jennifer Hudson, Ariana Grande, Demi Lovato na Miley Cyrus.
Mjukuu wa mtetezi maarufu wa haki za binadamu Martin Luther King Jr, alishangiliwa kwa shangwe na vigelegele aliposimama kuhutubia mkutano wa Washington. Yolanda Renee King III alisema kizazi cha sasa ndicho kitaleta mabadiliko yanayohitajika.
"Na itoshe! Na itoshe!" alisema msichana huyo.
Kundi kubwa la waandamanaji baadaye lilionekana nje ya ikulu likibeba mabango licha ya kuwa rais Donald Trump hakuwemo wakati huo. Baadaye waliyaweka mabango yao chini na kuyaacha nje ya uzio wa ikulu kama ishara kwamba walitaka rais Trump asome ujumbe wao.
0 comments: