Wednesday 11 April 2018

Tuesday 10 April 2018

UJUE UMUHIMU WA KUNYWA MAJI MENGI KILA SIKU


Unashauriwa kunywa maji zaidi lita 2 hadi 5 kila siku ili kuepuka mawe kutengenezeka kwenye figo zako. Maji ndio husafisha seli na kuondoa sumu na kemikali zinazojitengeneza mwilini kuwa mawe.

Wanawake ndio waathirika wakubwa wa tatizo hili maana miili yao ina joto kubwa hivyo maji hukaushwa kwenye figo na mawe haya hutengenezeka kirahisi wasipokunywa maji ya kutosha.

Magonjwa ya figo yanakadiriwa kuwaathiri takribani wanawake milioni 195 duniani kote na yanashika nafasi ya 8 kama chanzo cha vifo vya wanawake duniani.

Inakadiriwa kuwa wanawake 600,000 hupoteza maisha kutokana na matatizo ya figo duniani kote kila mwaka.

Nakutakia mazingatio katika hili
Share kwa wote uwapendao...

Monday 9 April 2018

TUCTA Nao Wataka Watumishi Darasa la 7 Warudishwe Kazini
Baraza Kuu la Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) jana Jumamosi Aprili 7, 2018 limetoa tamko lenye mambo saba, likiwemo la kupinga uamuzi wa Serikali kuwafuta kazi watumishi wake wenye elimu ya darasa la saba.

Akisoma tamko hilo mbele ya wajumbe wa baraza kuu la Tucta katika mkutano wa baraza hilo uliofanyika mkoani Morogoro mwenyekiti wa Tucta, Tumaini Nyamhokya alisema uamuzi huo wa Serikali si sahihi na hivyo wametaka watumishi hao kurejeshwa kazini.

Alisema baraza limesikitishwa na uamuzi wa kuwaondoa kazini watumishi wa umma na taasisi zinazopokea ruzuku kutoka serikalini.

Nyamhokya alisema uamuzi huo si wa kisheria ikizingatiwa kuwa watumishi hao waliajiriwa kwa kufuata taratibu halali za ajira.

“Kwa hiyo Tucta tunaitaka serikali kutengua uamuzi wake na kuwarudisha watumishi hao kazini bila kupoteza haki zao za kiutumishi kwa kipindi chote,” alisema.

Mambo mengine sita yaliyopo katika tamko hilo wanayotaka yafanyiwe kazi ni; ongezeko la mishahara, kodi ya mishahara (PAYE), kupandishwa madaraja na vyeo kwa watumishi wa umma, malimbikizo ya mishahara kwa wafanyakazi na watumishi kwa baadhi ya taasisi, ucheleweshwaji wa malipo ya wastaafu kwa baadhi ya mifuko ya hifadhi ya jamii na uamuzi wa Serikali kuunganisha mifuko ya hifadhi ya jamii.
AFCON 2018,Tanzania yatupwa nje
Timu ya taifa ya soka ya wanawake Twiga Stars imetupwa nje ya mashindano ya kuwania kufuzu fainali za AFCON 2018 kwa wanawake baada kutoa sare ya 1-1 ugenini dhidi ya Zambia.

Katika mchezo uliomalizika jioni hii Twiga imejitahidi kuzuia kufungwa lakini imeponzwa na sare ya 3-3 ambayo ilipatikana kwenye mchezo wa kwanza uliopigwa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam Jumanne iliyopita.

Zambia sasa imesonga mbele ambapo imebakiza mchezo mmoja itacheza na mshindi kati ya Namibia na Zimbabwe na endapo itashinda basi itakuwa imekata tiketi ya kucheza fainali hizo zitakazofanyika nchini Ghana.

Twiga Stars itarejea nyumbani kujipanga tena katika awamu nyingine na michuano mingine. Tanzania sasa inawakilishwa na Ngorongoro Heroes pekee ambayo inasubiri kucheza na DR Congo kwenye mchezo wa marudiano baada ya kutoka 0-0 kwenye mechi ya kwanza.
Waziri Mkuu Awataka Mabalozi Kutangaza Vivutio Vya Uwekezaji Vilivyopo Nchini
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nchini Urusi na Rwanda kutumia fursa hiyo kwa kutangaza vivutio vilivyopo nchini ili kuwavutia wawekezaji kuja kuwekeza kwenye sekta mbalimbali ikiwemo ya utalii.

Pia amewataka Mabalozi kila mwisho wa mwaka wajifanyie tathmini ya mafanikio waliyoyapata kutokana na uwakilishi wao katika Mataifa ambayo  ni kwa kiasi gani wamechangia kwenye uboreshaji wa maendeleo ya Taifa.

Ametoa maagizo hayo leo (Jumapili, Aprili 8, 2018) wakati akizungumza na Balozi Ernest Mangu anayewakilisha Tanzania nchini Rwanda na Balozi Simon Mumwi anayewakilisha Tazania nchini Urusi, katika ofisi ya Waziri Mkuu mjini Dodoma.

Waziri Mkuu amesema Tanzania ina vivutio vingi vya utalii ikiwa ni pamoja na uwepo wa mbunga za wanyama, hivyo ni vyema wanapoondoka wachukue nyaraka zote zitakazowasaidia katika kutangaza vivutio vya utalii ili kuongeza idadi ya watalii nchini.

Amesema mbali na kutangaza sekta ya utalii, pia watafute wawekezaji kwa ajili ya kuwekeza kwenye sekta nyingine kama vile madini, viwanda na kutafuta masoko ili wafanyabiashara na wakulima wa Tanzania waweze kuuza bidhaa zao nje ya nchi.

“Pia mkajifunze mbinu ambazo wenzetu wanazitumia katika kuboresha sekta mbalimbali ambazo na sisi tunazo hapa nchini kama za viwanda na kisha mje mtueleze namna ya kuziboresha. Kujifunza ni jambo zuri hivyo msisite kufanya hivyo huko muendako.”

Pia Waziri Mkuu amewataka mabalozi hao wakawatambue na kuwaunganisha Watanzania waishio kwenye nchi wanazoiwakilisha ili nao washiriki kwenye ujenzi wa uchumi wa viwanda na wawasisitize wafuate sheria za nchi wanazoishi na wakumbuke nyumbani.

Waziri Mkuu amewasisitiza mabalozi hao kwenda kupunguza gharama za uendeshaji wa Balozi kwa kuzuia matumizi katika mambo yasiyo ya lazima. “Pia maslahi ya nchi lazima mkayasimamie huko muendako hasa katika masuala ya kiuchumi.

Kwa upande wao mabalozi hao  wamesema watahakikisha wanayafanyia kazi maelekezo yote waliyopewa ikiwa ni pamoja na kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na nchi wanazoziwakilisha.

 (mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,

Monday 26 March 2018

Mo Salah kuongezewa mkataba Liverpool
Uongozi wa klabu ya Liverpool upo kwenye mipango ya kumuongezea mkataba mwingine Mshambuliaji wake kutoka Misri, Mohamed Salah.

Taarifa zinaeleza kuwa Liverpool itakuwa inamlipa mchezaji huyo kasi cha paundi £200,000 kwa wiki na kuzima ndoto za Real Madrid kumpata nyota huyo.

Salah amesema anafurahia zaidi kuchezea soka lake katika Ligi ya England sababu inaendana na aina ya uchezaji wake.

"Naipenda EPL sababu inaendana na aina ya uchezaji wangu, napenda kucheza hapa" alisema.

Real Madrid inatajwa kuwa klabu iliyoweka nguvu nyingi za kumsajili nyota huyo ambaye anafanya vizuri kwenye msimu huu wa ligi akiwa na Liverpool.